Rais Jakaya Kikwete akizungumza siku alipozindua Bunge la Katiba.
Anayefuata (kushoto) ni Spika wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta na Rais
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Wahenga walisema dalili ya mvua ni mawingi.
Usemi huo umejidhihirisha kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambao
tayari umeonyesha kuligawa taifa katika makundi matatu; Serikali,
taasisi za dini na vyama vya siasa. Dalili za vikwazo vya kukamilika kwa mchakato huo
zilianza kuonekana wakati wa Bunge la Katiba, ambako April 16 mwaka
jana, wabunge zaidi ya 200 wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), walisusia vikao vya Bunge hilo na kutoka nje.
Hata hivyo, hatua hiyo haikuonekana kuathiri Bunge
hilo kwa kuwa wajumbe wengine kutoka taasisi mbalimbali, kikiwamo chama
tawala CCM, United Democratic (UDP), Tanzania Labour (TLP) na UPDP,
waliendelea na mjadala.
Bunge hilo lilimalizika baada ya kupata zaidi ya
theluthi mbili ya kura kutoka pande zote mbili za Muungano, yaani
Tanzania Bara na Zanzibar, licha ya wajumbe wa Ukawa kulisusa.
Kitendo cha Ukawa kususia Bunge la Katiba
kilionekana kuchochea taasisi zingine kutoa matamshi mbalimbali ya
kutishia kuususia mchakato huo kama ifuatavyo;
Jumuia na Taasisi za Kiislamu
Mapema Februati mwaka huu, Jumuia na Taasisi za
Kiislamu zipatazo 11, zikiwamo Baraza Kuu, Tampro, Basuta, Jasuta, IPC,
Haiyat Ulamaa na Shura ya Maimamu Tanzania, zilitangaza kuwa zitafanya
kampeni za kuhamasisha wanajumuia wake kususia kupiga Kura za Maoni ya
Katiba Inayopendekezwa hadi pale watakapopata uhakika wa uwepo wa
Mahakama ya Kadhi yenye meno. Tangazo hilo lilitolewa na Naibu Katibu wa Jumuia ya Shura ya Maimamu Wilaya ya Kinondoni, Rajab Katimba.
Jumuia hizo zikaeleza kuwa kinachoendelea katika
mchakato wa upatikanaji wa Mahakama ya Kadhi, ni mwendelezo wa ulaghai
ambao umekuwa ukifanyika miaka yote hasa kinapofika kipindi cha kupiga
kura kwa lengo la kupata kura za waumini hao. Shehe Katimba anasema kuna baadhi ya taasisi za kidini na vyombo vya habari vinapotosha kuwa Mahakama ya Kadhi italeta vurugu.
Anasema kwamba Mahakama hiyo inatuhumiwa kuwa
itatoa adhabu za kikatili, ikiwamo kukata watu mikono, kuhukumu
wasiokuwa Waislamu na kuwabagua wasiokuwa Waislamu.
Shehe Abdallah Bawazir ambaye ni Makamu Mwenyekiti
wa Hay Atul-Ulamaa, akasema katika taarifa rasmi ya Jumuiya hiyo kuwa
muswada unaojadiliwa ili kupatikana Mahakama ya Kadhi ni kiini macho.
Bawazir katika taarifa hiyo anafafanua kuwa muswada huo unaitaka
Mahakama ya Kadhi ijiendeshe yenyewe bila kupata fedha kutoka
Serikalini kitu ambacho hakiwezekani.
“Zipo mahakama za makundi ya watu maalumu ambazo
zinaendeshwa kwa pesa za Serikali ambazo ni kodi za Watanzania wote.
Mfano ni kama vile Mahakama ya Kazi, Ardhi na Mahakama ya Biashara. Kwa
nini mahakama itakayotafsiri sheria za Kiislamu iwe nongwa?” alihoji.
Tamko la viongozi wa PCT
Machi 12, mwaka huu, Jukwaa la Kikristo Tanzania
(PCT) linaloundwa na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT)
na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) lilitoa tamko la kutounga
mkono Katiba Inayopendekezwa likidai kuwa katiba hiyo imeandaliwa katika
mazingira yasiyokuwa ya kiuadilifu.
Waraka wa baraza hilo, kwa vyombo vya habari
ulisainiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania
(KKKT), Dk Alex Malasusa kwa niaba ya (CCT), Rais wa Baraza la Maaskofu
Katholiki Tanzania Tracius Ngalalekumtwa (TEC) na Daniel Aweti kwa niaba
ya Wapentekoste (CPCT).
Katika tamko hilo PCT ilibainisha kwamba
kutokana na hali hiyo, kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa
Katiba Inayopendekezwa, hivyo liwataka waumini wao kuipigia kura ya
hapana.
Jukwaa hilo limeeleza kuwa Katiba Inayopendekezwa
haijajibu matakwa na malalamiko ya wananchi kwenye masuala mbalimbali
yanayohusu muundo wa Serikali, miiko na maadili ya viongozi wa umma,
uwiano wa mihimili ya dola, madaraka ya Rais na haki za binadamu.
“Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa
Katiba Inayopendekezwa kutokana na hali hii, hivyo basi Jukwaa
linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na
kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na
kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana,” ikasema sehemu ya
taarifa hiyo.
Hatua ya Serikali
Siku chache baada ya kauli ya viongozi hao, Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alitangaza hatua ya Serikali
kukusudia kuzifutia usajili taasisi mbalimbali za kidini, endapo
zitabainika kukiuka sheria ya vyama vya kijamii. Chikawe akasema kinachofanywa na taasisi hizo ni
kinyume cha sheria ya vyama vya kijamii Sura ya 337 na kanuni zake
inayosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
“Kuanzia Aprili 20, mwaka huu taasisi
zitakazoshindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za mwaka pamoja
na kulipa ada zao zitachukuliwa hatua,” akaeleza Chikawe.
“Viongozi wa taasisi hizi, wanapokutana na kutoa matamko
yanayolenga kuwashawishi waumini wao wafuate maelekezo yao kuhusu
masuala ya Katiba Inayopendekezwa au uchaguzi mkuu ujao, matamshi kama
hayo yanakiuka sheria za usajili wa taasisi hizo,” anasema Chikawe.
Wachambuzi wanasemaje?
Dk Benson Bana anaeleza kuwa “Si vizuri kukataza
watu kushiriki zoezi halali kisheria, aidha siyo vizuri kuanza kujenga
tabia ya kushinikiza mamlaka halali kufanya uamuzi kukidhi matakwa ya
vikundi shinikizi.”
Kwa mujibu wa Dk Bana ambaye ni Mhadhiri katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika masuala ya utawala na siasa
kufanya hivyo ni kujenga msingi mbaya kinyume na utawala bora.
Anasema Sheria ya Kura ya Maoni ipo wazi kwamba
kambi zinazotakiwa ni inayoikubali mapendekezo yaliyopo na kambi
inayoyakataa mapendekezo hayo. Kundi lolote linaruhusiwa kuhamasisha
upande unaotaka.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment