Social Icons

Pages

Friday, December 19, 2014

KATIBA NA FURSA MPYA ZA UCHUMI, BIASHARA


Jaji Joseph Warioba.
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado ni habari ya maana zaidi kwa sasa hapa nchini. Bahati mbaya sana wapo Watanzania wengi tu, ama kwa ujinga wa kutojua au tu kwa kutojali, hawakufuatilia mchakato huu kwa karibu na kwa umakini.

Na ukweli siku zote unauma, lakini pasipo kufanya utafiti unaweza kushangaa watu wanaojua ratiba ya ligi ya (Premium League) ya Uingereza, ile ya Ujerumani (Bundersliga) lakini wasijue chochote kuhusu yale yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba ama namna mchakato wa Katiba mpya unavyoendelea. Si nia ya safu hii kuhukumu fikra za watu, lakini inatosha tu kusema kwamba, kwako wewe msomaji wetu mpendwa unayefuatilia safu hii, kufahamu kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya yale yanayokuwamo ndani ya Katiba ya nchi (pamoja na utekelezaji wake) na maendeleo katika sekta takribani zote za uchumi na biashara.

Tunaamini kwamba pale tuhitimishapo safu hii kwa leo, utabaini sasa kwa nini Katiba mpya inayozingatia maoni ya wananchi itakuwa ni nuru mpya kwa mwekezaji, mfanyabiashara ama mjasiriamali aliyeko nchini na hata mwekezaji anayeingia ndani ya nchi kwa lengo tu si la kuweka mirija ya kunyonya Watanzania, bali kwa nia njema ya kutumia ujuzi ama mtaji alionao kushirikiana na Watanzania wanaomkaribisha ili kusaidiana si tu kumwongezea faida, lakini pia na yeye kutoa mchango wake katika kuinua uchumi wa nchi na kuinua ubora wa maisha wa raia wanaomkaribisha nchini. Ni kweli pia Katiba si mwarobaini lakini kama itapitishwa itatibu magonjwa mengi, tena zaidi ya hiyo 40. Baada ya utangulizi huu turejee sasa katika mada yetu.
Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 pamoja na Rasimu ya Pili ya Tume ya Warioba zote zimeyagusia masuala ya kiuchumi na biashara, ingawa kwa maneno na msisitizo tofauti. Zote mbili zinaelezea juu ya malengo ya nchi pamoja na kutambua ushirikishwaji wa wananchi na wadau wengine katika kuinua uchumi, biashara, kujenga jamii yenye usawa na pasipo kuwa na unyonyaji, utumwa na kadhalika.

Mathalani, Rasimu ya Katiba imeyagusia mambo haya katika ibara tofauti tofauti: Tunu za taifa (Ibara ya 5) ambamo masuala kama utu, uwazi na uwajibikaji yametajwa. Ibara ya 6 ya Rasimu inawapa wananchi mamlaka ambapo ibara hii ni njema kwa sababu Serikali itapaswa kuwajibika kwa wananchi (Ibara 5(c ) na kwamba lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi (ibara 5(b)).

Ibara nyingine za Katiba Mpya inavyopaswa kuwa Kulingana na Rasimu ya Warioba ina vipengele vya haki za Binadamu vilivyosheheni Sehemu yote ya Kwanza katika Sura ya Nne ya Rasimu (Ibara ya 22-47). Baadhi ya vile vilivyo na uhusiano wa moja kwa moja na fursa za kikazi, kiuchumi na kibiashara kwa kila mwananchi wa Tanzania ni pamoja na kuharamishwa kwa ubaguzi wa aina yoyote ile (kwa mujibu wa Ibara 24) na pia ya Haki ya Kutokuwa mtumwa (Ibara ya 25). Nyingine ni pamoja na haki za wafanyakazi na waajiri (Ibara ya 35) na pia haki ya kumiliki mali (ibara ya 36).

Mambo mengine yanayohusika na fursa za kimaendeleo ya kiuchumi/kibiashara ndani ya Rasimu ya Katiba ni pamoja na Haki ya Elimu na kujifunza (Ibara ya 4), na pia haki na wajibu wa makundi maalum ya kijamii kama vijana, ambao ndiyo nguzo kuu ya kiuchumi ambayo bado haijatumika vema hapa nchini (ibara ya 43), wenye ulemavu (ibara ya 55), haki za makundi madogo katika jamii (ibara ya 45), haki za wanawake (ibara ya 46) na kadhalika. Labda unaweza kujiuliza, mbona mambo yote haya yapo ndani ya Katiba tunayoitumia sasa tangu mwaka 1977? Jibu ni rahisi. Ni kweli kwamba, mengi kati ya haya yamo lakini kwa namna yalivyoandikwa ndani ya Katiba ya sasa, utekelezaji wake ni mgumu na mara nyingi imehitaji tafsiri za mahakama kueleza kama haki fulani imekiukwa ama la.

Na pili ufuatiliaji haki yenyewe pale mwananchi anapovunjiwa kile kilichomo ndani ya Katiba una masharti magumu na yenye utata hata miongoni mwa wanasheria waliobobea. Mathalani iwapo haki ya msingi inavunjwa raia anapaswa kutoa notisi (taarifa) ya angalao siku 90 kwa Mwanasheria Mkuu kabla hajaruhusiwa kuifungulia shauri Serikali mahakamani kwa mujibu wa Sheria ya Mashtaka dhidi ya Serikali iliyo kwa jina la Kiingereza kama Government Proceedings Act.

Awali kabla ya mwaka 1993 hali ilikuwa ngumu zaidi kwa sababu ilibidi kwanza, yule anayeamini haki yake imevunjwa kuiomba kwanza idhini serikali, kwamba anataka kuiburuza mahakamani na hadi hapo ambapo Serikali ingekubali kupitia Mwanasheria wake Mkuu, basi shtaka la aina hilo lisingekuwa na mashiko. Bahati nzuri kidogo, Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na ile ya Rufaa zikatamka kuwa, Sheria hii ilikinzana na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya sasa, ambayo inatoa haki ya mtu yeyote kudai haki, ama nafuu yoyote ya kisheria kupitia Mahakama.

Hukumu mbili muhimu zilizoifafanua haki hii, ni ile ya Peter Ng’omango dhidi ya Gerson Mwangwa (Shauri la madai ya Kikatiba la mwaka 1993) pamoja na ile ya Kukutia Ole Pumbun na mwenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (iliripotiwa mwaka 1994). Hata hivyo, mhimili wa mahakama ukawa umeacha sharti la siku 90 za kutoa taarifa kabla ya kushtaki.
Katiba mpya, italiweka suala hili wazi zaidi na hata kutokana na mkanganyiko ambao umeendelea kuwapo katika kuleta mashtaka ya ukiukwaji haki kwa sababu Katiba yenyewe, Sheria iitwayo Government Proceedings Act (1994), Sheria ya Utekelezwaji wa Haki Muhimu ya mwaka 1994 (inaitwa Basic Rights and Duties Enforcement Act) pamoja na uwezo wa mahakama kutoa amri kwa kufuata Kanuni maalum (Kijadi huitwa Writs ama zijulikanavyo Tanzania kama Prerogative Orders) zitumiwazo kubatilisha maamuzi ya vyombo vya ki-utawala ama vinavyokiuka haki za watu.

Amri hizi ni kama habeas corpus (Amri ya kumtoamtu kiuzuizini kama yuko hapo kinyume cha sheria), mandamus (kuagiza mtendaji ama mamlaka fulani kutekeleza wajibu wake kisheria), certiorari mandamus (kubatilisha kitendo au uamuzi wa mtendaji ama mamlaka fulani kwa kuwa kinyume kisheria ama katika misingi ya haki) pamoja na prohibition (kuzuia mamlaka au mtendaji kufanya jambo fulani). Bado kanuni hizi muhimu sana zimeendelea kutatiza vichwa vya wanasheria na hata majaji, katika utoaji wa haki za msingi za raia.
Katiba ya nchi, ifafanuapo mambo haya kwa uwazi na kutamka bayana utaratibu rahisi wa kudai haki ukiukwaji utokeapo basi hata matukio kama kiburi ama kubweteka, miongoni mwa watendaji wa umma kunakoambatana na ukikukwaji wa haki za raia kama vile ucheleweshwaji makusudi wa hata tu leseni za biashara, basi ustawi wa nchi kiuchumi unakuwa umewekewa mbolea bora.

Mfano halisi wa jambo hili ulitokea katika kesi ya Naila Majid Jiddawy, mwanasiasa maarufu mwanamke wa Zanzibar ambaye mwaka 994 alipokonywa leseni yake ya biashara, kwa sababu za kujihusisha na harakati za chama cha upinzani cha CUF. Hakuridhika na akaenda mahakamani kudai kuwa, haki zake za msingi za kumwezesha kuishi kupitia fursa za kiuchumi ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 zilikuwa zimekiukwa. Hili lilikuwa shauri namba 30 la mwaka 1994 lililofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Kesi nyingine muhimu za Katiba zinazogusa masuala ya kiuchumi na biashara zilizowahi kuamriwa hapa nchini, ni pamoja na ile ya Lohay Akoonaay Dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (fursa za kiuchumi kupitia ardhi), Simeon Manyaki dhidi ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha, IFM; Mahona dhidi ya Baraza la Utawala la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kesi maarufu ya MWATEX (haki ya ajira).

Hukumu nyingine muhimu za ki-katiba zilizohusika na fursa za kiuchumi hapa Tanzania ni pamoja na Sisya v. Mwanza Township Council (haki za kibiashara kupitia leseni) pamoja na ile ya BAWATA (ikiongozwa na Prof. Anna Tibaijuka wakati ule) dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (haki ya kujiunga na makundi maalum) kwa shughuli za kijamii au maendeleo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: