Social Icons

Pages

Wednesday, May 13, 2015

TUSUBIRI MOSHI MWEUPE URAIS 2015


Hakika kama Watanzania wote tungekuwa waumini wa Kanisa Katoliki, tungesema tunasubiri ‘moshi mweupe’ kwa hamu ili kumjua Rais wa awamu ya tano atakayemrithi Jakaya Kikwete.
Moshi mweupe ni ishara inayotumika kuashiria waumini na dunia kuwa makadinali wa Kanisa Katoliki, wamempata Papa mpya katika uchaguzi unaofanyika kwa usiri mkubwa huko Vatican.
Ingawa moshi huo ukitoka, dunia huwa  haijui kwa jina nani aliyechaguliwa, lakini angalau husaidia kupunguza presha kwa waumini wa kanisa hilo na dunia kwa jumla.
Hali hii ndiyo inayowakumba Watanzania hivi sasa, kwa sababu Januari 2005, walikuwa wameshahisi kama si kuwa na uhakika, ni nani angemrithi Benjamin Mkapa. Japokuwa tulikuwa hatujafika kwenye hatua ya sanduku la kura, lakini angalau Aprili kama siyo Januari 2005, Watanzania wengi ndani ya mioyo yetu tulishamfahamu Rais wa Awamu ya Nne.
Leo hii ikiwa ni Mei 13, tukiwa tumebakiza siku takriban 170 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba, Watanzania tuko gizani. Ni kama nchi imesimama vile. Nani atakuwa Rais?
Hakuna ubishi kigezo kikubwa cha nani atakuwa Rais kitategemea zaidi nani atateuliwa kupeperusha bendera ya CCM. Hapa ndiyo tungekuwa na uthubutu wa kusema huyu ‘ndiye Rais wa awamu tano’.
Tungemfahamu kwa dhati ni nani kwa upande wa CCM, atakayepitishwa na vikao vya juu vya chama hicho kumrithi Rais Kikwete. Tungekuwa na nafasi ya kupima pia na upande wa pili kisha tungepata muda wa kuwatathmini wagombea na kuona ni yupi anayefaa na kukubalika.
Nilitangulia kusema CCM ndiyo kipimo cha Rais ajaye, kwamba kitakapoboronga tu kinaweza kutoa nafasi kubwa zaidi kwa upinzani kuchukua nchi kilaini.
Hata hivyo, hakuna anayejua kwa dhati ndani ya CCM ni kada yupi atateuliwa ili kuipeperusha bendera yake. Kila aliyejaribu kunyanyua kichwa alikalishwa chini ama kwa kuambiwa anakiuka kanuni au anaanza kampeni mapema.
Rais Kikwete mwenyewe ndiye amebaki na siri hii nzito moyoni huku  Watanzania wakiumia kichinichini. Hakika nchi imesimama. Wamejitokeza makada wa CCM zaidi ya 12 ambao wameonyesha nia au kutajwatajwa, lakini yule ambaye Watanzania wanamtaja kwa kiwango kikubwa, ameanza kujengewa hofu kuwa jina lake litakatwa.
Tena taarifa hizi za ‘redio mbao’ zinadai jina la mwanasiasa huyo (usiniulize ni nani) litakatwa katika hatua za mwanzo kabisa katika vikao vya Kamati Kuu, lakini ukweli  na uongo wake anaujua Rais Kikwete. Kama nilivyotangulia kusema, bila kumjua mgombea wa CCM, si rahisi hata kidogo kujua kama safari hii Rais wa Awamu ya Tano atatoka CCM au atatoka ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Nimesema tangu mwanzo kuwa nchi imesimama, kila mtu anaongea lake. vijiweni, kwenye baa, vyuoni, sokoni, viwanjani kote watu wanaulizana swali moja tu; ‘nani Rais wa Awamu ya Tano?’
Kutojulikana mapema kwa mgombea wa CCM (japo siyo rasmi) na kusuasua kwa uboreshaji Daftari la Wapigakura kwa njia ya Kielektroniki (BVR), kunaongeza wasiwasi wa kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu. Japo Rais Kikwete anayemaliza muda wake, amewatoa hofu Watanzania na kueleza kuwa uchaguzi uko palepale, lakini bado hesabu zinakataa kama tutakwenda na mwendo huu wa kusuasua wa BVR.
Nasema nchi imesimama kwa vile hata wabunge wetu nao viti vyao ni vya moto, wamesimama mguu mmoja ndani na mguu mmoja nje. Hawajui kwa dhati wasimame upande upi. Hali ni tete. Japokuwa sisi raia wa kawaida tunaiona hali hiyo, lakini Rais wetu anayemaliza muda wake ambaye ni mwenyekiti wa Taifa wa chama tawala anaonekana kuwa kimya, kana kwamba hali ni shwari.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba kuna moto mkubwa unawaka ndani ya CCM na moto huu ndiyo ambao unawatia shaka Watanzania na kuhoji: ‘tutavuka salama 2015?’. Kila mmoja anajiuliza swali hili. Tunajiuliza swali hili kwa sababu moja kuu; CCM itakapoboronga katika uteuzi chama hicho kitabaki salama? Je, kama upinzani utashinda, CCM imejiandaa kisaikolojia kuachia madaraka?
Ndiyo maana nilitangulia kusema Watanzania tunasubiri ‘moshi mweupe’, tukikosea na ukatoka moshi mweusi, hakika kutakuwa hakuna mahali pa kutokea.
Narudia tena tunausubiri kwa hamu moshi mweupe.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: