Uchaguzi wa Tanzania umeingia katika wasiwasi baada ya visiwa vya
Zanzibar kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi kutokana na dosari, hali
iliyozusha hofu visiwani humo.
Lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania - NEC imesisitiza kuwa
kura za visiwani Zanzibar ni halali na ikaendelea kutoa matokeo, huku
matokeo kamili ya kura za rais yakitarajiwa kutangazwa leo.
Vyama vya upinzani pia vimedai kutokea wizi katika uchaguzi huo mkuu
uliofanyika Jumapili iliyopita, ambao unaonekana kuwa kinyang'anyiro
kikali kabisa kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki,
ambako chama tawala CCM kinakabiliwa na ushindani wa kwanza mkubwa baada
ya miongo kadhaa ya kutawala.
Tume ya uchaguzi ya Zanzibar - ZEC imesema uchaguzi wa visiwani humo -
ambako wapiga kura 500,000 pia walipiga kura ya kumchagua rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - lazima urudiwe kutokana na ukiukaji wa
sheria za uchaguzi.
Wakaazi wazungumzia uamuzi wa ZEC
Mwangwi wa uamuzi huo wa ZEC unaendelea kuakisika vichwani na
vinywani mwa wananchi wengi wa kawaida. Mwandishi wetu Mohammed Khelef
ametembelea mitaa ya mji wa Zanzibar, kutathmini athari za uamuzi huo
kwenye masuala ya umoja wa kitaifa, hali za kimaisha na usalama wa raia.
Katika mji wa Fuoni unaokuwa kwa kasi, kando ya kitovu cha mji wa
Zanzibar, umbali wa kilomita 5 kuelekea kusini mashariki mwa kisiwa cha
Unguja. Khatib Mohammed ni mmoja wa wakaazi: “Naam, kabla ya uamuzi wa
jana wa kufutwa matokeo, siku tatu kuelekea za nyuma yake zilikuwa refu
mno kwa namna zilivyojaza wasiwasi, mashaka na jakamoyo ndani ya nafsi
za watu“.
Kama ilivyo kwa Khatib Mohammed, naye Bi Mwantumu Juma anadhani ikiwa
kuna chochote kilicholetwa na hatua hii, basi ni kuendeleza wasiwasi
nyoyoni mwa watu na hivyo kuongeza ugumu wa maisha kwa walio wengi:
Mbali na athari hiyo kwenye maisha, wote wawili, Khatib na Mwantumu,
wanakubaliana kuwa hatua ya kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kutaigusa
moja kwa moja serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na maridhiano ya
Wazanzibari, ambayo pamoja na yote, yalisimamiwa na serikali inayomaliza
muda wake sasa. Kwa wote wawili, kitendo cha Mwenyekiti wa ZEC kufuta
uchaguzi wa Zanzibar, kimerejesha upya uhasama wa kijamii uliokuwa
ukijaribiwa kuzikwa na uongozi unaoondoka madarakani sasa:
Marekani yakosoa uamuzi wa ZEC
Hapo jana, ubalozi wa Marekani ulitoa kauli yake kupitia
taarifa kwa vyombo vya habari, ukisema kuwa serikali ya Marekani
imeshitushwa na hatua hiyo ya mwenyekiti wa ZEC, ikitoa wito wa kufutwa
kwa kauli yenyewe na pande zote husika kurejea kwenye mchakato wa
kidemokrasia na kuukamilisha uchaguzi ambao waangalizi wa Umoja wa
Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika,
SADC, walikuwa wamesema uliendeshwa kwa amani na ustaarabu mkubwa.
Bwana Abdullah Juma anaamini kuwa bila ya jambo kama hilo kutendeka,
thamani ya kura yake itakuwa haikuheshimiwa, na jitihada zake za kuamka
alfajiri ya Jumapili ya tarehe 25 Oktoba kwenda kupanga foleni ya kupiga
kura, zitakuwa zimechukuliwa kama hazina maana yoyote kwa kura yake
kuwa miongoni mwa zile zilizofutwa:
La kutokuthaminiwa kwa muda wake, ndilo pia analosema Bi Mwantumu Juma,
ingawa yeye akienda mbali hadi kwenye uchaguzi ujao, na tangu leo
akitilia shaka ushiriki wake kwawo:
Kwa vyovyote iwavyo, mwangwi wa uamuzi huu wa mwenyekiti wa tume ya
uchaguzi ya Zanzibar utaendelea kuakisika siku kadhaa miongoni mwa
wananchi hapa Zanzibar, kama si miezi na miaka, endapo tu hakutakuwa na
jitihada za makusudi na za haraka kuukwamua mkwamo wa kisiasa na
kisheria ambao kwa mara nyengine visiwa hivi vya marashi ya karafuu
vimejikuta vikiingizwa. Na kama anavyosema Bwana Abdullah Juma wa Fuoni,
ili uchaguzi usiwe sehemu ya mateso kwa Wazanzibari, bali sehemu ya
mchakato wa kawaida wa kidemokrasia.
CHANZO: DW
No comments:
Post a Comment