Social Icons

Pages

Wednesday, September 02, 2015

WATU WASOME SHERIA YA MITANDAO KUEPUKA MATATIZO

Katuni.
Sheria ya Makosa ya Mitandao ilianza kutumika nchini jana baada ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete.
Maana yake sasa usimamizi wa utekelezaji wa sheria hiyo utafanywa na vyombo vya dola yaani Jeshi la Polisi na Mahakama.
Sheria hiyo kabla ya kusainiwa na kuanza kutumika ililalamikiwa na makundi mbalimbali na kuzua mjadala mkali miongoni mwa wananchi, ambao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kwa shughuli zao mbalimbali za kila siku.
Miongoni mwa maeneo yanayoguswa na sheria hiyo ni pamoja na kusambaza ujumbe wa uchochezi kupitia mitandao ya kijamii. Serikali iliandaa sheria hiyo kwa kueleza kuwa ina lengo la kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ikiwamo ya Watsapp, Facebook, Youtube, Instagram na mingine.
Pamoja na maelezo hayo ya serikali kwamba lengo la kutungwa kwa sheria hiyo ni mazuri, lakini makundi kadhaa ya kijamii hayakuridhishwa na maelezo hayo na kuendelea kuhoji kuhusiana na kuandaliwa kwa sheria hiyo pamoja na kusainiwa na Rais kuwa sheria kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Kuna watu wanaamini kuwa lengo la sheria hiyo ni kudhibiti uhuru wa maoni ya wananchi na hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi huo  wa Rais, wabunge na madiwani.
Watu hao wanaamini hivyo kutokana na moja ya vifungu vya sheria hiyo kupiga marufuku ujumbe wa uchochezi ama ushawishi wa kisiasa unaoweza kuleta athari kwa jamii kupitia mitandao.
Pia, sheria hiyo inabana kuhusu masuala ya kusambaza au kutunga ujumbe unaoleta uchochezi wa kidini unaoweza kusababisha kuvuruga amani na maelewano ndani ya jamii kupitia mitandao.
Sheria hiyo inaeleza wazi kwamba, wavunjaji wa sheria hiyo wanaweza kukabiliwa na vifungo vya gerezani au faini ya fedha isiyopungua Sh. milioni tano kulingana na kosa lililofanyika.
Kutokana na ukweli kuwa sheria yenyewe ilishapitishwa na wabunge, ni vizuri sasa Watanzania wakazingatia utekelezaji wake ili kujiepusha na adhabu zake.
Mathalani, matumizi ya mitandao yamekuwa ya kiwango cha juu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu. Mitandao hiyo imekuwa ikitumika kwa njia mbalimbali ikiwamo kampeni miongoni mwa wagombea, lakini pia kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia kuwashambulia wenzao.
Kadhalika, mitandao hiyo imekuwa ikitumika vibaya na kuwazushia mambo, kuwatukana na kuwadhalilisha watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa kitaifa.
Pamoja na ukali wa sheria yenyewe, ni vizuri wananchi wakaisoma na kuielewa vizuri ili kujiepusha na matatizo yanayoweza kuwakuta huko mbele ya safari.
Tunaelewa kuwa sheria hiyo ni kali na inadhibiti baadhi ya maeneo na hasa yale ya utoaji wa maoni, lakini pia inabidi tukubali kuwa Taifa letu katika kipindi hiki linahitaji miongozo ya kudumisha amani na utulivu.
Tunasisitiza kuwa ni bora wananchi wakaisoma vizuri sheria hiyo na kuielewa kwa kuwa atakayefanya makosa atamshughulikia bila kusamehewa kwa kuwa kutojua sheria siyo utetezi.
Tunaamini kuwa kwa kuwa serikali ilishasema kama yataonekana mapungufu wakati wa utekelezaji wake itakuwa tayari kuipitia, ni vizuri itekeleze ahadi hiyo kwa kuwa upitishaji wake uliacha maswali mengi kuliko majibu kutoka kwa wananchi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: