Social Icons

Pages

Friday, December 19, 2014

MGOGORO EALA UMEKWISHA, WABUNGE KAZINI


Baada ya shughuli za Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kukwama kwa muda mrefu kutokana na kukumbwa na migogoro, ukiwamo wa wabunge kususia vikao wakitaka Spika Margaret Zziwa ajiuzulu, hatimaye juzi walifanikiwa kumng’oa madarakani wakisema amepoteza sifa za kuendelea kushika wadhifa huo.
Jitihada zote za Dk Zziwa kuzima uasi wa wabunge hao dhidi yake ziligonga mwamba, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Afrika Mashariki kutupilia mbali pingamizi aliloweka mahakamani akipinga Bunge hilo lisimwondoe katika wadhifa wake. Kwa muda mrefu, bunge hilo la tatu lilikuwa halifanyi shughuli zozote zenye tija. Tangu lianze kipindi chake miaka minne iliyopita, tumeshuhudia migogoro mingi isiyo na msingi. Mwaka uliopita, kwa mfano baadhi ya wabunge walisusia vikao wakipinga vinafanyika jijini Arusha pekee.
Kama siyo busara za wakuu wa nchi wanachama, bunge hilo lingesambaratika. Kanuni ziliboreshwa na kuwezesha vikao hivyo kufanyika kwa mzunguko katika kila nchi mwanachama.
Baada ya sakata hilo, ndipo ulipoibuka tena mgogoro kuhusu hoja ya kumng’oa Spika Zziwa kiasi cha kukwamisha shughuli zote za chombo hicho, zikiwamo za uwasilishaji wa bajeti ya jumuiya hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2014/15. Wabunge wengi walitaka Spika Zziwa ang’oke kwa madai kwamba alishindwa kuendesha bunge kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa. Walimtuhumu kwa ubabe, kuwagawa wabunge na kutumia madaraka yake vibaya.
Hata hivyo, alijitetea kwamba chuki dhidi yake zilitokana na msimamo wake wa kukataa matakwa ya wabunge ya kupewa nyongeza kubwa za mishahara na posho. Kwa hivyo, mgogoro huo ndio hasa umekuwa chanzo cha vikao vya chombo hicho kuvunjika au kuahirishwa kutokana na kukosa akidi.
Kama hiyo haitoshi, ulizuka mgogoro mwingine kati ya mmoja wa wabunge kutoka Tanzania na wabunge wengine ambao walitaka mbunge huyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa madai kwamba aliwadhalilisha wakati walipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Ubelgiji.
Bunge lilipokutana Kigali kwa wiki mbili lilishindwa kufanya vikao, kwani wabunge walitaka Spika Zziwa kwanza amchukulie hatua za kinidhamu mbunge huyo kutoka Tanzania badala ya kumkingia kifua. Kilichotokea ni kwamba wenyeviti wanne wa bunge hilo kati ya sita pamoja na makamishna watano kati ya 10 wanaounda Tume ya Uongozi wa Bunge walijiuzulu, wakisema hawakuwa na imani na Spika Zziwa.
Hatua hiyo ilikuza mgogoro huo, kwani hatua ya viongozi hao kujiuzulu ilimaanisha kwamba bunge hilo lisingeweza kufanya shughuli yoyote hadi iundwe upya Tume ya Bunge na kufanya uchaguzi wa wenyeviti wapya. Kazi hiyo isingefanyika pasipo Spika Zziwa, aliyekuwa akipingwa na zaidi ya theluthi mbili za wabunge, kujiuzulu. Inasikitisha kwamba tangu bunge hilo la tatu lianze shughuli zake limepitisha miswada 10 tu, ikilinganishwa na Bunge la Pili lililopitisha miswada zaidi ya 30.
Lakini pia kazi ambayo Bunge lilipanga kuifanya, yaani kurekebisha kanuni zake ili kuwa na uendeshaji mzuri unaozingatia weledi, uwazi na uwajibikaji, ilikwama tangu Aprili, mwaka huu kutokana na migogoro. Spika Zziwa sasa ameondolewa. Ni matarajio yetu kwamba wabunge watachapa kazi na kumaliza viporo vyote vya shughuli walizopaswa kuzifanya. Hatutarajii tena kuona wabunge hao wakiendekeza migogoro badala ya kufanya shughuli zenye tija kwa wananchi wa Afrika Mashariki.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: