Social Icons

Pages

Wednesday, May 13, 2015

VITAMBULISHO VYA TAIFA VYALALAMIKIWA

Kazi ya uchukuaji alama za vidole na picha kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa, imeanza mjini Tanga na dosari kadhaa zimeripotiwa, ikiwamo wananchi kusota muda mrefu kwenye vituo.
Gazeti hili lilitembelea vituo mbalimbali tangu mwishoni mwa wiki iliyopita na kukutana na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi. Katika Kituo cha Gongagonga kilichopo Msambweni, wananchi walilalamika kusimama kwenye foleni muda mrefu, lakini pia wakakosoa ufanyaji kazi polepole wa watendaji.
Kadhalika, wananchi wengi walishindwa kutofautisha kazi hiyo na ile ya kuandikisha watu kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura. Hata hivyo, baadhi ya maofisa waliokuwa wanasimamia kazi hiyo, walidai kasoro zinazolalamikiwa ni za kawaida katika uandikishaji.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdullah Lutavi alisema jana kuwa kazi ya uandikishaji katika wilaya hiyo itadumu kwa siku saba. “Kuna makundi mawili, moja lilianza Mei 10 hadi 17 mwaka huu, likijumuisha Kata za Central, Nguvumali, Chumbageni na Ngamiani Kaskazini.
“Kata zingine ni Ngamiani Kati, Ngamiani Kusini, Majengo, Usagara, Makorora, Mabawa, Mzingani, Duga, Marungu na Maweni,” alisema mkuu huyo wa wilaya na kuongeza.
Kundi la pili litaanza Mei 16 hadi 23 mwaka huu na kuzihusu kata za Chongoleani, Mabokweni, Kiomoni, Mzizima, Pongwe, Tangasisi, Kirare na Tongoni.”

CHANZO: MWANANCHI

No comments: