Social Icons

Pages

Thursday, December 18, 2014

BEI YA SUKARI YAPANDA GHAFLA

Sukari ikiwa imewekwa kwenye mfuko wake tayari kwa kupelekwa sokoni. Kumeibuka sintofahamu miongoni mwa wananchi na wafanyabiashara wa maduka ya rejareja baada ya bei ya sukari kupanda ghafla na kufikia Sh80,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Hali hiyo imesababisha kilo moja iliyokuwa ikiuzwa kwa kati ya Sh1,600 na Sh1,800 sasa kuuzwa kwa Sh2,000 katika maduka ya rejareja na taarifa za wauzaji wa jumla zikisema bei itapanda zaidi wiki hii.
Sehemu kubwa ya sukari inayouzwa mikoa ya kaskazini inatoka kiwanda cha TPC cha mjini Moshi ambacho kimeweka wazi msimamo wake kuwa upungufu wa sasa wa sukari unasababishwa na baadhi ya waagizaji wakubwa wa sukari ya nje ili kuhalalisha hujuma.
Msemaji wa TPC, Jaffar Ally aliliambia gazeti hili jana kuwa kuna vita kubwa inayoendelea kati ya wazalishaji wakubwa wa ndani na wafanyabiashara wanaoingiza sukari toka nje ya nchi.
“Tunachokiona ni kwamba, baada ya Serikali kufuta vibali vya uagizaji sukari, hao wafanyabiashara wameamua kuficha sukari ili ionekane bila sukari ya nje ni lazima bei ipande,” alisema Ally.
Ally alisema licha ya Serikali kutotoa vibali vya uagizaji wa sukari nje ya nchi kuanzia mwaka jana, bado katika soko la Tanzania kuna sukari inayozalishwa nchini Brazil iliyoingizwa nchini Julai na Agosti, mwaka huu. Alisema mwezi uliopita, sukari Dar es Salaam ilikuwa ikiuzwa Sh80,000 kwa mfuko wa kilo 50, hali ambayo ilisababisha wafanyabiashara kufurika Moshi kununua sukari ya TPC.
“Huwezi kuamini jana (juzi) peke yake tumeuza tani 900 kwa siku, wakati wastani wetu ni kuuza tani 320 kwa siku. Tumelazimika kurekebisha bei ili kulinda sukari isihamishiwe yote Dar es Salaam.
“Ili kulinda sukari isiadimike tulipandisha bei ya mfuko kutoka Sh67,000 hadi Sh72,000 ili mawakala wetu wakubwa wakiongeze asilimia 3 basi wauze kwa Sh74,000,” alisema Ally.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, hata baada ya kuongeza bei, bado sukari ilikuwa ikichukuliwa kwa wingi na TPC ikalazimika kupandisha tena hadi Sh76,000 ili muuzaji wa jumla asiuze zaidi ya Sh78,000.
“Hiki kinachoendelea ni njama za kutengeneza uhaba feki wa sukari,” alisema. Mabadiliko hayo ya bei yanadaiwa kufanyika baada ya Serikali kuzuia kwa mara nyingine uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi.
Mfanyabiashara Esther Mgonja anayemiliki duka la rejareja eneo la Pasua katika Manispaa ya Moshi, aliliambia gazeti hili kuwa juzi alinunua mfuko wa sukari wa wkilo 50 kwa Sh80,000. Kwa mujibu wa Mgonja, atalazimika kuuza kilo moja kwa Sh2,000 au zaidi ili asiingie hasara.
Wiki iliyopita, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza aliagiza kufanyika kwa ukaguzi katika bodi ya sukari nchini ili kubaini kama kuna vibali vya sukari vilivyotolewa mwaka jana.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: