Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania , Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Hivi karibuni, mwandishi mmoja aliandika akihoji hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuwateua Waislamu kushika wizara nyeti zote.
Huyu aliandika akitetea hoja yake kwa takwimu,
hata waliomfuatia nao walimjibu kwa takwimu. Hivyo hawa wote hawawezi
kuwa wapumbavu kwa wanayoyaamini.
Ni vigumu kusema ni upumbavu au siyo upumbavu kila
mtu kushikilia hoja yake. Inategemea mtu analiangalia hili kutoka kona
ipi na kwa lengo lipi.
Kwa maoni yangu mimi, tatizo lenyewe ni kubwa
zaidi ya ndugu hawa wote wanavyoliona. Nina imani kwamba hawa watatu
waliojitokeza kuliongelea suala la udini katika Serikali wana wafuasi
wao.
Wote wanatoa ushahidi kwamba jambo hili
linaongelewa mitaani. Ni kweli linaongelewa, lakini ukweli ni kwamba
jambo ni zaidi ya Ukristo na Uislamu.
Hata kama Rais Kikwete, angejitahidi kulinganisha
uteuzi wa Wakristo na Waislamu, bado Wahaya wangekuja juu kwamba
Wanyakyusa ni wengi zaidi katika Serikali yake.
Angejaribu kutoa haki sawa kwa makabila yote, bado
watu warefu wangelalamika kwamba watu wafupi wamependelewa zaidi! Kama
angefanikiwa kutoa haki sawa kwa warefu na wafupi, basi suala la sura
lingejitokeza.
Wenye sura “nzuri” wangelalamika kwamba,
amewapendelea watu wenye sura “mbaya” Kama tunakumbuka wakati wa kampeni
kuna baadhi ya watu walikuwa wanasema kwamba mgombea Jakaya Kikwete,
alikuwa na sura ya kuvutia kuliko wagombea wengine.
Walimpenda siyo kwa sababu nyingine, ni kwa vile sura yake ni nzuri! Hivyo na sura inaweza kuwa hoja!
Tuliangalie kwa upana zaidi
Hoja yangu ni kwamba hili la kuwapendelea Waislamu
au Serikali za awamu nyingine kuwapendelea Wakristo, linakwenda mbali
zaidi ya Ukristo. Ni lazima kuliangalia kwa upana zaidi.
Malalamiko haya yanayojitokeza na ambayo
yataendelea kujitokeza kila mara ni ushahidi wa kutosha kwamba bado
hatujafanikiwa kuwa na mfumo wa kutusaidia kulenga pamoja kama Taifa.
Hatujapata falsafa na siasa nzuri ya kutuwezesha kujenga mambo
ya msingi katika Taifa letu. Mambo ambayo yako juu ya dini zote, juu ya
makabila yote na juu ya kila Mtanzania.
Wasiwasi unaojitokeza ni kwamba akiteuliwa
Muislamu katika wizara au nafasi nyingine, atawapendelea Waislamu
wenzake. Hivyo hivyo akiteuliwa Mkristo.
Hata hivyo, tungekuwa na mfumo wa kuwateua watu
kufuatana na sifa zao, wasiwasi huu usingekuwapo. Maana hata kama
akiingia Muislamu, Mkristo au mpagani, anaongozwa na mfumo wa kitaifa.
Kama ni kusambaza maji katika Wilaya ya Misungwi,
Waziri anayetoka Biharamulo, hatasambaza maji Wilaya ya Chato. Kila mtu
anaamini kwamba waziri akitoka kwenye wilaya yoyote, basi huko maji
yatapatikana.
Elimu, imekuwa ya kushindania na hasa nafasi ya
kusoma nje ya nchi, wengine wanafikiri udini unaweza kusaidia
upatikanaji wa nafasi, kwa maana kwamba waziri akiwa Mkristo, watoto wa
Wakristo watapata upendeleo au waziri akiwa Muislamu, watoto wa Waislamu
watapata upendeleo.
Badala ya kulalamika kwamba Rais Kikwete
anawapendelea Waislamu, ni bora kuanza mjadala wa kuhoji mfumo wa
kulisaidia Taifa letu kuainisha mambo muhimu na kuyapa kipaumbele.
Mfano kama taifa tungekuwa na mpango wa kujenga
sekondari tano kwenye kila wilaya ndani ya miaka mitano, Waziri wa
Elimu, anaweza kuwa wa dini yoyote au wa chama chochote, maana kwa vile
mpango upo na unasimamiwa na sheria za nchi, hawezi kufanya upendeleo
kuzigeuza sekondari hizo za Kikristo au kuzijenga zote wilayani kwake.
Hata kama mawaziri wote wangekuwa Waislamu, lakini
watu hawa wanafanya kazi kwa manufaa ya Taifa zima, tatizo liko wapi?
Tunaangalia utendaji wa mtu au dini yake?
Tatizo ni kwamba bado hatujayaweka wazi masilahi
ya Taifa letu. Masilahi ambayo kila Mtanzania anakubaliana nayo na yuko
tayari kuyafia.
Masilahi ambayo hayana dini, kabila, wilaya au
mkoa. Masilahi ya Kitanzania. Siyo lazima mtu awe Mkristo au Muislamu
kutunza mazingira yetu. Dini siyo lazima katika kutunza na kulinda
rasilimali za taifa letu.
Leo hii Wakristo wanalalamika kwamba Waislamu
wanapendelewa. Kesho, watu wakifumbuka macho wataanza kulalamika kwamba
ni kwa nini wana CCM peke yao ndo wanateuliwa katika ngazi mbalimbali
ndani ya Serikali.
Jinsi tunavyofumbwa macho na suala la udini kiasi
kwamba hata mtu mwenye sifa kama si wa dini yako basi hafai kwa lolote,
ndivyo tunavyofunikwa na hili la vyama vya siasa.
Hadi leo hii bado kuna Watanzania wanaochanganya Utanzania na
U-CCM. Kwa maana kwamba kama wewe siyo mwana CCM, basi wewe siyo
Mtanzania au si mzalendo na kama ni Mtanzania basi ni Mtanzania nusu. Bila kuwa mwanachama wa CCM, mtu anaonekana kama msaliti. Tanzania ina watu zaidi ya milioni 35, Wana CCM, hawafiki milioni 10.
Ndiyo kusema wapo Watanzania wengi ambao siyo wana CCM. Hii haina maana kwamba hawa si Watanzania na kwamba si wazalendo. Leo hii kama Rais Jakaya Kikwete, agefanya uteuzi
wa mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya ambaye siyo mwana CCM, basi huu
ungeonekana ni usaliti wa chama.
Kwa maoni yangu, malalamiko ya Ukristo na Uislamu
yanafichua dhambi kubwa ambayo ni kama kansa katika Taifa letu. Kansa
hii ni makundi yasiyoleta maendeleo. Makundi ya kidini, kikabila,
ukanda, kijinsia na wakati mwingine makundi yanayowagawa watu kufuatana
na sura zao au mila zao.
Tatizo ni kubwa na linahitaji mjadala wa kina.
Mambo kama haya yasipojadiliwa kupitia kwenye vyombo vya habari,
yatajadiliwa wapi? Kuwa mwaminifu na mpenzi wa kiongozi siyo kumsaidia
kufunika yale yanayochemka, bali ni kumsaidia kuyapoza kwa njia ya
kuyaweka wazi na kuwashirikisha watu wengine wenye nia njema.
Sina nia ya kumtetea Rais Kikwete, ila ni kumkosea
haki kumhukumu kwa mambo ambayo yapo na kwa namna moja ama nyingine
yako juu ya uwezo wake. Asipomteua Mkristo, atamteua Muislamu. Pia, kama
ikitokea Waislamu watano ni bora na wana sifa, ni wachapakazi na
wazalendo, hawezi kuwatupa nje kwa kuogopa Wakristo.
Tuache kulalamika, tushirikiane naye kuijenga
Tanzania, iliyoshikamana. Tutofautiane kwa mengine, lakini kwa masilahi
ya Taifa letu tushikamane!
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment