Wakazi wa Lindi wakigombea nakala za Katiba inayopendekezwa
zilizokuwa zikigawiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma, Hashim Rungwe.
Baada ya Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (Nec) kuahirisha Kura ya Maoni kwa ajili ya Katiba
Inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu, wadau
mbalimbali walitoa maoni wakitaka fursa hiyo itumike kwa ajili ya
kuzigawa nakala za katiba hiyo na kuzisambaza maeneo mbalimbali nchini.
Wanaharakati, wanasiasa, wasomi na wananchi wa
kawaida wametaka nakala za Katiba hiyo zisambazwe kwa wingi mikoani ili
kutoa fursa kwa wananchi kuzisoma na kuelewa kilichomo, kisha kufanya
uamuzi sahihi wakati wa kupiga Kura ya Maoni.
Mikoa ya Lindi na Mtwara ni baadhi ya maeneo
nchini ambayo nakala za Katiba Inayopendekezwa zimeonekana kuadimika.
Wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa wakihaha kuzitafuta nakala hizo bila
mafanikio na inapotokea fursa ya kuonekana, wanazigombea kwa fujo.
Mwandishi wa makala haya aliyetembelea baadhi ya
maeneo ya mikoa hiyo, ameshuhudia namna wananchi hao wanavyohangaika
kupata nakala za Katiba hiyo Inayopendekezwa ili wajisomee kama sehemu
ya maandalizi ya Kura ya Maoni.
Katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama
cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na kufanyika kwenye Uwanja wa Mkanaledi,
wananchi hao kwa nyakati tofauti, wanaeleza kuwa tangu Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilipoenda kukusanya maoni yao kwa ajili ya
kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, hawajui kinachoendelea kuhusu
Mchakato wa Katiba Mpya.
Hali hiyo imewafanya wawe na shauku kubwa ya kujua
kinachoendelea kwenye mchakato huo kiasi cha kufanya wagombee nakala
chache za Katiba Inayopendekezwa zilizokuwa zikigawiwa na mwenyekiti wa
chama hicho Hashim Rungwe.
Wakazi hao walikuwa wakigombea nakala hizo kwa
fujo na kusababisha uharibifu wa mali vikiwamo viti na meza zilizokuwa
zikitumika katika mkutano huo.
Nini kifanyike?
Mkazi wa Magomeni, Asha Saidi anasema wakazi hao
wanagombea nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa hazionekani kokote,
hivyo kugawiwa siku hiyo ilikuwa ni neema.
Anasema baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
kukusanya maoni yao na kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, walikuwa
wanakutana na wanasiasa ambao hufika na kuwataka wakaipigie Katiba hiyo
kura ya hapana wakati hawajaiona na kuisoma.
“Tunagombea nakala za Katiba kwa kuwa sisi bado
hatujaziona, lakini wanasiasa wanatuambia tukaipigie Katiba
Inayopendekezwa kura ya hapana,” anasema Saidi.
Anabainisha kuwa kukosekana kwa nakala za katiba
hiyo kumewafanya wananchi wengi wakose kujiamini juu ya uamuzi
watakaofanya siku ya kuipigia kura, hasa baada ya wanasiasa kuwashawishi
wakapige kura wanayoona wao inafaa.
Kauli ya wanasiasa
Mchakato upelekwe mbele
“Fikiria mimi sijaiona katiba yenyewe lakini mtu (mwanasiasa)
ananiambia nikaipigie kura ya hapana, hapa napigia kura kitu gani? Ndiyo
maana ninagombea ili angalau niwe na nakala yangu,” anasema.
Kauli ya wanasiasa
Mwenyekiti wa CHAUMMA mkoa wa Mtwara, Fatma
Seleman anasema kuwa wananchi hawawezi kupata mabadiliko kama Katiba
itakuwa haiweki mfumo sahihi wa usimamizi wa sheria na kanuni.
Anasema kitendo cha serikali kutosambaza Katiba
kinawanyima wananchi uhuru wa kuwa na maamuzi sahihi wakati wa upigaji
wa kura ya kuipitisha katiba hiyo.
Kwa mujibu wa Suleiman, kura ina thamani kubwa,
hivyo ni vyema Serikali ikafanya jitihada za dhati kuhakikisha nakala za
katiba hiyo zinawafikia wananchi ili waweze kuzisoma na kufanya uamuzi
sahihi.
“Kiongozi anatakiwa kutatua kero badala ya kuwa na
maneno mengi, wananchi sisi kilio chetu kilikuwa ni kupata Katiba Mpya,
lakini sasa kadiri siku zinavyokwenda hali inakuwa tofauti. Unakuta
wanasiasa wanakuja kutushawishi kuipiga kura ya ndiyo au hapana Rasimu
ya Katiba tusiyoijua,” anasema.
Mchakato upelekwe mbele
Wakazi wa Wilaya ya Masasi wanaiomba Serikali
kusogeza mbele mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ili wazisake
nakala hizo na kuzisoma.
Abdul Juma anasema kuwa kitendo cha Serikali
kutosambaza nakala hizo kwa wingi kinawaweka wananchi katika wakati
mgumu, kwani wakati wa kuipigia kura watashindwa kuwa na maamuzi sahihi.
“Wananchi tulio wengi bado hatujabahatika kuipitia
Katiba Inayopendekezwa, kwa hiyo hatujui kilichoandikwa ndani yake.
Kama Serikali ingezileta mapema nakala za katiba nina imani haya yote
yasingejitokeza kama hivi watu kukanyagana na kusababisha viti kuvunjika
katika kurupushani,” anasema Juma.
Kassim Abdurahman anasema kuwa kutokana na uwepo
wa rasilimali zilizogundulika katika mikoa ya Lindi na Mtwara, Tanzania
inahitaji Katiba imara ya kulinda rasilimali hizo. “Hii pengine ndiyo
sababu wakazi wengi wa mikoa hiyo wanazigombea nakala za katiba ili
kujua kilichomo kuhusu gesi asilia,” anasema.
“Katiba ya sasa haiendani na uhalisia wa maisha ya
sasa. Ukiangalia Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zimegundulika
baada ya katiba ile kutungwa. Sasa hivi tuna gesi na mafuta hatujui sisi
wananchi tutanufaika vipi navyo, tungetaka kuona Katiba inazungumzia
mambo hayo,” anasema Abdurahman.
Anaongeza, “Katiba zilizokuja kwenye maeneo yetu zilikuwa chache
na kugaiwa kwa viongozi tu jambo ambalo siyo zuri. Serikali inatakiwa
kusambaza hiyo katiba kwa wingi ili wananchi wengi tuisome tuone kama
ina maslahi na sisi na kama ikiwa tofauti basi mchakato uanze mapema
hatuna ulazima wa kuipata Katiba Mpya sasa.”
Anapozungumzia suala hilo , mwenyekiti wa Chama
cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Hashim Rungwe, anasema kuwa serikali bado
inatakiwa kuzisambaza nakala kwa wananchi ili kufahamu kilichomo ndani
yake na bila kufanya hivyo, itakuwa haiwatendei haki.
“Wananchi wengi bado wana shauku ya kuisoma katiba
na kujua kilichoandikwa. Sasa ni wajibu wa Serikali kuisambaza kwa
wingi ili iwafikie watu waisome na kufanya uamuzi sahihi,” anasema.
Hata hivyo Rungwe anaeleza hatua yake ya kufanya
ziara katika miko ya kusini, imelenga kuhamasisha wananchi waisome
Katiba Inayopendekezwa na kushiriki katika shughuli kubwa iliyoko mbele
yao ya kuipigia kura katiba hiyo.
“Lakini kikubwa wanapaswa kupata nakala na
kuzisoma vizuri ili wajue kuna nini ndani yake kabla ya kufanya uamuzi
wa kuikubali au kuikataa katiba hiyo,” anasema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment