Social Icons

Pages

Wednesday, December 24, 2014

MTANZANIA ASIMAMIA MRADI UJENZI WA BANDARI QATAR


Ndugu Potty Msuku
Serikali ya Qatar inajenga bandari mpya katika eneo la jangwa, mradi unaogharimu Dola za Marekani 80 bilioni na ikimteua raia wa Tanzania asimamie kazi hiyo.
Ujenzi huo unatokana na Serikali ya nchi hiyo kuamua kuhamisha bahari na kuipeleka katika eneo hilo la jangwa. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyemaliza ziara ya kuzitembelea nchi za Falme za Kiarabu juzi usiku, alitembelea mradi huo wa bandari mpya ambao unajengwa eneo la jangwa na baadaye kuelekeza maji ya bahari kufika eneo hilo.
Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa mradi huo, Potty Msuku alisema kazi kubwa anayofanya ni kusimamia na kuhakikisha kazi inakwenda kwa wakati. Alisema bandari hiyo itakayoanza kufanya kazi kuanzia mwakani, ina magati zaidi ya 10 ya kuegeshea meli.
“Ninachoshukuru ni kwamba tuko mbele ya muda tuliopewa, tunakwenda vizuri.”
Mtanzania huyo alisema mpango wa ujenzi wa bandari hiyo mpya ulibuniwa na Serikali ya Qatar ili kufungua lango la biashara kwa mataifa makubwa. Alisema mradi huo ukikamilika utaifanya Qatar kuwa moja ya mataifa yenye bandari kubwa dunia sanjari na mataifa ya Kiarabu, Dubai na Abu Dhabi.
“Tumechimba eneo hili ambalo hadi Aprili mwakani tutakuwa tumepasua mwamba wa bahari na maji yatakuja huku,” alisema.
Alisema ujenzi huo ulioanza 2011 utakamilika 2016.
Msuku ambaye ni mhandisi kitaaluma, alisema ujenzi wa bandari hiyo unakwenda kwa awamu, nyingine inayofuata ni ya kuiunganisha bandari hiyo na reli na uwanja wa ndege utakaojengwa karibu na eneo.
“Kazi kubwa inayoendelea sasa ni ya kuchimba kina, tumefikia pazuri na nyingine ni kujenga eneo la biashara huru na kitengo cha makontena.”
Msuku alisema sehemu kubwa ya wafanyakazi wanaojenga bandari hiyo wengi wanatoka katika mataifa mbalimbali duniani ikilinganishwa na raia wa nchi hiyo.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akipokea taarifa za ujenzi huo, alielezea kuvutiwa na jinsi bahari itakavyohamishiwa jangwani kwa ajili ya bandari hiyo. “Tumesikia nyumbani wanataka kujenga Bandari Bagamoyo, tutakuja, lazima tuendeleze nchi yetu,” alisema. Wakati huohuo, Waziri Mkuu, juzi usiku alihitimisha ziara yake hapa Qatar kwa kukutana na jumuiya ya wafanyabiashara.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: