
Wakati CCM
ikifanya jitihada za kudhibiti makada wake wanaotajwa kuwania urais,
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amemtuma waziri mkuu wa zamani,
Edward Lowassa kuendesha moja ya shughuli ambazo chama hicho kinaamini
kuwa ni moja ya majukwaa ya kampeni kwa wagombea.
Dk Bilal amemtuma Lowassa, mmoja wa makada
wanaotajwa kutaka urais, kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa
msikiti wa Patandi mkoani Arusha Alhamisi wiki hii, ambako habari
zinasema siku mbili baadaye huenda mbunge huyo wa Monduli akatangaza
rasmi nia yake ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu kwa tiketi ya CCM.
Taarifa iliyotolewa jana na mwandishi wa habari wa
Makamu wa Rais, Boniface Makene inaeleza kuwa Dk Bilal anakabiliwa na
majukumu mengine ya kitaifa na hivyo ametoa ombi maalumu la kuwakilishwa
kwenye harambee ya kukamilisha ujenzi wa msikiti huo ulioanza mwishoni
mwa miaka 90.
“Makamu wa Rais ameona kuwa shughuli hii ya
uchangiaji wa ujenzi wa msikiti isisogezwe mbele kumsubiri, bali
iendelee kwa kuwa anaamini Lowasa ana uzoefu katika kufaninikisha
shughuli za aina hii. Pia mchango wake katika shughuli za harambee
katika shughuli ni wa mfano,” inasema taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa mchango wa
wanajamii wanaoswali katika msikiti wa Patandi ni mkubwa kwani wamekuwa
wakijitoa kwa namna nyingi kujenga mshikamano baina ya jamii
zinazowazunguka bila kuwa na vikwazo na wameshiriki kuwasaidia watoto
yatima.
Uamuzi huo wa Dk Bilal, ambaye kwa nafasi yake
anaingia kwenye vikao vyote vya juu vya chama tawala, vikiwamo vya
Zanzibar, utakuwa umetikisa harakati za kudhibiti baadhi ya makada
wanaotajwa kuwania urais, hasa kambi ya Lowassa ambayo inasemekana
inalalamikia kuchezewa rafu na uongozi wa CCM, ingawa haijabainisha rafu
hizo.
Lowassa ni mmoja wa makada sita waliopewa onyo
kali na CCM Februari mwaka jana, likiwazuia kujihusisha na uchaguzi kwa
zaidi ya miezi 12 baada ya kubainika kuwa walianza kampeni mapema kwa
kushiriki vitendo vinavyokiuka maadili, zikiwamo za harambee na hivyo
kutakiwa kuomba kibali kabla ya kushiriki.
Hata hivyo, wiki mbili zilizopita Lowassa na
makada wengine wanaotajwa kuwania urais walialikwa Zanzibar kwenye
harambee ya kuchangia mfuko wa maendeleo wa mkoa mpya wa Magharibi,
ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki tangu walipofungiwa na chama hicho
mwaka jana.
Wasomi waliotafutwa na Mwananchi kuzungumzia uteuzi huo walikuwa na maoni tofauti. “Sina mengi, hakuna atakayeshindwa kuona kuwa wana
mu-endorse (wanamuunga mkono) huyo. Yeye (Lowassa) ni miongoni mwa watu
wanaotajwa kuwania urais, kwa hiyo hii ni moja ya ‘technic’ mbinu,”
alisema Profesa Tolly Mbwete ambaye ni mkuu wa Chuo Kikuu Huria.
Alisema uteuzi huo ni miongoni mwa harakati za kumuweka vizuri Lowassa katika uchaguzi ujao.
Lakini mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema iwapo Lowassa amepewa
jukumu hilo na Dk Bilal, maana yake ameonekana ana uzoefu na anaifahamu
kazi hiyo na aangaliwe kama waziri mkuu mstaafu na si vinginevyo.
Dk Makulilo alisema kuteuliwa kufanya kazi ya harambee hiyo
wakati kama huu kunatafsiriwa kama ni kitendo cha kupigiwa chapuo
kisiasa katika uchaguzi mkuu. “Lakini Lowassa ana ujuzi, kwa sababu ni waziri
mkuu mstaafu, lakini katika siasa hakuna shida ya kumtumia kiongozi huyo
kwa sababu aliwahi kufanya harambee nyingi za kiserikali, kichama na za
kwake binafsi,” alisema.
Dk Makulilo alisema kupewa kwa Lowassa kuifanya kazi hiyo kunachanganywa na nafasi yake ya kutaka urais na makundi ndani ya CCM.
Kabla ya kufungiwa, Lowassa alikuwa akipata
mialiko mingi ya kushiriki katika harambee za vikundi mbalimbali vya
kijamii ikiwa ni pamoja na makanisa, misikiti na vikundi vya wasanii na
kufanikisha kupatikana mamilioni ya fedha.
Tangu apewe adhabu hiyo, Lowassa amekuwa kimya na
badala yake vikundi vya watu mbalimbali vimekuwa vikienda jimboni kwake
Monduli mkoani Arusha na kwenye makazi yake akiwa bungeni mjini Dodoma
kumshawishi aingie kwenye mbio za urais.
Lakini wakati vikundi hivyo vikizidi kumiminika,
viongozi wa CCM walianza kutoa kauli za kuponda vitendo vya kushawishi
makada wa chama hicho kugombea urais, wakisema kuwa ni mchezo wa
kuigiza.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alikaririwa akidai kuwa watu waliokuwa wakienda nyumbani kwa kada wa
chama hicho, ambaye hakumtaja jina, kwa lengo la kumshawishi achukue
fomu za kuwania urais, walikuwa wanapangwa kwa kuwa mwanachama huyo
alishatia nia na ndio maana alianza mapema kampeni zilizosababisha apewe
adhabu.
Nape amekuwa akikaririwa mara kwa mara akitoa
kauli zinazoonyesha kukinzana na kambi ya mbunge huyo wa Monduli na
wakati fulani Lowassa, bila ya kumtaja katibu huyo wa uenezi wa CCM,
alisema madai hayo ni ya kipuuzi na kwamba hawezi kumjibu kwa kuwa
akifanya hivyo atampa umaarufu.
Vita ya urais kwa tiketi ya CCM imekuwa na sura
tofauti na inazidi kupamba moto kadri siku za kuanza kwa mchakato wa
Uchaguzi Mkuu zinavyokaribia.
Mapema wiki hii ulienea ujumbe kwenye mitandao
unaoonyesha kuwa Lowassa ameguswa na maombi ya wananchi ya kumtaka
agombee urais na kwamba amepanga kutangaza rasmi uamuzi wake Jumamosi
kwenye hafla itakayofanyika mjini Arusha.
Kambi ya Lowassa ilijitokeza mapema kupinga
taarifa hiyo ikisema kuwa haikutumwa na mwandishi wa mbunge huyo wa
Monduli, Aboubakar Liongo na kwamba taarifa zinazotolewa na ofisi ya
kada huyo huwa hazimuelezei kuwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa
Lowassa anaweza kutangaza rasmi uamuzi wake wa kuingia kwenye mbio hizo
Jumamosi kwenye Uwanja wa NMC mjini Arusha baada ya uwanja wa chama
chake wa Sheikh Amri Aneid kufungwa.
Hivi sasa kuna kesi Mahakama Kuu ambako makada wawili wa CCM,
John Guninita, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Dar es
Salaam, na Hamisi Mgeja, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho mkoani
Shinyanga, wamefungua kesi dhidi ya mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana
wa CCM, Paul Makonda kwa madai kuwa aliwadharirisha.
Makonda ambaye kwa sasa ni mkuu wa wilaya ya
Kinondoni anadaiwa kuwaelezea wawili kuwa ni vibaraka wa Lowassa
kutokana na kueleza msimamo wao kwa mbunge huyo wa Monduli.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment