Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema pamoja na Tanzania kuwa na uhaba wa hoteli za kisasa kwa ajili ya watalii, Serikali haitaacha kunadi utalii na vivutio vyake vya ndani.
Akizungumza katika Kongamano la Utalii la
ushirikiano wa Tanzania na Dubai, Waziri Mkuu alisema pamoja na hali
hiyo, bado jukumu la Serikali ni kuhakikisha utalii unakua. “Ni kweli tuna uhaba wa vyumba na hoteli, lakini
hatutaacha kutangaza utalii, wapo watalii wengine wanapenda kukaa hata
kwenye mahema na si lazima kukaa hotelini,” alisema. Alisema Serikali kwa sasa inaandaa mpango wa
kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo ya utalii kupitia mpango wa
ushirikiano na Sekta Binafsi maarufu kama PPP.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Devota Mdachi
alisema kwa sasa wameanzisha mpango wa kuitangaza Tanzania kuvutia
watalii zaidi kupitia michezo, ikiwamo Ligi Kuu ya Uingereza. Katika Kongamano hilo, Mdachi alisema ligi hiyo ni
miongoni mwa ligi inayotangazwa na kuvutia wengi duniani, hivyo nguvu
hiyo itasaidia kuitangaza Tanzania.
Hivi karibuni, wachezaji wa Sunderland walivaa
fulana zilizoandikwa ‘Visit Tanzania’ walipokuwa wakipasha misuli moto
kabla ya mpambano wao na Manchester City. Mdachi alisema Tanzania imeweka mkakati wa kuvutia
watalii kwa kualika waandishi wa habari wa kimataifa pamoja na
kushiriki misafara ya kitalii.
Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai, Omar Rajab Mjenga
alisema ni aibu kujitangaza kimataifa kuwa nchi inaingiza watalii
milioni moja kwa mwaka, huku Tanzania ikiwa na vivutio vingi zaidi
duniani. Akizungumza katika mahojiano maalum kwenye Hoteli
ya Kempinsky mjini hapa, Mjenga alisema kuwa mpango wa sasa ni
kuhakikisha kuwa Tanzania inaingiza watalii zaidi ya milioni tatu hadi
kufikia mwishoni mwa 2015.
“Tunatumia njia nyingi kuitangaza Tanzania…kwa
hapa tunaandaa makongamano ya utalii kwa ajili ya kuitangaza Tanzania na
lengo ni kuvutia watalii zaidi,” alisema. Balozi Mjenga alisema kuwa pamoja na kufanya kazi
ya kuvutia watalii, bado Tanzania hakuna hoteli za kitalii za
kutosha...tunatafuta pia wawekezaji kuwekeza katika eneo hili la kujenga
hoteli za nyota tano za kitalii kama ilivyo hapa Dubai,” alisema.
Akitolea mfano, Balozi Mjenga alisema kuwa wananchi wa Dubai
wanatumia fedha zao mifukoni kujenga majengo marefu ya kuvutia ambayo
peke yake ni kivutio cha utalii. Wananchi wamehamasika kujenga na kuwa kitovu cha biashara kwa mji wa Dubai na imekuwa kivutio wengi kuja Tanzania. Akihutubia kongamano hilo, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu aliwataka wawekezaji kuingia Kusini mwa Tanzania
kuwekeza zaidi na kutumia uzoefu wa Dubai kuijenga Tanzania.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment