Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party
(TLP), Augustine Mrema, amesema hata kama vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimefanikiwa kumwangusha kwenye
kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, bado
ana nguvu ya kuendelea kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na wala
hajakata tamaa ya kukisuka upya chama chake.Mrema aliangushwa katika kiti hicho na hasimu wake kisiasa, James
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi,
aliyevunja rekodi ya kupata kura nyingi kwa upande wa wabunge wa
upinzani, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa kura 60,187 dhidi ya
6,416 alizoambulia Mrema (TLP) aliyekuwa akishikilia jimbo hilo huku
mgombea wa CCM, Innocent Shirima, akipata kura 16,097.
Alikuwa akihojiwa jana na kituo kimoja cha redio mkoani Kilimanjaro
kuhusu majaliwa yake kisiasa, baada ya yeye na chama chake kukosa
uwakilishi kwenye Bunge na Halmashauri za Wilaya. Mbali ya kupoteza kiti
cha ubunge, TLP haikuambulia hata kiti kimoja cha udiwani.
“Chama changu hakifi na wala sijakata tamaa, tutaanza moja na
ninawaomba wanachama wa TLP watulie…Nitashirikiana na Rais ajaye
aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), na tutakijenga chama
chetu…Hata Dk. John Magufuli, anajua mimi ni mchapakazi na alinipigia
debe na wananchi wakapuuza,” alisema Mrema.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro wenye majimbo tisa ya uchaguzi, viti
saba vya ubunge vimenyakuliwa na baadhi ya vyama vinavyounda Ukawa vya
Chadema na NCCR-Mageuzi, huku majimbo mawili ya Mwanga na Same
Magharibi, yakiangukia CCM.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Chadema iliyovuna wabunge sita na
NCCR-Mageuzi yenye mbunge moja mkoani Kilimanjaro, sasa zitaunda
halmashauri tano za wilaya ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Rombo,
Moshi Vijijini na Vunjo; wakati CCM ikiwa imeambulia Halmashauri mbili
za Mwanga na Same.
Majimbo hayo na idadi ya kata ambazo Chadema na NCCR-Mageuzi zitaunda halmashauri zake ni kama ifuatavyo; Moshi Mjini, Chadema imeshinda Kata 19 kati ya 21 na CCM imepata
Kata mbili za Bondeni na Kilimanjaro, wakati Jimbo la Hai, Chadema
imeshinda kata 16 kati ya 17, ambapo Kata moja ya Bomang’ombe ndio pekee
haijafanya uchaguzi kutokana na mgombea wa CCM kufariki dunia wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu.
Aidha, Chadema iliyoshinda kata 27 kati ya 28 za Wilaya ya Rombo,
ndiyo itakayounda halmashauri ya wilaya hiyo, huku NCCR-Mageuzi
iliyoshinda kata nane, kati ya 16 na Chadema iliyoshinda viti 15 vya
udiwani katika Jimbo la Moshi Vijijini, sasa zitaunda Halmashauri moja
ya Wilaya ya Moshi.
Katika Jimbo la Moshi Vijijini, CCM imeshinda kata moja tu.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment