
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid.
Serikali imesema hadi Aprili mwaka huu, Sh.
228,720,505,813.00 zilitumika kuhakikisha upatikanaji dawa, vifaa, vifaa
tiba na vitendanishi katika vituo vya afya vya umma.
Aidha, mwaka huu wa fedha Sh. 336,002,706,847.00 zimetengwa kwa
ajili ya kununua, kutunza na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi
katika vituo vya huduma za afya vya umma. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid,
alisema jana bungeni, wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2015/16.
Alisema katika mwaka wa fedha 2014/15 serikali imeendelea kudhibiti
upotevu wa dawa ambapo bohari ya dawa imeweza kuweka nembo ya GOT
(Government of Tanzania) kwenye aina 65 za dawa ambayo ni sawa na
asilimia 50 ya utekelezaji wa lengo lililopangwa.
Dk. Seif alisema katika kuboresha upatikanaji wa dawa, wizara
imeanza kushirikisha sekta binafsi kwa ajili ya ununuzi wa dawa pale
ambapo bidhaa hizo zitakosekana Bohari ya Dawa. Aliongeza kuwa wizara inaendelea na uratibu wa kufanya mabadiliko
ya Sheria iliyoanzisha Bohari ya Dawa ili kuiwezesha kufanyakazi kwa
ufanisi zaidi kwa mwaka huu wa fedha , wizara hiyo itawasilisha Muswada
wa Sheria ya Wakala wa Maabara ya Mkemia wa Serikali na Muswada wa
Sheria ya Watalaam wa Kemia ili usomwe bungeni kwa mara ya pili.
Kadhalika, alisema wizara kupitia mabaraza ya taalumaa ilisimamia
maadili na kusajili wataalamu waliokidhi viwango vya kutoa huduma za
afya nchini. “Hadi kufikia Machi 2015, jumla ya wataalam 9,123 walisajiliwa kupitia mabaraza yao ya kitaaluma,” alisema.
Alisema wizara kupitia Baraza la Madaktari lilipitisha hospitali za
rufaa za mkoa za St. Gaspar (Itigi), Tumbi (Pwani) na Songea (Ruvuma)
kutoa mafunzo kwa vitendo kwa madaktari wapya na hivyo kufanya hospitali
zinazotoa mafunzo kwa vitendo kufikia 20.
Alisema mwaka 2014/15 wataalamu bingwa kutoka Marekani na India
waliletwa na kutoa huduma za mishipa ya damu iliyoziba ambapo wagonjwa
19 walihudumiwa. Pia, watalaamu 33 kutoka Saud Arabia chini ya ufadhili wa DHI
Nurevn Islamic Foundation wakishirikiana na madaktari bingwa wa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili walifanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa
66, kati yao wagonjwa 23 walifanyiwa upasuaji mkubwa na catheterization
kwa wagonjwa 43.
Aidha, mashine tano za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo zimenunuliwa na kufanya idadi ya mashine zilizopo kuwa 16. Alisema serikali iliendelea kutoa huduma za msingi zikiwemo
chakula, malazi, mavazi, matibabu na unasihi kwa wazee na watu wenye
ulemavu wasiojiweza 869 wanaotunzwa na kulelewa katika makazi 17 ya
serikali.
Alisema wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilipokea
sampuli 10,974 zikiwemo za vyakula, dawa, kemikali, maji na maji taka,
bidhaa za viwandani na mazingira. Kati ya hizo sampuli 2,658
zilichunguzwa na kutolewa matokeo. Alisema sampuli nyingine 7,714 zilikuwa na makosa ya jinai, kati ya hizo 6,318 zilichunguzwa na kutolea matokeo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment