Mbunge wa Afrika Mashariki (Eala),
Abdullah Mwinyi akipiga kura wakati Bunge la Eala lilipopiga kura kupitisha
azimio la kumuondoa Spika wake, Margret Zziwa madarakani lilipokutana Arusha
jana. Nyuma yake ni Nderakindo Kessy.
Wabunge wa Bunge la Afrika
Mashariki (Eala), jana walimng’oa madarakani Spika, Dk Margret Zziwa baada ya
kukubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Sheria, Kanuni na Madaraka ya Bunge
kuwa amepoteza sifa za kuendelea kushikilia wadhifa huo. Wabunge 36 kati ya 39 waliohudhuria
kikao cha dharura cha Bunge hilo kilichofanyika hapa jana chini ya uenyekiti wa
Kaimu Spika, Chris Opoka-Okumu walipiga kura za ndiyo kukubali hoja hiyo.
Wabunge wawili walipiga kura ya
hapana, wakati mmoja hakupigia kura hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa
Kenya, Peter Mathuki Machi mwaka huu na kuibua mvutano miongoni mwa wabunge
waliokuwa wakimtetea Zziwa na wale waliotaka ang’oke. Uamuzi wa kumng’oa Spika
umechukuliwa kwa kuzingatia Kifungu cha 53(3) cha katiba ya kuanzishwa kwa EAC,
inayowapa mamlaka wabunge kumwondoa ofisini Spika.
Mwenyekiti wa kamati uchunguzi dhidi
ya Spika Zziwa, Frederick Ngenzebuhoro kutoka Burundi alisema madai yote dhidi
ya kiongozi huyo yamethibitika kuwa kweli na kuomba Bunge lipitishe azimio la
kumng’oa madarakani. “Baada ya kuchunguza, kufanya
mahojiano na kukusanya nyaraka mbalimbali zikiwamo barua za Spika Zziwa
mwenyewe, picha za mgando na video, kamati inapendekeza aondolewe madarakani
mara moja kwa kushindwa kutimiza wajibu na matumizi mabaya ya madaraka,”
alisema Ngenzebuhoro katika taarifa yake ya kurasa 18 kuthibitisha tuhuma dhidi
ya Dk Zziwa.
Awali, kabla ya uamuzi huo,
Mwanasheria wa Spika Zziwa, Jet-John Tumwebaze alizungumza na waandishi wa
habari na kudai kuwa kikao cha Bunge cha jana ni batili kwa sababu hakiko
kwenye kalenda na kinaongozwa na Kaimu Spika, cheo alichosema hakipo kikatiba. Alisema kamati iliyochunguza tuhuma
dhidi ya Dk Zziwa haikuwa huru kwa sababu wajumbe 11, kati 15 ni miongoni mwa
waliosaini hati ya hoja ya kumng’oa madarakani.
Mtoa hoja Mathuki alielezea furaha
yake baada ya Bunge kupitisha azimio la kumwondoa madarakani kiongozi huyo. “Nimefarijika kuwa Bunge hili
limethibitisha pasipo shaka kuwa hoja yangu ililenga masilahi mapana ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki na siyo ajenda binafsi kama baadhi walivyojaribu
kupotosha,” alisema Mathuki.
Kwa uamuzi huo, Uganda inapewa fursa
ya kuteua mtu au watu watakaopigiwa kura kushika wadhifa huo kwa sababu kiti
hicho kinashikiliwa kwa kupokezana miongoni mwa nchi wanachama na hii ni zamu
ya Uganda. Katibu wa Bunge, Kenneth Madette anatakiwa kutumia Kifungu cha 7(3),
cha kanuni za Bunge hilo, kutangaza kuwa nafasi ya Spika iko wazi na kutoa fomu
za kugombea kwa wabunge wanaotaka kuwania nafasi hiyo ndani ya saa 48 tangu
kiti kinapobaki wazi.
Tuhuma
Spika Zziwa anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kuwaingiza baadhi ya
ndugu zake akiwamo mumewe kwenye shughuli za Eala wakati siyo wabunge wala
watumishi wa Bunge hilo. Anatuhumiwa kwa upendeleo na ubaguzi miongoni mwa wabunge pamoja na matumizi
ya lugha na kauli za kudhalilisha dhidi ya wabunge na watumishi wa Eala.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment