Rais Jakaya Kikwete amemteua Dk
James Mataragio kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC). Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilisema uteuzi huo ulianza Desemba 15 mwaka huu.
Sefue alisema Dk Mataragio ni Mtanzania ambaye
hivi sasa anaishi na kufanya kazi nchini Marekani, akiwa Senior
Geoscientist wa Kampuni ya Bell Geospace, Houston, Marekani. Kuhusu uzoefu kazini, taarifa hiyo ilisema mwaka
2001/2004 wakati akisoma Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha
Missouri, alikuwa Mhadhiri Msaidizi na mwaka 2000 na 2001 alikuwa
Mhadhiri Msaidizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka 1999/2000 alikuwa
Meneja Mradi, Anglo Gold (Buzwagi).
“Miongoni mwa kampuni kubwa za kimataifa za mafuta
na gesi alizofanya nazo kazi kwa niaba ya mwajiri wake, Bell Geospace
ni pamoja na Petrobras (Brazil), BP, Anadarko, Tullow, Pemex (Mexico),
ANP (Brazil), Ecopetrol (Colombia), Petronas, (Malaysia) na Vale Rio
Doce,” ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza: “Dk Mataragio ni mmoja wa wataalamu wa
sekta ya madini, mafuta na gesi asilia waishio Marekani (Diaspora) ambao
walijitolea kuishauri Serikali kuhusu sekta hiyo bila malipo. Kwa
kuzingatia elimu yake, uzoefu wake na uzalendo wake, Rais (Kikwete) ana
matumiani makubwa kuwa ataleta nguvu mpya na uzoefu mkubwa wa kimataifa
katika kuiongoza TPDC ili iwe kampuni kubwa ya kitaifa ya mafuta na gesi
asilia kama zilivyo kampuni nyingine za gesi asilia duniani.” Wakati huohuo, Rais Kikwete amemteua Willy Kitima
kuwa Msaidizi wake - Nyaraka (Documentation), uteuzi ulioanza Desemba 11
mwaka huu.
Kabla ya uteuzi wake, Kitima alikuwa Mratibu wa
Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya Biashara nchini Business Action
Against Corruption (BAAC) Tanzania.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment