
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),
umelaani kuvamiwa na kukamatwa kwa wafanyakazi 36 wa Kituo cha Uangalizi
wa Uchaguzi (TACCEO).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema kitendo hicho ni kinyume
cha utawala bora, kwani kituo hicho kilipewa kibali cha uangalizi wa
uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kimekuwa kikifanya
kazi hiyo kila kunapokuwa na uchaguzi na kutoa ripoti za uchaguzi na
kasoro zilizojitokeza.
Alisema asasi za Tanzania zimeendelea kufuatilia mchakato wa
uchaguzi mkuu 2015 tangu uandikishwaji wapigakura, uhamasishaji hadi
kampeni kwa umakini na kwamba tukio hilo la uvamizi ni la pili baada ya
la mkoani Njombe waangalizi wa uandikishaji wapigakura kuvamiwa na
kupigwa na polisi.
"Kitendo cha kuhisi kuwa TACCEO wanakusanya na kutoa matokeo ya
uchaguzi na kuwavamia kimefanywa na Jeshi la Polisi siyo kwa hiari yao
bali kwa shinikizo la wanasiasa hasa walioshiriki mchakato wa uchaguzi
mkuu," alisema na kuongeza:
"Taarifa zetu za kiuchunguzi zinaonyesha kuwa, kulikuwa na
mawasiliano mengi siku hiyo kati ya vyombo mbalimbali ikiwamo Kurugenzi
ya Azaki (asasi za kiraia) iliyopo Wizara ya Maendeleo, Jinsia na Watot
na siku hiyo hiyo askari walikwenda TGNP -Matandao lakini hawakufanikiwa
chochote na kisha kwenda TACCEO."
Olengurumwa alisema hali hiyo ni viashiria vibaya kwa mustakabali
wa Azaki nchini na kwamba vyombo vinavyopaswa kuwa mtetezi wa asasi hizo
vinakuwa sehemu ya kudidimiza uhuru wake.
Alilitaka Jeshi la Polisi kutokubali kutumiwa na baadhi ha vyama
vya siasa/wanasiasa, kwani kufanya hivyo kunawanyima raia haki zao za
msingi za kushiriki masuala ya umma na kupunguza uhuru wa asasi za
kiraia katika utendaji kazi zake.
"Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola vifuate kanuni za
demokrasia na utawala wa sheria na kuheshimu mikataba mbalimbali ya
kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama ili kulinda amani na utulivu
nchini," alisema.
Aidha, Olengurumwa alitoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi na Umoja
wa Mataifa kuendelea kutoa ushauri na kuingilia kati vitendo vya
ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu vilivyojitokeza katika mchakato
mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu vinavyorudisha nyuma demokrasia,"
alisema.
Waangalizi hao walivamiwa Oktoba 29, mwaka huu, katika eneo la
Kawe, jijini Dar es Salaaam na baadhi ya wafanyakazi na vifaa ikiwamo
komyuta mpakato mbili, kampyuta za kawaida 36 na simu zao kukamatwa.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment