Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein akizindua mradi wa umeme
katika Kijiji cha Dongongwe, Mkoa wa Kusini Unguja.
Akihutubia katika uzinduzi huo, Dk Shein alisema
Serikali ina wajibu wa kuwapa wananchi huduma bora za kijamii, kiuchumi
na maendeleo wananchi. Akinukuu ibara ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984, Dk Shein alisema: “Kwa madhumuni ya kuendeleza umoja na
maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika nchi, itakuwa ni wajibu wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa huduma za kutosha kwa ajili ya
kuendeleza watu.”
Alisema maendeleo ni mchakato na ni jambo ambalo
halikamiliki kwa siku moja, badala yake huenda hatua kwa hatua, hivyo
Serikali itaendelea kupeleka huduma nyingine zilizobaki kijijini humo,
ikiwamo barabara akiahidi kuwa itajengwa hatua kwa hatua. Alisema maendeleo hayachagui mtu wala eneo
analotoka, hivyo Serikali anayoiongoza itahakikisha inawapelekea
maendeleo wananchi wote bila kujali itikadi zao kwani hilo ndilo jukumu
la Serikali na pia ni malengo ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ya
Zanzibar .
Dk Shein alisema jitihada za kupeleka umeme vijijini ni kubwa kwa upande wa Unguja na Pemba na kusisitiza ingawa
Zanzibar ni nchi ya mwanzo katika Afrika Mashariki kuwa na umeme toka
mwaka 1875, lakini sio watu wote waliobahatika kuupata.
Akitoa historia ya huduma hiyo Zanzibar, Dk Shein
alisema matumizi rasmi ya umeme kwa kisiwa cha Unguja yalianza mwaka
1908 na kwa kisiwa cha Pemba ni mwaka 1959 na kusema kuwa wananchi wengi
walianza kupata huduma ya umeme baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari
12, mwaka 1964. Dk Shein alisema hayo ndiyo yaliyoleta maendeleo ikiwamo
kusambaza huduma za umeme kwa wananchi.
Aliongeza kuwa watawala wote walioitawala Zanzibar
wakiwemo Wareno na Sultan kutoka Oman ambaye ametala zaidi ya miaka 100
hawakupeleka umeme katika kijiji hicho cha Dongoongwe lakini Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Chama cha Mapinduzi kimepeleka huduma
hiyo na nyenginezo. Alisema kuwa hatua kubwa za maendeleo hapa
Zanzibar zimefanywa kutokana na Sera za ASP na sasa ni CCM chama ambacho
kimekuwa kikitekeleza Sera na Ilani yake. Aidha, Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa shirika la umeme Zanzibar
ZECO, Wizara husika pamoja na wananchi wa kijiji hicho na viongozi wao.
Katika sherehe hizo za uzinduzi Dk. Shein alitoa
wito kwa wananchi wa Dongongwe kuitumia huduma hiyo ya umeme kama
inavyotakiwa kwa lengo la kuwapatia maendeleo pamoja na huduma zao
nyenginezo za kijamii. Dk. Shein katika Sherehe hizo za uzinduzi wa umeme
kijijini hapo, alitoa vyeti maalum kwa viongozi wa Kamati za Umeme
katika Jimbo hilo la Uzini huku sherehe hizo zikipambwa kwa tenzi na
ngoma ya maubwa ambayo ilitoa burudani safi.
Nae Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi Mhe. Ramadhan
Abdalla Shaaban alisema kuwa hayo yote ni Matunda ya Mapinduzi kwani
bado yanaendelea na kusisitiza kuwa umeme si anasa ni kitu muhimu hivyo
ni lazima kitumike hasa katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia.
Mapema Mkurugenzi wa Shirika la umeme Zanzibar
ZECO Bwana Hassan.. alisema kuwa Sera ya Serikali ya Mapindyuzi ya
Zanzibar ni kuhakikisha kuwa inawasogezea huduma za kijamii wananchi
wake popote walipo na kazi hiyo ni endelevu hadi Serikali ihakikishe
wananchi wote wanafikiwa na huduma zote muhimu ikiwemo umeme.
Alisema kuwa gharama zilizotumika katika kupelekea
umeme kijijini hapo ni shilingi milioni 100,480,500.00 ambapo kati ya
fedha hizo Shirika limechangia jumla ya shilingi milioni 85,480,500.00
na Mbunge wa Jimbo hilo amechangia shuilingi milioni 15,000,000.00. Alieleza kuwa kazi ziliyofanywa ni pamoja na
ujenzi wa njia kubwa ya umeme ya mkondo wa kilovoti 33 yenye urefu wa
kilomita 2.7, uwekani wa vitop viwili vya transfoma zenye uwezo wa
100KVA kwa Ghana na 50 KVA kwa Dongongwe, ujenzi wa njia ndogo zenye
urefu wa kilomita 2.5 pamoja na malipo ya fidia ya vipato shilingi
milioni 18,614,7000.00 huku akiwataka wananchi wa kijiji cha Mkuku
kujiandaa kupata huduma hiyo hivi karibuni.
Katika risala yao wananchi wa Dongongwe walisema
kuwa wanakamilisha safari ndefu ya kusaka umeme na wanakuwa kijiji cha
mwisho katika jimbo la Uzini kupata umeme na kutoa shukurani kwa
Serikali, Shirika la Umeme, pamoja na viongozi wao wa Jimbo akiwemo
Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Mohamed Seif Khatib.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment