Watanzania wapiga kura
Uchaguzi kwa jumla ulifanyika kwa amani. Lakini kabla matokeo rasmi
kutangazwa tume ya uchaguzi kisiwani Zanzibar ilibatilisha matokeo ya
uchaguzi huo.Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Andrea Schmidt anatoa maoni yake.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania umefanyika uchaguzi
ambapo wagombea -John Magufuli wa CCM na Edward Lowasa wa upinzani
walienda takriban sambabamba na hivyo kuwepo uwezekano mkubwa wa chama
cha CCM kuondolewa madarakani baada ya kutawala kwa muda wa zaidi ya
nusu karne.
Uchaguzi waTanzania ungeliweza kuwa mfano barani Afrika. Baada
ya mabadiliko ya mamlaka yaliyofanyika kwa amani nchini Nigeria,
Tanzania ingeliweza kuwa mfano mwingine wa kutia moyo wa maendeleo ya
demokrasia barani Afrika.
Lakini siku moja tu baada ya watu kupiga kura ,umoja wa vyama vya
wapinzani,UKAWA ulitoa madai kwamba chama cha mapinduzi kilifanya
udanganyifu mkubwa wa kura! Ukawa inataka kura zihesabiwe tena.
Hali nchini Tanzania ni ya wasi wasi mkubwa. Kila upande umesimama
kidete.Hakuna anaekubali kushindwa. Kila upande unadai kuwa mshindi.
Swali sasa ni iwapo kura zitahesabiwa tena au chama tawala,CCM kitasonga
mbele kwa nguvu zote na hesabu za sasa, na kujitangaza mshindi wa
uchaguzi?Na ikiwa kweli kura zitahesabiwa tena nani atahakikisha kwamba
kazi hiyo itafanyika kwa njia ya uwazi ili kila upande uweze kuridhika
na matokeo?
Mvutano kisiwani Zanzibar
Hali ya kisiwani Zanzibar pia ni ya mvutano.Wagombea wakuu wa uchaguzi, Rais Ali Mohamed Shein wa Chama cha Mapinduzi na Seif Sharif Hamad wa
chama cha upinzani CUF, pia walienda sambamba.
Chama hicho kikuu cha upinzani,kisiwani Zanzibar ,tayari kilishalalamika
juu ya udanganyifu mkubwa katika chaguzi za miaka ya 1995, 2000 na
2005.Chama hicho kilihisi kuwa kiliibiwa ushindi.
Wakati watu walipojiandikisha kupiga kura palikuwapo na vitisho na wale
wanaounga mkono upinzani walishambuliwa .Hata hivo kwa jumla katika siku
ya kupiga kura mambo yalikuwa shwari kisiwani Zanzibar.
Matokeo yabatilishwa
Baada ya Kiongozi wa upinzani Seif Sharif Hamad Jumatatu kujitangaza
mshindi, na kuitaka tume ya uchaguzi safari hii iutambue ushindi wake,
wanajeshi na polisi waliizingira tume ya uchaguzi. Waangalizi wa
kimataifa pia walifungiwa ndani ya ofisi ya tume hiyo kwa masaa kadhaa.
Yumkini hatua yake ya kujitangaza mapema kuwa mshindi ilimrudisha nyuma
.Kazi ya kuhesbu kura ilisuasua na tume ya uchaguzi ilitangaza kwamba
palikuwapo na udanganyifu mkubwa wa kura uliofanywa na wapinzani na
kwamba Sharif alijitangaza mapema kuwa mshindi. Kwa hivyo matokeo
yamebatilishwa na kwamba uchaguzi mwingine ufanyike mnamo muda wa siku
90.
Lakini chama cha upinzani kinaupinga uamuzi huo na kimesimama kidete na kushikilia kuwa ni mshindi.
Katika mazingira hayo ya mvutano jambo la kipaumbele ni kudumisha amani.
Jumuia ya kimataifa inao wajibu wa kuzishinikiza pande zote ilikuepusha
mambo kuwa mabaya zaidi. Hayo hayapaswi kutokea katika nchi kama
Tanzania ambayo kwa miaka yote imekuwa nanga ya utulivu na pepo ya
amani.
CHANZO: DW
No comments:
Post a Comment