Social Icons

Pages

Friday, December 19, 2014

DK MWAKYEMBE KUWATIMUA KAZI WAZEMBE

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akizungumza na Kaimu Meneja wa Mgodi wa Uchimbaji Kokoto wa Kongolo Uswisi mkoani Mbeya, Juma Michael wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu, juzi.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema hatosita kuwatimua kazi watendaji wabovu wa Shirika ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara) wanaoshindwa kusimamia kikamilifu utendaji kazi wao na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha kwa masilahi binafsi.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi na Kamati ya Bunge ya Miundombinu walipotembelea Mradi wa Mgodi wa kiwanda cha kuzalisha kokoto wa Kongolo uliopo katika Kijiji cha Mswiwi sambamba na kukagua karakana ya Tazara.
Alisema utendaji kazi kwa mazoea ni changamoto ambayo Serikali inapaswa kuisimamia na kuwawajibisha watendaji wataobainika kuisababishia hasara kwa makusudi. Alisema Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa yenye wawekezaji wengi wanaofanya biashara ndani na nje ya nchi na kwamba wanalazimika kusafirisha mizigo yao kwa kutumia magari makubwa ya mizigo huku wakikwepa kutumia reli kwa sababu ya ukubwa wa gharama za usafirishaji.
Mjumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Rebecca Michael Mngodo alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kutenga fedha katika bajeti bungeni ili Tazara iweze kujiendesha yenyewe na kuachana na mvutano uliopo baina ya Tanzania na Zambia hali inayosababisha uchumi wa nchi yetu kuporomoka.
“Jamani sisi wenyewe wabunge tumefika na tumejionea hali halisi ya shirika letu ni hoi na kwamba huko tuendapo tukatafakari nini kifanyike ili tuinusuru na tuangalia mfumo mwingine wa kuiendesha kutokana na wenzetu wa zambia kukata mawasiliano ya ushirikiano”alisema.
Naye Mbunge wa Ileje (CCM) na Mjumbe wa kamati ya bunge Miundombinu ,Aliko Kibona aliomba Serikali kuangalia kwa jicho la huruma swala zima ya upatikanaji wa mishahara ya wafanyakazi ,na huduma za afya kwani hiyo na changamoto kubwa inayowakumba wafanyakazi wa Tazara.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: