Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe, amesema kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania
dhidi ya Dola ya Marekani kunakoshuhudiwa hivi sasa, kunaiweka nchi
katika shaka kubwa ya maendeleo kiuchumi.
Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, kuporomoka kwa Shilingi kutaendelea kuathiri uwekezaji mkubwa nchini. Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, alisema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya
Chadema cha siku mbili, kilichoanza jijini Dar es Salaam jana.
Alisema hali hiyo inatokana na wawekezaji kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya kisiasa na hatima ya uchaguzi mkuu. “Kwa hiyo, uchumi utazidi kuathirika zaidi kwa siku zijazo iwapo kitendawili hicho hakitatatuliwa,” alisema Mbowe.
Alisema anashangazwa kuona namna Rais Jakaya Kikwete anavyoendelea
kukaa kimya, huku akishuhudia jinsi uchumi unavyoyumba, uwekezaji
unavyozidi kuzorota na sarafu ya Tanzania inavyozidi kuporomoka kwa
sasa.
UCHAGUZI MKUU
Mbowe alisema taifa liko njia panda kutokana na wakuu wa serikali,
akiwamo Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kukimbia kuzungumza
ukweli kwamba uchaguzi mkuu uko shakani. Alisema ni wazi kwamba, mazingira ya nchi kuelekea uchaguzi huo
hayako sawa kutokana na kuwapo ishara zote zinazoonyesha unaweza
usifanyike.
Aliwashauri viongozi wakuu wa Taifa kuwa na utashi wa kuwa wakweli
kuhusu suala la uchaguzi mkuu na kura ya maoni kuliko kuendelea
kulidanganya Taifa. “Ili nchi iwe na utulivu na usalama, lazima iwepo hali ya
kutabirika. Angalau ijulikane nini kinafuata ndani ya miezi mitatu au
mwaka mmoja ujao. Lakini kwa sasa hali hiyo haipo. Suala hilo linaleta
mashaka makubwa kuhusu taifa linakoelekea,” alisema Mbowe.
Alisema serikali inastahili kulaumiwa kwa sasa kwa sababu
imeshindwa kuwaandaa wananchi kuelekea katika uchaguzi huo, huku wengi
wao wakiwa njia panda, hawajui kama uchaguzi upo au haupo. Mbowe alisema hadi wakati huu hakuna mwelekeo wa kujua lini uandikishaji wa wapiga kura katika mfumo mpya wa BVR utafanyika.
Hata hivyo, alisema Rais Kikwete amekuwa akiendelea kusisitiza
kwamba, kura ya maoni lazima iwepo na uchaguzi mkuu lazima utafanyika
kwa wakati, wakati suala hilo linaloonekana kuwa ni ndoto. “Kimsingi ni kwamba tunaona mazingira yote ya kufanyika kwa
uchaguzi mkuu hayapo. Hata kama wanataka kulazimisha kwa kauli zao
kwamba ufatanyika,” alisema Mbowe.
MREMA: UMAKINI WA SERIKALI UNATIA MASHAKA
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema,
ameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuokoa Shilingi ya Tanzania,
ambayo imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 dhidi ya dola ya Marekani
ili kunusuru uchumi wa nchi.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na
serikali.
Mrema, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alisema kwa hali ilivyo,
serikali bado haijachukua hatua za kutosha kukabiliana na tatizo hilo na
hivyo kutia shaka umakini wake katika kushughulikia mambo muhimu
yanayowagusa wananchi. “Ninachokiona ni kwamba, serikali inachukua suala la kuporomoka kwa
Shilingi ya Tanzania kama ni jambo la kawaida. Na ndiyo maana
imeshindwa kuweka mkazo katika kushughulikia tatizo hilo,” alisema
Mrema.
Alisema kama tatizo hilo litataendelea kuwapo hata baada ya
uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu, hali ya maisha ya
Watanzania itazidi kuwa mbaya. Mrema alisema viongozi waandamizi wa
serikali wanalichukulia suala hilo kirahisi kwa sababu wana fedha nyingi
na kwamba wakati wa mkutano wa 20 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, unaotarajia kuanza Mei 12 mwaka huu, atahakikisha anaibana
serikali itoe majibu ya namna itakavyokuwa imeshughulikia tatizo hilo.
Kuhusu uchaguzi mkuu, aliwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Alisema ili kufanya mabadiliko ya uongozi na kukiondoa chama tawala
(CCM) madarakani, wananchi wanahitajika kujitokeza kwa wingi kushiriki
uchaguzi mkuu na kwamba, chama chake kitahakikisha kinaibana serikali
ili kazi ya uandikishaji wapigakura ikamilike kwa wakati.
Kinana (Katibu Mkuu wa CCM ), anang’ang’ana kupambana na Mrema
kumhujumu jimboni wakati serikali ya chama chake imeshindwa kuyapatia
ufumbuzi matatizo ya msingi yanayowagusa wananchi,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment