Social Icons

Pages

Wednesday, May 13, 2015

SERIKALI SASA KUFUTA MIKATABA YA WAKANDARASI WAZEMBE

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Serikali iko mbioni kufuta mikataba ya wakandarasi walioshindwa kukamilisha kazi ya kusambaza umeme vijijini kwa wakati uliopangwa.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema hayo juzi alipohutubia wananchi wa Kata ya Mlunduzi wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma baada ya kukagua miradi ya umeme.
Alisema katika maeneo mengi kazi hiyo imesimama huku wakandarasi wakilipwa fedha nyingi.
“Serikali haiko tayari kucheka na wakandarasi wazembe wanaoshindwa kwenda na kasi inayotakiwa. Natangaza kuanzia leo kuwa tutawafutia mikataba na watarudisha fedha ya umma,” alisema Simbachawene.
Waziri alisema wakandarasi hao wamekuwa wakipoteza muda kwa kuzunguka wakati wote, huku nguzo zikiwa zimelazwa chini na wananchi ndiyo walinzi.
Mkazi wa Mlundizi, Jackson Lengwa alisema wamekuwa wakishangazwa na Serikali kujisifu kuwa umeme unasambazwa wakati wakandarasi hufanya kazi wanapowaona viongozi.
Lengwa alisema kauli ya Waziri Simachawene itakuwa na maana zaidi endapo itatekelezwa kwa vitendo.
Mwakilishi wa Kampuni ya Derm Electricity, Aziz Msuya alisema usambazaji wa umeme wilayani Mpwapwa umefikia asilimia 52 ingawa kwa Mkoa wa Dodoma wamesambaza kwa asilimia 75. Msuya alisema wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha kazi hiyo inakwisha kwa wakati waliokubaliana na Serikali na hawatakubali kukatisha mikataba yao.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: