Social Icons

Pages

Wednesday, December 24, 2014

RAIS HAJAKIDHI KIU YA WANANCHI ESCROW


Juzi, Rais Jakaya Kikwete alitangaza uamuzi wake kuhusu sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ilifunguliwa kutunza fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) kwenda IPTL baada ya kutokea mzozo baina ya pande hizo mbili.
IPTL iliingia mkataba wa kuiuzia umeme Tanesco miaka 20 iliyopita. Lakini mkataba huo ukaingia dosari baada ya Tanesco kufungua mashtaka mahakamani ikidai tozo hiyo ni kubwa, hali ambayo ililazimisha pande hizo mbili kukubaliana kufungua akaunti maalumu ya kutunza fedha hizo hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.
Lakini suala hilo liliisha katika njia ambayo ilizua shaka baada ya taarifa kuvuja kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo zilichotwa kinyemela na kwamba zimelipwa kwa watumishi wa umma, viongozi wa kidini na watu wengine.
Shaka hiyo ndiyo iliyofanya Bunge lihoji na kuamumuru uchunguzi ufanywe na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Takukuru na baadaye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ipitie ripoti hizo na kutoa taarifa bungeni. Baada ya kuwasilisha taarifa yake, Bunge lilijadili na kufikia maazimio manane, yakiwamo ambayo yalimtaka Rais atoe uamuzi kwa mujibu wa mamlaka yake.
Katika uamuzi wake, Rais Kikwete amemuondoa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, bado anasubiri uchunguzi dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na katibu wake, Eliakimu Maswi, wakati Bodi ya Tanesco iliyotakiwa ivunjwe kutokana na ushiriki wake kwenye sakata hilo, imeshamaliza muda wake na hivyo kurahisisha kazi.
Hali kadhalika, suala la kumchukulia hatua Mwanasheria Mkuu, lilishajitatua kutokana na Jaji Frederick Werema kujiuzulu. Rais pia amekataa azimio la kutaifisha mitambo ya IPTL kwa kuwa kitendo hicho kitawatisha wawekezaji wa nje, huku azimio la kuimarisha Takukuru likiendelea kufanyiwa kazi.
Kiu ya wananchi ilikuwa ni kuona sakata hilo linamalizwa kabisa, lakini wengi waliozungumza na vyombo vya habari juzi na jana na kwenye mitandao ya kijamii baada ya hotuba ya Rais Kikwete, wameonyesha kuwa mkuu huyo wa nchi hajakidhi kiu yao.
Wengi walitegemea kuwa angehutubia wakati akiwa na uamuzi kamili kuhusu maazimio yanayomhusu  moja kwa moja baada ya suala hilo kuchukua muda mrefu na kutafuna fedha nyingi za walipa kodi kwa njia moja au nyingine.
Baada ya kuwa na muda mwingi wa kutafakari tangu Bunge lifikie maazimio hayo Novemba 29, ilitegemewa kuwa Rais angekuwa na uamuzi kuhusu Profesa Muhongo kama ilivyokuwa kwa Profesa Tibaijuka, katibu mkuu wa nishati, majaji, suala la uwazi wa mikataba na hata hatua kwa ajili ya kudhibiti hali kama hiyo isitokee hapo baadaye.
Hatua za awali dhidi ya majaji zilitakiwa ziwe zimeshachukuliwa kama kuwasimamisha wakati uchunguzi unaendelea kwa mujibu wa Ibara ya 110 (A) (3).
Si nia yetu kumpangia Rais nini cha kufanya, lakini kunapokuwa na kiu kubwa ya wananchi kujua hatima ya suala zito kama hilo ambalo linahusu mabilioni ya fedha na lililoonekana kugubikwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili kwa viongozi wa juu, hatua ya Rais kutangaza uamuzi, inatakiwa ifanywe wakati kukiwa na majibu ya maswali mengi.
Kwa hali ilivyo sasa, fikra za wananchi ni kuwa suala hilo ndiyo limeshamalizika kama masakata mengine yalivyoisha, yakiwamo ya EPA na Richmond.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: