Social Icons

Pages

Wednesday, June 03, 2015

NAKALA ZA KATIBA ZINAVYOGEUKA LULU MIKOA YA LINDI, MTWARA

Wakazi wa Lindi wakigombea nakala za Katiba inayopendekezwa zilizokuwa zikigawiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma, Hashim Rungwe.
Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuahirisha Kura ya Maoni kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu, wadau mbalimbali walitoa maoni wakitaka fursa hiyo itumike kwa ajili ya kuzigawa nakala za katiba hiyo na kuzisambaza maeneo mbalimbali nchini.
Wanaharakati, wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida wametaka nakala za Katiba hiyo zisambazwe kwa wingi mikoani ili kutoa fursa kwa wananchi kuzisoma na kuelewa kilichomo, kisha kufanya uamuzi sahihi wakati wa kupiga Kura ya Maoni.
Mikoa ya Lindi na Mtwara ni baadhi ya maeneo nchini ambayo nakala za Katiba Inayopendekezwa zimeonekana kuadimika. Wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa wakihaha kuzitafuta nakala hizo bila mafanikio na inapotokea fursa ya kuonekana, wanazigombea kwa fujo.
Mwandishi wa makala haya aliyetembelea baadhi ya maeneo ya mikoa hiyo, ameshuhudia namna wananchi hao wanavyohangaika kupata nakala za Katiba hiyo Inayopendekezwa ili wajisomee kama sehemu ya maandalizi ya Kura ya Maoni.
Katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na kufanyika kwenye Uwanja wa Mkanaledi, wananchi hao kwa nyakati tofauti, wanaeleza kuwa tangu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipoenda kukusanya maoni yao kwa ajili ya kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, hawajui kinachoendelea kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya.
Hali hiyo imewafanya wawe na shauku kubwa ya kujua kinachoendelea kwenye mchakato huo kiasi cha kufanya wagombee nakala chache za Katiba Inayopendekezwa zilizokuwa zikigawiwa na mwenyekiti wa chama hicho Hashim Rungwe.
Wakazi hao walikuwa wakigombea nakala hizo kwa fujo na kusababisha uharibifu wa mali vikiwamo viti na meza zilizokuwa zikitumika katika mkutano huo.

Nini kifanyike?
Mkazi wa Magomeni, Asha Saidi anasema wakazi hao wanagombea nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa hazionekani kokote, hivyo kugawiwa siku hiyo ilikuwa ni neema.
Anasema baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukusanya maoni yao na kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, walikuwa wanakutana na wanasiasa ambao hufika na kuwataka wakaipigie Katiba hiyo kura ya hapana wakati hawajaiona na kuisoma.
“Tunagombea nakala za Katiba kwa kuwa sisi bado hatujaziona, lakini wanasiasa wanatuambia tukaipigie Katiba Inayopendekezwa kura ya hapana,” anasema Saidi.
Anabainisha kuwa kukosekana kwa nakala za katiba hiyo kumewafanya wananchi wengi wakose kujiamini juu ya uamuzi watakaofanya siku ya kuipigia kura, hasa baada ya wanasiasa kuwashawishi wakapige kura wanayoona wao inafaa.
“Fikiria mimi sijaiona katiba yenyewe lakini mtu (mwanasiasa) ananiambia nikaipigie kura ya hapana, hapa napigia kura kitu gani? Ndiyo maana ninagombea ili angalau niwe na nakala yangu,” anasema.

Kauli ya wanasiasa
Mwenyekiti wa CHAUMMA mkoa wa Mtwara, Fatma Seleman anasema kuwa wananchi hawawezi kupata mabadiliko kama Katiba itakuwa haiweki mfumo sahihi wa usimamizi wa sheria na kanuni.
Anasema kitendo cha serikali kutosambaza Katiba kinawanyima wananchi uhuru wa kuwa na maamuzi sahihi wakati wa upigaji wa kura ya kuipitisha katiba hiyo.
Kwa mujibu wa Suleiman, kura ina thamani kubwa, hivyo ni vyema Serikali ikafanya jitihada za dhati kuhakikisha nakala za katiba hiyo zinawafikia wananchi ili waweze kuzisoma na kufanya uamuzi sahihi.
“Kiongozi anatakiwa kutatua kero badala ya kuwa na maneno mengi, wananchi sisi kilio chetu kilikuwa ni kupata Katiba Mpya, lakini sasa kadiri siku zinavyokwenda hali inakuwa tofauti. Unakuta wanasiasa wanakuja kutushawishi kuipiga kura ya ndiyo au hapana Rasimu ya Katiba tusiyoijua,” anasema.

Mchakato upelekwe mbele
Wakazi wa Wilaya ya Masasi wanaiomba Serikali kusogeza mbele mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ili wazisake nakala hizo na kuzisoma.
Abdul Juma anasema kuwa kitendo cha Serikali kutosambaza nakala hizo kwa wingi kinawaweka wananchi katika wakati mgumu, kwani wakati wa kuipigia kura watashindwa kuwa na maamuzi sahihi.
“Wananchi tulio wengi bado hatujabahatika kuipitia Katiba Inayopendekezwa, kwa hiyo hatujui kilichoandikwa ndani yake. Kama Serikali ingezileta mapema nakala za katiba nina imani haya yote yasingejitokeza kama hivi watu kukanyagana na kusababisha viti kuvunjika katika kurupushani,” anasema Juma.
Kassim Abdurahman anasema kuwa kutokana na uwepo wa rasilimali zilizogundulika katika mikoa ya Lindi na Mtwara, Tanzania inahitaji Katiba imara ya kulinda rasilimali hizo. “Hii pengine ndiyo sababu wakazi wengi wa mikoa hiyo wanazigombea nakala za katiba ili kujua kilichomo kuhusu gesi asilia,” anasema.
“Katiba ya sasa haiendani na uhalisia wa maisha ya sasa. Ukiangalia Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zimegundulika baada ya katiba ile kutungwa. Sasa hivi tuna gesi na mafuta hatujui sisi wananchi tutanufaika vipi navyo, tungetaka kuona Katiba inazungumzia mambo hayo,” anasema Abdurahman.
Anaongeza, “Katiba zilizokuja kwenye maeneo yetu zilikuwa chache na kugaiwa kwa viongozi tu jambo ambalo siyo zuri. Serikali inatakiwa kusambaza hiyo katiba kwa wingi ili wananchi wengi tuisome tuone kama ina maslahi na sisi na kama ikiwa tofauti basi mchakato uanze mapema hatuna ulazima wa kuipata Katiba Mpya sasa.”
Anapozungumzia suala hilo , mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Hashim Rungwe, anasema kuwa serikali bado inatakiwa kuzisambaza nakala kwa wananchi ili kufahamu kilichomo ndani yake na bila kufanya hivyo, itakuwa haiwatendei haki.
“Wananchi wengi bado wana shauku ya kuisoma katiba na kujua kilichoandikwa. Sasa ni wajibu wa Serikali kuisambaza kwa wingi ili iwafikie watu waisome na kufanya uamuzi sahihi,” anasema.
Hata hivyo Rungwe anaeleza hatua yake ya kufanya ziara katika miko ya kusini, imelenga kuhamasisha wananchi waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki katika shughuli kubwa iliyoko mbele yao ya kuipigia kura katiba hiyo.
“Lakini kikubwa wanapaswa kupata nakala na kuzisoma vizuri ili wajue kuna nini ndani yake kabla ya kufanya uamuzi wa kuikubali au kuikataa katiba hiyo,” anasema.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: