
Mgombea urais wa Zanzibar wa Chama cha Wananchi
(CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amepinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi
visiwani humo (Zec) kufuta matokeo ya uchaguzi na kwamba kuna njama za
makusudi za kutaka kuvuruga demokrasia na kuingiza nchi katika machafuko
kwa maslahi ya watu binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Maalim Seif
alisema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim
Jecha, hakutafakari kufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, kwani una athiri
pia Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu wapiga kura
ni walewale waliomo katika Daftari la Wapigakura la Zec na kufanya kazi
ya uwakala wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Alisema hali hiyo inaitia Jamhuri ya Muungano katika taharuki bila ya sababu yoyote ya msingi.
Alisema Rais wa Jamuhuri ya Muungano hawezi kupatikana kwa kupigiwa
kura na wananchi wa Tanzania Bara pekee, hivyo Cuf inaona uwamuzi huo
umekuja baada ya majaribio yote ya kutaka kulazimisha ushindi usiokuwapo
wa CCM kushindikana.
“Tumetambua zilikuwapo njama za kutaka kumtangaza mgombea urais wa
CCM, Dk. Ali Mohammed Shein, kwa nguvu lakini njama hizo zimeshindikana
kutokana na ukweli uliokuwa ukiibuka kupitia uhakiki wa matokeo ya
uchaguzi,” alisema Seif.
Maalim Seif alidai CUF ndiyo mshindi wa uchaguzi wa urais wa
Zanzibar pamoja na majimbo yote 18 ya Pemba na majimbo tisa ya Unguja na
kuzitaka jumuiya za kimataifa kutoiruhusu CCM kukandamiza haki za
kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar kwa mara nyingine na kuwataka
wananchi kubakia watulivu na kuitunza amani iliyopo.
“Tunatamka wazi CUF hatutambui uamuzi huo binafsi wa mwenyekiti wa
tume na tunaitaka serikali na CCM kuiachia tume iendelee na kazi yake ya
uhakiki wa matokeo ya uchaguzi na kisha kutangaza mshindi,” alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania (Tamwa) Zanzibar, Mzuri Issa Ali, alisema uwamuzi wa Zec umetia
doa kubwa katika historia ya Zanzibar na kuwataka viongozi wa vyama vya
siasa pamoja na tume ya uchaguzi kukaa pamoja kutafuta muafaka kuepusha
gharama za uchaguzi mpya kufanyika visiwani hapa.
“Tume ya Uchaguzi na wanasiasa wanatakiwa kukaa pamoja na
kukubaliana kwa sababu sasa hivi huduma za kijamii Zanzibar zimesimama
na suala la kurejea uchaguzi ni gharama kubwa,” alisema Mzuri.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadhi Ali Said,
alisema uamuzi wa Mwenyekiti wa Zec umeingiza Zanzibar katika mgogoro wa
kikatiba na Rais pamoja na mawaziri wake wakiendelea kubaki huku muda
wao ukiwa umemalizika wa miaka mitano.
“Uamuzi wa tume umeingiza nchi katika mgogoro wa kikatiba kuhusu
uhalali wa Rais kukaa madarakani wakati miaka mitano imepita na
anatakiwa kuchaguliwa Rais mpya kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar,”
alisema Awadhi.
Alisema kwamba kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar baraza la
wawakilishi linapovunjwa ndani ya siku 90 wajumbe wake wanatakiwa
kuchaguliwa ili uwepo uwakilishi wa wananchi na baraza hilo lilivunjwa
Agosti 13, mwaka huu.
Baadhi ya waangalizi wa uchaguzi huo wametofautiana na madai ya
kasoro za uchaguzi zilizodaiwa kufanyika akiwamo muangalizi kutoka
Jukwaa la Vijana Zanzibar (Zyf), Ali Khamis, ambaye alisema haikuwa
muafaka matokeo ya uchaguzi huo kufutwa wakati kazi ya kupiga na
kuhesabu kura ikiwa imefanyika na kukamilika katika majimbo.
Thabir Shaabani muangalizi wa uchaguzi alisema maeneo mengi ya
Unguja uchaguzi ulikwenda vizuri na sababu za kuahirisha uchaguzi
zilizotolewa hazikuwa na hoja ya msingi na badala yake majimbo yenye
matatizo kasoro zilihitaji kurekebishwa ili kuepusha hasara ya kurejea
uchaguzi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment