Rais Jakaya Kikwete
Wadau wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari,
wahariri na waandishi wa habari nchini, wamepinga vikali miswada ya
Takwimu na Makosa ya Mtandaoni ambayo ina kandamiza uhuru wa habari na
kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutoisani, badala yake irudi bungeni
kujadiliwa na wadau kutoa maoni.
Ombi hilo walilitoa jana wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika hapa nchini mjini Morogoro, chini ya kauli mbiu ya ‘Usalama wa vyombo vya habari katika zama za kidigitali, uandishi makini, usawa wa kijinsia na faragha’.
Ombi hilo walilitoa jana wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika hapa nchini mjini Morogoro, chini ya kauli mbiu ya ‘Usalama wa vyombo vya habari katika zama za kidigitali, uandishi makini, usawa wa kijinsia na faragha’.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi
la Tanzania (Misa-Tan), Simon Berege, alisema pamoja na serikali
kuonyesha nia ya kuruhusu uhuru wa kujieleza na wa kupata taarifa
kupitia Katiba inayopendekezwa, serikali hiyo hiyo imeanza kufanya mambo
yenye kila dalili za kuminya uhuru wa wananchi na vyombo vya habari wa
haki ya kupata taarifa.
“Miswada hii ina vipengele vingi vinavyoleta ukiritimba katika
upatikanaji wa taarifa na kuminya uhuru wa vyombo vya habari kufanya
kazi zake,” alisema na kuongeza: “Pamoja na kwamba Rais kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu
ameshatoa msimamo wa kusaini miswada hiyo, sisi bado tunatoa rai kwa
kumsihi (Rais) kutosaini bali irudishwe bungeni na kuwasilishwa upya kwa
utaratibu wa kawaida ili wadau waweze kuijadili na kutoa maoni yao
yatakayoboresha.”
Alisema hakuna asiyetambua kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete
amekuwa mliberali, anayependa kusikiliza maoni na kuyafanyia kazi, hivyo
kusainiwa kwa sheria hizo kutatia dosari sifa nzuri aliyojiwekea kwa
wapenda demokrasia, ndani na nje ya nchi.
“Jambo moja la msingi ambalo watendaji na viongozi wetu wa
serikali na hata wa taasisi na mashirika binafsi wanapaswa kukumbuka ni
kwamba, ulimwengu kwa sasa uko kwenye zama za taarifa. Kuminya taarifa
ni kuwafanya wananchi wapitwe na zama hizi ambazo zinampa nguvu na
ushindi zaidi mtu mwenye taarifa sahihi kuliko asiye nazo, tujihadhari
kutokufanya mambo yatakayosababisha zama hizi zitupite kama
zilivyotupita zama za mapinduzi ya viwanda,” alisema.
Berege alisema harakati za serikali kutaka kufifisha uhuru wa
vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa zinafanyika huku tafiti
zikionyesha kwamba nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania zinaendelea
kuporomoka kwenye viwango vya kidunia vya kupima hali ya uhuru wa
vyombo vya habari.
Berege alitolea mfano wa waandishi kutishwa, kupigwa na kunyanyaswa
wakiwa kazini ikiwamo gazeti hili Julai, 2014 Mhariri Mtendaji, Jesse
Kwayu (NIPASHE) na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa The Guardian
Limited, Kiondo Mshana, kuitwa polisi kuhojiwa kuhusiana na habari
kuhusu madai ya rushwa miongoni mwa askari wanaodhibiti ujambazi kwa
kutumia pikipiki, lakini hawakuhojiwa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda,
alisema mwaka huu ni wa kipekee kwa kuwa unahitimisha kipindi cha
utawala wa miaka 10 ya serikali ya awamu ya nne ikiwa na misukosuko ya
vyombo vya habari na waandishi wa habari.
“Wanahabari na wahariri wameingia kwenye misukosuko mikubwa,
kupoteza maisha, kujeruhiwa na kukamatwa na polisi, polisi kuvamia
vyombo vya habari kuwapiga na kuwajeruhi waandishi na kumwagiwa
tindikali na kufikishwa mahakamani,” alieleza na kuongeza:
“Tunahitimisha jinamizi la mateso kwa wanahabari na waandishi,
viongozi wanasema wasichomaanisha na kutishia waandishi wa habari…sheria
kandamizi zimepitishwa na Bunge, hili ni jinamizi hatari na tishio kwa
uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kupata habari.”
Kibanda alikumbushia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu
dhidi ya kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili yeye na wenzake kuwa kwa
mara ya kwanza mahakama ilithibitisha kuwa serikali ilifungua kesi hiyo
kwa misingi ya uonevu.
Aidha, aliutaka Umoja wa Ulaya (EU) kuingilia kati na kutoa tamko
kwani wakati wa kuumizwa, kuteswa na kujeruhiwa kwake (Kibanda), Waziri
mmoja alitoa taarifa potofu kwa mataifa ya nje kuwa alipatwa na janga
hilo kutokana na sababu za maisha yake binafsi na si masuala ya kazi. “Ninaitaka EU ije na kauli thabiti, kukaa kimya ni kuruhusu
serikali ijayo kuendeleza matukio haya zaidi ya ilivyosasa,” alisema.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Waandishi wa Habari Tanzania (TMF), Ernest
Sungura, alisema wamekumbana na mkono wa vyombo vya dola mara kadhaa na
kwamba ameshahojiwa mara tatu, watumishi wake mara mbili, polisi kufika
kwenye ofisi hizo na kutaka ushahidi na waliponyimwa waliahidi kutumia
nguvu za kisheria kuupata.
Alisema misukosuko hiyo imetokana na TMF kufadhili vyombo vya
habari na waandishi wa habari za uchunguzi ambazo zinagusa maslahi yao
moja kwa moja.
Mwakilishi wa Shirika la Ujerumani (Kas), Stefan Reith, alisema
Tanzania inahitaji sheria zinazotetea uhuru wa habari na vyombo vya
habari kwa utetezi wa demokrasia. “Serikali imesema Sheria ya Takwimu na Mitandao ni kwa ajili ya
usalama wa nchi, lakini cha kujiuliza ni kwa usalama wa nchi au usalama
wa watawala?” alihoji.
Makamu wa Rais wa Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari
Tanzania (UTPC), Jane Mihanji, alisema asilimia 80 ya waandishi hawana
mikataba na wanapewa malipo duni na hawana vitendea kazi. Alisema wanaangalia uwezekano wa kuanzisha vyama vya wafanyakazi
ili kupata stahiki zao na kwamba wataendelea kudai uhuru wa waandishi
wote na mmoja mmoja.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania
(MOAT), Henry Muhanika, alisema chama chake kitaunga mkono tamko ambalo
lilitarajiwa kutolewa baada ya mkutano huo jana jioni.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Kiongozi wa mabalozi wa EU
nchini, Balozi Filiberto Bregondi, alisema EU itaendelea kuishawishi
serikali kuheshimu haki za binadamu, haki ya kupata taarifa na huduma
kwa vyombo vya habari, kwa maendeleo endelevu ya taifa lenye misingi ya
demokrasia na utawala bora.
Naye Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini (UN), Balozi Alvero
Rodriguez, alisema mwaka huu ni muhimu kwa waandishi wa habari na vyombo
vya habari kuangalia mazingira ya uandishi wa habari katika chaguzi
zijazo na sheria mpya na wajibu wa kuimarisha ulinzi na usalama.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment