Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid akiwasilisha bungeni
makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2015 / 2016,
Dodoma jana.
Wabunge wa Kamati ya
Bunge ya Huduma za Jamii na wa Kambi ya Upinzani Bungeni, wameitaka
Serikali kulipa deni la Sh125 bilioni ambalo Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
inadaiwa na pia kuilipa Hospitali ya Apollo ya nchini India.
Wamesema kitendo cha Serikali kushindwa kuongeza
bajeti katika sekta ya afya hadi kufikia asilimia 15 ya bajeti yake
yote, ni kukiuka Azimio la Abuja linalozitaka nchi wanachama kutekeleza
suala hilo ifikapo mwaka 2015.
Kamati hiyo pia ilieleza matatizo mbalimbali
yanayoikabili sekta hiyo ikiwa ni pamoja na upungufu wa watumishi,
gharama kubwa za matibabu ya saratani, kutotekelezwa kwa mpango wa bima
kwa wote na huduma kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Akiwasilisha taarifa ya kamati jana kuhusu
utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii mwaka
2015/16, mjumbe wa kamati hiyo, Martha Umbulla alisema deni la Hospitali
ya Apollo linalotokana na gharama za matibabu ya Watanzania limefikia
Dola 9milioni za Marekani (Sh17bilioni), huku deni la MSD likifikia
Sh108 bilioni.
Umbulla alisema mbali na madeni hayo, wizara hiyo inakabiliwa na changamoto 17 zinazotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
“Serikali ilipe deni la MSD na kutoa fedha za
ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa mkupuo. Pia, taarifa za
mapokezi ya dawa kutoka MSD katika hospitali au vituo vya afya nchini
ziwekwe wazi na MSD itoe takwimu za usambazaji wake wa dawa ili
kujitathmini katika utendaji wake,” alisema.
“Serikali inatakiwa kulipa deni la Apollo ili
kutokiuka mkataba wa makubaliano baina ya Serikali na hospitali hiyo kwa
kuwahudumia wagonjwa wa Tanzania,” alieleza.
Alisema kwa sasa idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje
ya nchi kwa ajili ya matibabu imeongezeka ikilinganishwa na bajeti
inayotengwa.
Alisema bado sehemu kubwa ya shughuli za maendeleo
za wizara hiyo zinategemea fedha za wahisani, kwamba mwaka 2014/15
zilitengwa Sh305 bilioni za maendeleo, Sh251.7 bilioni kati ya fedha
hizo zilitoka kwa wadau wa maendeleo, jambo linaloathiri ununuzi wa
dawa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo.
Akiwasilisha taarifa ya Kambi ya Upinzani kwa
wizara hiyo, msemaji wake Dk Antony Mbassa alisema: “Fedha za maendeleo
zilizotolewa katika wizara hiyo ni asilimia 26 ya mahitaji. “Mpaka Machi mwaka huu ilipatiwa Sh8.8 bilioni za maendeleo kati ya Sh305.7 bilioni ya mahitaji halisi ya wizara.”
Kambi hiyo pia iligusia suala la uhaba wa dawa
katika hospitali nyingi nchini na kufafanua kuwa takwimu za Shirika la
Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa upatikanaji wa dawa katika vituo
vya Serikali ni asilimia 24 na vituo binafsi ni asilimia 47. “Jambo ambalo tafsiri yake ni kwamba, dawa zinazosambazwa na MSD
zinafika kwanza katika vituo binafsi kabla ya kufika katika vituo vya
Serikali. Pia, tunataka majibu ya Serikali kuhusu deni la MSD na
kuongezeka kwa gharama za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi,” alisema
Mbassa.
Akiwasilisha bajeti ya Sh813.9 bilioni ya wizara
hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alieleza
mafanikio katika sekta hiyo kwa mwaka 2015/16, akitaja vipaumbele vinane
vya bajeti hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.
Vipaumbele hivyo ni kuimarisha huduma na tiba,
kuimarisha miundombinu kwenye vyuo vya afya na ustawi wa jamii,
ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuimarisha Tehama na
kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Kuhusu wakimbizi wa Burundi, Dk Rashid alisema hadi Mei 25, mwaka huu, wakimbizi 50,829 walikuwa wameingia nchini. “Pamoja na hali hiyo, kumetokea mlipuko wa ugonjwa
wa kipindupindu na tangu Mei 25, mwaka huu, kuna wagonjwa 4,435 wa
kipindupindu na 31 walifariki dunia,” alisema.
Bajeti hiyo haikupitishwa jana kutokana na kifo cha mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa. Bunge litaendelea kesho.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment