Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla.
Taasisi za serikali zinadaiwa Sh. bilioni 20 na mamlaka za maji nchini.Hayo yalisemwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla,
alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema),
Leticia Nyerere.
Mbunge huyo alisema ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara
inadaiwa Sh. milioni 102 na Jeshi la Wananchi wa Tanzania linadaiwa Sh.
milioni nane na kuhoji kwa nini serikali haiingilii kati ili kuhakikisha
kwamba madeni hayo yanalipwa ili kuiwezesha Mamlaka ya Maji ya Musoma
(Muwasa) kufanyakazi yao kikamilifu na kwa mafanikio.
Akijibu, Makalla alikiri serikali kutambua kuwapo kwa madeni hayo. Alisema Jeshi la Wananchi linadaiwa Sh. milioni 2.4, hospitali
zinadaiwa Sh. milioni 113 na madeni mengine hivyo mamlaka hiyo inaidai
serikali jumla ya Sh. milioni 390 na kwamba mamlaka zote za maji nchini
zinaidai taasisi za serikali Sh. bilioni 20.
"Sisi (Wizara ya Maji) tutashirikiana na Wizara ya Fedha kuona
kwamba madeni haya yanalipwa ili mamlaka hizi ziweze kufanyakazi kwa
ufanisi," alisema.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent
Nyerere, alitaka kujua kama serikali ipo tayari kutoa ruzuku kwa mamlaka
za maji ikiwamo Muwasa ili ziweze kujiendesha na kupunguza mzigo kwa
wananchi. Pia alihoji kama ni sawa wizara na idara za serikali kama JWTZ, Polisi, Ikulu kukatiwa maji kwa kushindwa kulipia huduma hiyo.
Akijibu, Makalla alisema serikali ilianzisha mamlaka za majisafi na
usafi wa mazingira nchini ambazo ziko katika madaraja matatu, 'A', 'B'
na 'C'. Alifafanua kuwa mamlaka za daraja 'B' ni zile ambazo zinapata ruzuku ya kulipia sehemu ya gharama za umeme wa kuendesha mitambo.
Alisema mamlaka 'C' ni zile ambazo zinapata ruzuku ya mishahara ya
wafanyakazi wake pamoja na kulipia sehemu ya gharama za umeme wa
kuendesha mitambo na gharama za umeme za uwekezaji.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment