Social Icons

Pages

Monday, May 04, 2015

DK. AUGUSTINE MAHIGA, BALOZI MSTAAFU UMOJA WA MATAIFA



Dk Augustine Mahiga. Aliendelea na masomo ya sekondari hapahapa nchini na mwaka 1968, alijiunga katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es Salaam na kuhitimu Shahada ya Sanaa akibobea kwenye elimu mwaka 1971.
Historia yake
Dk Augustine Mahiga alizaliwa Agosti 28, 1945 huko Tosamanganga, Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa (atatimiza miaka 70 ifikapo Agosti mwaka huu). Amesoma elimu ya msingi katika shule za Serikali enzi ya mkoloni na alihitimu darasa la VIII muda mfupi baada ya uhuru. Safari ya elimu ya Dk Mahiga ilikuwa ya umaskini uliopitiliza, alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa kutokuwa na fedha za kulipia mashuka na mablanketi hadi aliposaidiwa na msamaria mwema kutoka Shirika la Kennedy wakati huo.
Aliendelea na masomo ya sekondari hapahapa nchini na mwaka 1968, alijiunga katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es Salaam na kuhitimu Shahada ya Sanaa akibobea kwenye elimu mwaka 1971.
Mwaka huohuo, Dk Mahiga alipata ufadhili na kuendelea na masomo ya juu nchini Canada katika Chuo Kikuu cha Toronto ambako alihitimu Shahada ya Uzamili. Aliendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika chuo hichohicho akijikita katika Uhusiano wa Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975.
Mwaka huohuo 1975 (akiwa na miaka 30), Dk Mahiga alirejea nchini akiwa daktari wa falsafa kitaaluma na alipangiwa kazi ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mhadhiri katika Idara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kikanda. Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977 alipohamishiwa katika Ofisi ya Rais kuwa Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo na alidumu hapo akifanya kazi pamoja na Mwalimu Julius Nyerere hadi mwaka 1980.
Kati ya mwaka 1980 hadi 1983, Dk Mahiga alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Nafasi hii aliitumikia kwa weledi mkubwa katika historia ya watu waliowahi kuitumikia, aliweza kuifahamu nchi vizuri na mifumo yake kwa mtizamo wa ndani na nje.
Mwaka 1989 hadi 1992, aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa akifanyia kazi Geneva – Uswisi na mwaka 1992 hadi 1994, Balozi Mahiga aliteuliwa kuwa Kiongozi (Mwakilishi) wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi duniani (UNHCR) mjini Monrovia, Liberia na huu ndiyo wakati aliponusurika kuuawa na Majeshi ya Rais Charles Taylor, kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kuna wakati akiwa katikati ya operesheni ya wakimbizi hapo Monrovia, Serikali ya Tanzania ilimteua kuwa Balozi na kumuongezea jukumu jingine zito.
Mwaka 1994–1998, Balozi Mahiga alihudumu akiwa Mratibu na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni ya Dharura ya Ukanda wa Maziwa Makuu akifanyia kazi hiyo kutokea Geneva–Uswisi na kati ya mwaka 1998 – 2002 aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu (Mwakilishi) wa Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) huko mjini Delhi India kabla ya kuteuliwa tena kuwa mwakilishi wa shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na Jamhuri ya San Marino kati ya mwaka 2002 – 2003.
Balozi Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010 na alishiriki kikamilifu katika mipango ya kimataifa pamoja na kusimamia mazungumzo ya kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani (mwaka 2005). Pia kushiriki kwenye masuala ya maingiliano ya serikali mbalimbali na makundi yanayofanya kazi zisizo rasmi, maendeleo, amani, usalama na ujenzi wa ushirikiano wa uhakika kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Balozi Mahiga alirejesha heshima ya Tanzania hadi kuwa mojawapo ya nchi zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi yetu ilipopata heshima hiyo, yeye aliteuliwa kuwa mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika Baraza hilo, hii ilikuwa ni mwaka 2005.
Dk Mahiga ameoa na ana watoto watatu.

Mbio za ubunge
Wanasiasa wengi ambao baadaye huongoza nchi huanzia katika uwakilishi wa ngazi za chini kama ubunge huku wakipanda juu. Balozi Mahiga hajapitia njia hii, hakuwahi kuwa mbunge wala mwanasiasa moja kwa moja, maisha yake yote amekuwa kiongozi wa kimataifa lakini akiifahamu na kuiwakilisha vizuri Tanzania.

Mbio za urais
Dk Mahiga alianza kuhusishwa na mbio za urais muda mrefu tu, wala haikuanza leo. Yeye mwenyewe aliamua kuvunja ukimya na kuzungumzia jambo hilo Aprili akiwa mjini Iringa. Alilieleza gazeti moja kuwa “…anafuatwa na makundi ya watu wanaomshawishi achukue fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM, lakini hajatoa jibu”.
Kauli hii ya Dk Mahiga inahusishwa na ile kauli ya Rais Kikwete katika maadhimisho ya CCM, Songea – Ruvuma kuwa “…watu wanaofaa kuwa marais, bado hawajajitokeza na kwamba wapo wengi tu”.
Katika kuonyesha kuwa huenda amedhamiria kuingia katika kinyang’anyiro, alikwenda mbele zaidi na kueleza kuwa ikiwa ataamua kugombea, akapitishwa na CCM na kushinda urais, masuala atakayoyapatia kipaumbele ni pamoja na “uimarishaji wa demokrasia, kuongeza uwajibikaji, kuimarisha maadili, kuboresha mwelekeo wa uchumi, kilimo, kuimarisha reli na kupambana na rushwa”.

Nguvu yake
Dk Mahiga ni mtu wa kujisimamia na mara nyingi hafungwi na mitizamo au matakwa ya kikundi chake ikiwa mitizamo na matakwa hayo havina manufaa. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipotoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Dk Mahiga hakujali misimamo na matakwa ya chama chake katika kukosoa waraka ule. Wakati CCM ilikuwa inapinga kwa nguvu suala la Serikali tatu, yeye alieleza kuwa muundo huo umekuja kwa wakati muafaka. Alisisitiza kuwa Rasimu ile ya Kwanza imebeba majibu na kero zote za Muungano. Kiongozi huyu ana msimamo wa kipekee.
Katika kupongeza na kuunga mkono msimamo na mtizamo wa Dk Mahiga kuhusu Rasimu ya Kwanza ya Katiba, mwanahabari na mchambuzi maarufu wa masuala ya kijamii na kisiasa, Maggid Mjengwa aliandika kwenye mtandao wake wa Facebook kuwa “…na kwa kusoma alama za nyakati. Ukiniuliza leo swali hilo jibu langu liko wazi kabisa, kuwa tuwe na Serikali Tatu; ya Muungano, Zanzibar na Tanzania Bara (Tanganyika) na hii si heshima tu tutakayoipata kimataifa, bali itachangia kwa watu wa pande mbili hizi za Muungano kuheshimiana na kushirikiana zaidi”.
Dk Mahija ni kati ya wasomi wachache waliopata kufanya kazi na kuteuliwa kushikilia madaraka na mamlaka makubwa ya nchi na marais wote wa Tanzania, kuanzia Mwalimu Nyerere, Mwinyi, Mkapa na sasa Kikwete. Mzee huyu ana uzoefu usio na mfano.
Tatu ni uwezo na usomi wake. Dk Mahiga ni msomi wa haja aliyebobea na aliyetoka mbali. Watu kadhaa waliofanya naye kazi UN wanasema kuwa akianza kuongea katika viunga vya UN lazima kila mtu atamsikiliza, ana ushawishi wa kipekee linapokuja suala la kusimamia masuala ya msingi na hii ni sifa muhimu kwa kiongozi wa nchi.

Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa wa Balozi Mahiga ni kutofahamika kwa wananchi wa kawaida. Nilipokuwa nafanya utafiti juu ya balozi huyu nilishangazwa nilipomhoji mwalimu mmoja wa kiwango cha juu katika Chuo cha Diplomasia (Kurasini) na hakuwa anamfahamu Balozi Mahiga, hata nilivyojaribu kumfafanulia kumhusu bado hakumuelewa. Kwa mtu yeyote ambaye anahitaji kuongoza dola, kufahamika kwa watu wa kati na chini ni jambo la lazima.
Udhaifu wake mwingine ni uungwaji mkono duni ndani ya chama. Ndani ya CCM tayari kila mtu ana mgombea wake. Watu wanaopendekezwa dakika hizi za mwisho wana nafasi ndogo ya kupata uungwaji mkono na makundi yaliyogawanyika ndani ya chama hicho na karata waliyonayo ni “ikiwa tu watapigiwa chapuo na viongozi wakuu wa CCM.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama kuna jambo linamtofautisha Dk Mahiga na wagombea wote wa CCM mwaka huu ni uzoefu wa kimataifa, hakuna mwana CCM wa kumfananisha naye kwa sasa. Huyu ni mwanadiplomasia aliyebobea labda akishindana na watu kama Dk Salim Ahmed Salim (ambaye amekwishatangaza kuwa hatahusika na vinyang’anyiro vya kusaka uongozi wa nchi tena).
Ikiwa CCM itahitaji mtu ambaye anakubalika kimataifa na amekwishafanya kazi kubwa za kimataifa zinazoheshimiwa, basi Balozi Mahiga ndiye atakuwa chaguo la kwanza. Hata Februari mwaka huu, gazeti moja la kila wiki nchini, lilimtaja kama “mwanadiplomasia anayeheshimika kuliko wote nchini Tanzania”.
Jambo jingine linampa nafasi ya kupitishwa ni kutokuwa na kundi la kukigawa chama hicho na hasa kutokuwa karibu hata na makundi mengine. Jambo hili si la kupuuza hasa ikiwa CCM itahitaji kuwa na Rais anayeheshimika na atakayeungwa mkono na “mapande makubwa ya urais” yanayosigana ndani ya chama hicho.
Lisemwalo lipo, kama halipo basi linakuja. Kauli ya Rais Kikwete “kubeza” wagombea waliojitangaza kwa kusisitiza kuwa hajaona Rais kati yao si ya kudharau. Baba yangu aliwahi kunisisitiza kuwa ukisikia mtu mzima anasema neno lolote hata kama ni la kipuuzi au kiutani usilidharau.
Watu ambao wamepata bahati ya kuongoza nchi kama Rais Kikwete wana matatizo mengi vichwani, mizigo ya matatizo ya nchi inakuwa imewaelemea na hutamka baadhi ya mambo ili kujipunguzia mambo yanayowasumbua. Wachambuzi wa siasa watakubaliana nami kuwa huenda Rais Kikwete amechoshwa na mivutano na pilikapilika zisizo salama za wagombea nguli wa chama chake na suluhisho linaweza kumpata mtu ambaye hategemewi wala kujulikana sana, Balozi Mahiga anaweza kupenya kwenye mlango huu.
Nini kinaweza kumwangusha?
Baadhi ya watu muhimu na wakongwe niliobadilishana nao mawazo ndani ya CCM wanatoa maoni kuwa hapajapata kutokea mtu mwenye umri mkubwa akakabidhiwa uongozi kupitia CCM. Umri wa Balozi Mahiga wa miaka 70, unachukuliwa kama mkubwa utakaovunja rekodi ndani ya chama hicho na hata nchi.
Wakongwe hawa wana hofu na mamilioni ya wapigakura vijana watakaoongezeka ambao chaguo lao kuu linaweza kuwa wagombea wenye umri wa kadri. Mfano thabiti ni kuwa Mwalimu Nyerere alianza kuongoza Tanzania akiwa na miaka 40, Mwinyi alikuwa na miaka 60, Mkapa 57 na Kikwete alianza akiwa na 55. Hofu hii ya wakongwe wa chama hicho si ya kuidharau, ichukuliwe kwa uzito mkubwa kama moja ya vinavyoweza kuwa vitanzi vya Balozi Mahiga.
Jambo la pili linalowapatia shida wana CCM wakongwe ni Kutojulikana kwa Dk Mahiga. Nilipohoji kuwa hata Mkapa alipoteuliwa mwaka 1995 hakuwa anajulikana walinijulisha kuwa Mkapa alijulikana ghafla kwa sababu watu walikuwa wanamsikia bila kumtilia maanani wakati akiongoza wizara mbalimbali, pili alijulikana haraka kwa sababu mtu wa kumnadi alikuwapo, Mwalimu Nyerere. Vigogo hawa wanasema kuwa ikiwa Dk Mahiga atapitishwa, wanachama wengi wasiomfahamu vizuri watakatishwa tamaa na umaarufu wa wagombea wengine hususan kutoka Ukawa. Mbaya zaidi, inasisitizwa kuwa katika kampeni za mwaka huu, mgombea wa CCM hatakuwa na mtu imara wa kumnadi, zaidi ya umaarufu wake na rekodi.
Jambo jingine linaloweza kumhukumu Balozi Mahiga, ni msimamo wake kuunga mkono Serikali tatu. Nilikuwa Dodoma kwenye Bunge Maalumu la Katiba (BMK) na nilijionea mwenyewe, “kuunga mkono serikali tatu kwa mwana CCM kulikuwa ni dhambi kuliko kuua”. Dk Mahiga amewahi kuweka msimamo wake akiunga mkono muundo huo, kama hatakuja tena hadharani kugeuka msimamo wake wa awali, atajengewa hoja nzito kuwa yeye si muumini wa Muungano, kwa sababu ndani ya CCM, mtu anayeunga mkono Muungano lakini kwa serikali tofauti na mbili, anachukuliwa kama “mtu mwenye njama za kuvunja muungano”. Hili ni jambo zito kwa Dk Mahiga.
Asipopitishwa (Mpango B)
Balozi Mahiga atakuwa na mipango kama minne ya kufuata ikiwa hatapitishwa kugombea kwa CCM.
Moja itakuwa ni kustaafu utumishi umma kwa majukumu ya moja kwa moja (majukumu ya kila siku) kwa sababu umri wake huenda kwa sasa unahitaji mapumziko na kujenga afya thabiti ya uzeeni kuliko kuendelea kukimbizana. Katika mapumziko haya ndipo anaweza kuwa anaishauri Serikali juu ya mustakabali wa mambo ya ndani na nje ya nchi.
Pili, anaweza kuendelea kuhudumu kimataifa katika misheni za muda mfupi za utatuzi wa migogoro barani Afrika na kwingineko. Yeye ni mzoefu kwenye eneo hilo na anaweza kuendelea kutoa msaada.
Tatu, ni kurudi kusaidia ulezi wa wanafunzi vyuoni ikiwa ni pamoja na kufundisha. Idara za mambo ya nje za vyuo vikuu vyetu hazina wabobezi wa kiwango cha Balozi Mahiga. Akirejea kuwapa uzoefu vijana, itakuwa jambo lenye heri. Ikumbukwe kuwa hadi sasa anatumia muda wake mwingi kutoa mihadhara kwenye vyuo vikuu mbalimbali duniani kuhusu utawala bora, utatuzi wa migogoro, ulinzi na usalama na uhusiano wa kimataifa.
Hitimisho
Tangu Balozi Mahiga atangaze kushawishiwa kuwania urais, mmoja wa watu muhimu kwenye moja ya kambi kuu za urais ndani ya CCM alinieleza kwa uwazi kuwa mzee huyu tayari amewaogofya wenzake. Rekodi yake kimataifa katika kazi za kidiplomasia na hata ile ya kuwahi kuongoza kitengo cha Usalama wa Taifa (akiwa mwanzilishi) wa nchi yetu, ukijumlisha na asili yake ya kuwa mtu asiye na makuu lakini thabiti, ambaye hajawahi kuwa na tuhuma nzito za rushwa, vinamfanya awe mtu wa pekee ambaye ni kitisho halisi kwa watu waliokuwa wanahitaji kutengenezewa “chui wa ukweli”.
Kama kambi kuu za wagombea ndani ya CCM zilidhani kazi imeshakwisha, ndiyo kwanza kumekucha na kama zilidhani kuwa pataendelea kutengenezwa “chui wa karatasi” basi zitambue kuwa kazi itakuwa ngumu zaidi. Namtakia kila la heri mzee huyu, Balozi mstaafu Mahiga kwenye safari ambayo anaitumaini.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: