
Katuni.
Sheria ya Makosa ya Mitandao ilianza kutumika nchini
jana baada ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete.
Maana yake sasa usimamizi wa utekelezaji wa sheria hiyo utafanywa na vyombo vya dola yaani Jeshi la Polisi na Mahakama.
Sheria hiyo kabla ya kusainiwa na kuanza kutumika ililalamikiwa na
makundi mbalimbali na kuzua mjadala mkali miongoni mwa wananchi, ambao
wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kwa shughuli zao mbalimbali za
kila siku.
Miongoni mwa maeneo yanayoguswa na sheria hiyo ni pamoja na kusambaza ujumbe wa uchochezi kupitia mitandao ya kijamii. Serikali iliandaa sheria hiyo kwa kueleza kuwa ina lengo la
kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ikiwamo ya Watsapp,
Facebook, Youtube, Instagram na mingine.
Pamoja na maelezo hayo ya serikali kwamba lengo la kutungwa kwa
sheria hiyo ni mazuri, lakini makundi kadhaa ya kijamii hayakuridhishwa
na maelezo hayo na kuendelea kuhoji kuhusiana na kuandaliwa kwa sheria
hiyo pamoja na kusainiwa na Rais kuwa sheria kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Kuna watu wanaamini kuwa lengo la sheria hiyo ni kudhibiti uhuru wa
maoni ya wananchi na hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi huo
wa Rais, wabunge na madiwani.
Watu hao wanaamini hivyo kutokana na moja ya vifungu vya sheria
hiyo kupiga marufuku ujumbe wa uchochezi ama ushawishi wa kisiasa
unaoweza kuleta athari kwa jamii kupitia mitandao.
Pia, sheria hiyo inabana kuhusu masuala ya kusambaza au kutunga
ujumbe unaoleta uchochezi wa kidini unaoweza kusababisha kuvuruga amani
na maelewano ndani ya jamii kupitia mitandao.
Sheria hiyo inaeleza wazi kwamba, wavunjaji wa sheria hiyo wanaweza
kukabiliwa na vifungo vya gerezani au faini ya fedha isiyopungua Sh.
milioni tano kulingana na kosa lililofanyika.
Kutokana na ukweli kuwa sheria yenyewe ilishapitishwa na wabunge,
ni vizuri sasa Watanzania wakazingatia utekelezaji wake ili kujiepusha
na adhabu zake.
Mathalani, matumizi ya mitandao yamekuwa ya kiwango cha juu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu. Mitandao hiyo imekuwa ikitumika kwa njia mbalimbali ikiwamo kampeni
miongoni mwa wagombea, lakini pia kuna baadhi ya watu wamekuwa
wakiitumia kuwashambulia wenzao.
Kadhalika, mitandao hiyo imekuwa ikitumika vibaya na kuwazushia
mambo, kuwatukana na kuwadhalilisha watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa
kitaifa.
Pamoja na ukali wa sheria yenyewe, ni vizuri wananchi wakaisoma na
kuielewa vizuri ili kujiepusha na matatizo yanayoweza kuwakuta huko
mbele ya safari.
Tunaelewa kuwa sheria hiyo ni kali na inadhibiti baadhi ya maeneo
na hasa yale ya utoaji wa maoni, lakini pia inabidi tukubali kuwa Taifa
letu katika kipindi hiki linahitaji miongozo ya kudumisha amani na
utulivu.
Tunasisitiza kuwa ni bora wananchi wakaisoma vizuri sheria hiyo na
kuielewa kwa kuwa atakayefanya makosa atamshughulikia bila kusamehewa
kwa kuwa kutojua sheria siyo utetezi.
Tunaamini kuwa kwa kuwa serikali ilishasema kama yataonekana
mapungufu wakati wa utekelezaji wake itakuwa tayari kuipitia, ni vizuri
itekeleze ahadi hiyo kwa kuwa upitishaji wake uliacha maswali mengi
kuliko majibu kutoka kwa wananchi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment