
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile.
Sakata la madeni ya walimu limezidi kuchukua sura
mpya baada ya serikali kusema haidaiwi na kwamba imebaini kuwapo kwa
majina hewa ya walimu zaidi 4,000 yaliyowasilishwa kwa ajili ya malipo.
Imesema imegundua hivyo baada ya kufanya uhakiki wa deni la Sh.
bilioni 19.6 lililowasilishwa na walimu baada ya kuwalipa madai yao kwa
mara ya mwisho mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius
Likwelile, baada ya kuhakiki madeni hayo mwaka jana, serikali imegundua
deni halisi inalodaiwa na walimu ni Sh bilioni 5.6 tu. Alisema endapo serikali isingefanya uhakiki wa deni hilo na kulilipa ingeingia hasara ya Sh. bilioni 14.
Alisema katika uhakiki huo, wizara hiyo imebaini kulikuwa na deni
hewa kubwa la mwalimu mmoja wa Halmashauri ya Tunduru Mkoani Lindi Sh.
milioni 500 na kwamba baada ya kuhakiki imegundua deni lake halali ni
Sh. 500,000 tu.
Dk. Likwelile alisema kwa madeni ya mwaka jana, serikali imelipa walimu Sh. bilioni 5.6 baada ya kufanya uhakiki. “Katika uhakiki tumebaini kuwapo udanganyifu wa fedha kwa walimu
kujiongezea huku wengine wakidai deni la aina moja mara nne,” alisema.
SABABU ZA KUKATAA MADENI
Dk. Likwelile alitaja sababu za serikali kukataa kulipa baadhi ya
madai ya walimu yaliyowasilishwa ni pamoja na kukosa vibali au
vielelezo, madai mengine kuwa yameshalipwa, mishahara iliyowasilishwa
kama madai yasiyo ya mishahara, baadhi ya walimu kutotambuliwa na
halmashauri, baadhi ya walimu kutokuwa na madai katika majalada na
makosa ya ukokotoaji na uandishi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment