
Dk Augustine Mahiga. Aliendelea na masomo ya sekondari hapahapa nchini na
mwaka 1968, alijiunga katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es
Salaam na kuhitimu Shahada ya Sanaa akibobea kwenye elimu mwaka 1971.
Historia yake
Dk Augustine Mahiga alizaliwa Agosti 28, 1945 huko
Tosamanganga, Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa (atatimiza miaka 70
ifikapo Agosti mwaka huu). Amesoma elimu ya msingi katika shule za
Serikali enzi ya mkoloni na alihitimu darasa la VIII muda mfupi baada ya
uhuru. Safari ya elimu ya Dk Mahiga ilikuwa ya umaskini uliopitiliza,
alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa kutokuwa na fedha za
kulipia mashuka na mablanketi hadi aliposaidiwa na msamaria mwema kutoka
Shirika la Kennedy wakati huo.
Aliendelea na masomo ya sekondari hapahapa nchini
na mwaka 1968, alijiunga katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Dar es
Salaam na kuhitimu Shahada ya Sanaa akibobea kwenye elimu mwaka 1971.
Mwaka huohuo, Dk Mahiga alipata ufadhili na
kuendelea na masomo ya juu nchini Canada katika Chuo Kikuu cha Toronto
ambako alihitimu Shahada ya Uzamili. Aliendelea na masomo ya Shahada ya
Uzamivu (PhD) katika chuo hichohicho akijikita katika Uhusiano wa
Kimataifa na kuhitimu mwaka 1975.
Mwaka huohuo 1975 (akiwa na miaka 30), Dk Mahiga
alirejea nchini akiwa daktari wa falsafa kitaaluma na alipangiwa kazi ya
kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mhadhiri katika Idara ya
Kimataifa na Ushirikiano wa Kikanda. Alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977
alipohamishiwa katika Ofisi ya Rais kuwa Mkurugenzi wa Utafiti na
Mafunzo na alidumu hapo akifanya kazi pamoja na Mwalimu Julius Nyerere
hadi mwaka 1980.
Kati ya mwaka 1980 hadi 1983, Dk Mahiga alikuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Nafasi hii aliitumikia kwa
weledi mkubwa katika historia ya watu waliowahi kuitumikia, aliweza
kuifahamu nchi vizuri na mifumo yake kwa mtizamo wa ndani na nje.
Mwaka 1989 hadi 1992, aliteuliwa kuwa mwakilishi
wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa akifanyia kazi Geneva –
Uswisi na mwaka 1992 hadi 1994, Balozi Mahiga aliteuliwa kuwa Kiongozi
(Mwakilishi) wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi duniani (UNHCR) mjini
Monrovia, Liberia na huu ndiyo wakati aliponusurika kuuawa na Majeshi ya
Rais Charles Taylor, kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kuna wakati
akiwa katikati ya operesheni ya wakimbizi hapo Monrovia, Serikali ya
Tanzania ilimteua kuwa Balozi na kumuongezea jukumu jingine zito.
Mwaka 1994–1998, Balozi Mahiga alihudumu akiwa
Mratibu na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni ya Dharura ya Ukanda wa
Maziwa Makuu akifanyia kazi hiyo kutokea Geneva–Uswisi na kati ya mwaka
1998 – 2002 aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu (Mwakilishi) wa Shirika la
Wakimbizi Duniani (UNHCR) huko mjini Delhi India kabla ya kuteuliwa tena
kuwa mwakilishi wa shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na Jamhuri
ya San Marino kati ya mwaka 2002 – 2003.
Balozi Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa
Tanzania katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010 na alishiriki
kikamilifu katika mipango ya kimataifa pamoja na kusimamia mazungumzo ya
kuanzishwa kwa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani (mwaka 2005). Pia kushiriki
kwenye masuala ya maingiliano ya serikali mbalimbali na makundi
yanayofanya kazi zisizo rasmi, maendeleo, amani, usalama na ujenzi wa
ushirikiano wa uhakika kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Balozi Mahiga alirejesha heshima ya Tanzania hadi
kuwa mojawapo ya nchi zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
na nchi yetu ilipopata heshima hiyo, yeye aliteuliwa kuwa mkuu wa ujumbe
wa Tanzania katika Baraza hilo, hii ilikuwa ni mwaka 2005.
Dk Mahiga ameoa na ana watoto watatu.
Mbio za ubunge
Wanasiasa wengi ambao baadaye huongoza nchi huanzia katika
uwakilishi wa ngazi za chini kama ubunge huku wakipanda juu. Balozi
Mahiga hajapitia njia hii, hakuwahi kuwa mbunge wala mwanasiasa moja kwa
moja, maisha yake yote amekuwa kiongozi wa kimataifa lakini akiifahamu
na kuiwakilisha vizuri Tanzania.
Mbio za urais
Dk Mahiga alianza kuhusishwa na mbio za urais muda
mrefu tu, wala haikuanza leo. Yeye mwenyewe aliamua kuvunja ukimya na
kuzungumzia jambo hilo Aprili akiwa mjini Iringa. Alilieleza gazeti moja
kuwa “…anafuatwa na makundi ya watu wanaomshawishi achukue fomu kuwania
urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM, lakini hajatoa jibu”.
Kauli hii ya Dk Mahiga inahusishwa na ile kauli ya
Rais Kikwete katika maadhimisho ya CCM, Songea – Ruvuma kuwa “…watu
wanaofaa kuwa marais, bado hawajajitokeza na kwamba wapo wengi tu”.
Katika kuonyesha kuwa huenda amedhamiria kuingia
katika kinyang’anyiro, alikwenda mbele zaidi na kueleza kuwa ikiwa
ataamua kugombea, akapitishwa na CCM na kushinda urais, masuala
atakayoyapatia kipaumbele ni pamoja na “uimarishaji wa demokrasia,
kuongeza uwajibikaji, kuimarisha maadili, kuboresha mwelekeo wa uchumi,
kilimo, kuimarisha reli na kupambana na rushwa”.
Nguvu yake
Dk Mahiga ni mtu wa kujisimamia na mara nyingi
hafungwi na mitizamo au matakwa ya kikundi chake ikiwa mitizamo na
matakwa hayo havina manufaa. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipotoa
Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Dk Mahiga hakujali misimamo na matakwa ya
chama chake katika kukosoa waraka ule. Wakati CCM ilikuwa inapinga kwa
nguvu suala la Serikali tatu, yeye alieleza kuwa muundo huo umekuja kwa
wakati muafaka. Alisisitiza kuwa Rasimu ile ya Kwanza imebeba majibu na
kero zote za Muungano. Kiongozi huyu ana msimamo wa kipekee.
Katika kupongeza na kuunga mkono msimamo na
mtizamo wa Dk Mahiga kuhusu Rasimu ya Kwanza ya Katiba, mwanahabari na
mchambuzi maarufu wa masuala ya kijamii na kisiasa, Maggid Mjengwa
aliandika kwenye mtandao wake wa Facebook kuwa “…na kwa kusoma alama za
nyakati. Ukiniuliza leo swali hilo jibu langu liko wazi kabisa, kuwa
tuwe na Serikali Tatu; ya Muungano, Zanzibar na Tanzania Bara
(Tanganyika) na hii si heshima tu tutakayoipata kimataifa, bali
itachangia kwa watu wa pande mbili hizi za Muungano kuheshimiana na
kushirikiana zaidi”.
Dk Mahija ni kati ya wasomi wachache waliopata
kufanya kazi na kuteuliwa kushikilia madaraka na mamlaka makubwa ya nchi
na marais wote wa Tanzania, kuanzia Mwalimu Nyerere, Mwinyi, Mkapa na
sasa Kikwete. Mzee huyu ana uzoefu usio na mfano.
Tatu ni uwezo na usomi wake. Dk Mahiga ni msomi wa
haja aliyebobea na aliyetoka mbali. Watu kadhaa waliofanya naye kazi UN
wanasema kuwa akianza kuongea katika viunga vya UN lazima kila mtu
atamsikiliza, ana ushawishi wa kipekee linapokuja suala la kusimamia
masuala ya msingi na hii ni sifa muhimu kwa kiongozi wa nchi.
Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa wa Balozi Mahiga ni kutofahamika
kwa wananchi wa kawaida. Nilipokuwa nafanya utafiti juu ya balozi huyu
nilishangazwa nilipomhoji mwalimu mmoja wa kiwango cha juu katika Chuo
cha Diplomasia (Kurasini) na hakuwa anamfahamu Balozi Mahiga, hata
nilivyojaribu kumfafanulia kumhusu bado hakumuelewa. Kwa mtu yeyote
ambaye anahitaji kuongoza dola, kufahamika kwa watu wa kati na chini ni
jambo la lazima.
Udhaifu wake mwingine ni uungwaji mkono duni ndani ya chama.
Ndani ya CCM tayari kila mtu ana mgombea wake. Watu wanaopendekezwa
dakika hizi za mwisho wana nafasi ndogo ya kupata uungwaji mkono na
makundi yaliyogawanyika ndani ya chama hicho na karata waliyonayo ni
“ikiwa tu watapigiwa chapuo na viongozi wakuu wa CCM.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama kuna jambo linamtofautisha Dk Mahiga na
wagombea wote wa CCM mwaka huu ni uzoefu wa kimataifa, hakuna mwana CCM
wa kumfananisha naye kwa sasa. Huyu ni mwanadiplomasia aliyebobea labda
akishindana na watu kama Dk Salim Ahmed Salim (ambaye amekwishatangaza
kuwa hatahusika na vinyang’anyiro vya kusaka uongozi wa nchi tena).
Ikiwa CCM itahitaji mtu ambaye anakubalika
kimataifa na amekwishafanya kazi kubwa za kimataifa zinazoheshimiwa,
basi Balozi Mahiga ndiye atakuwa chaguo la kwanza. Hata Februari mwaka
huu, gazeti moja la kila wiki nchini, lilimtaja kama “mwanadiplomasia
anayeheshimika kuliko wote nchini Tanzania”.
Jambo jingine linampa nafasi ya kupitishwa ni
kutokuwa na kundi la kukigawa chama hicho na hasa kutokuwa karibu hata
na makundi mengine. Jambo hili si la kupuuza hasa ikiwa CCM itahitaji
kuwa na Rais anayeheshimika na atakayeungwa mkono na “mapande makubwa ya
urais” yanayosigana ndani ya chama hicho.
Lisemwalo lipo, kama halipo basi linakuja. Kauli
ya Rais Kikwete “kubeza” wagombea waliojitangaza kwa kusisitiza kuwa
hajaona Rais kati yao si ya kudharau. Baba yangu aliwahi kunisisitiza
kuwa ukisikia mtu mzima anasema neno lolote hata kama ni la kipuuzi au
kiutani usilidharau.
Watu ambao wamepata bahati ya kuongoza nchi kama
Rais Kikwete wana matatizo mengi vichwani, mizigo ya matatizo ya nchi
inakuwa imewaelemea na hutamka baadhi ya mambo ili kujipunguzia mambo
yanayowasumbua. Wachambuzi wa siasa watakubaliana nami kuwa huenda Rais
Kikwete amechoshwa na mivutano na pilikapilika zisizo salama za wagombea
nguli wa chama chake na suluhisho linaweza kumpata mtu ambaye
hategemewi wala kujulikana sana, Balozi Mahiga anaweza kupenya kwenye
mlango huu.
Nini kinaweza kumwangusha?
Baadhi ya watu muhimu na wakongwe niliobadilishana
nao mawazo ndani ya CCM wanatoa maoni kuwa hapajapata kutokea mtu
mwenye umri mkubwa akakabidhiwa uongozi kupitia CCM. Umri wa Balozi
Mahiga wa miaka 70, unachukuliwa kama mkubwa utakaovunja rekodi ndani ya
chama hicho na hata nchi.
Wakongwe hawa wana hofu na mamilioni ya wapigakura
vijana watakaoongezeka ambao chaguo lao kuu linaweza kuwa wagombea
wenye umri wa kadri. Mfano thabiti ni kuwa Mwalimu Nyerere alianza
kuongoza Tanzania akiwa na miaka 40, Mwinyi alikuwa na miaka 60, Mkapa
57 na Kikwete alianza akiwa na 55. Hofu hii ya wakongwe wa chama hicho
si ya kuidharau, ichukuliwe kwa uzito mkubwa kama moja ya vinavyoweza
kuwa vitanzi vya Balozi Mahiga.
Jambo la pili linalowapatia shida wana CCM
wakongwe ni Kutojulikana kwa Dk Mahiga. Nilipohoji kuwa hata Mkapa
alipoteuliwa mwaka 1995 hakuwa anajulikana walinijulisha kuwa Mkapa
alijulikana ghafla kwa sababu watu walikuwa wanamsikia bila kumtilia
maanani wakati akiongoza wizara mbalimbali, pili alijulikana haraka kwa
sababu mtu wa kumnadi alikuwapo, Mwalimu Nyerere. Vigogo hawa wanasema
kuwa ikiwa Dk Mahiga atapitishwa, wanachama wengi wasiomfahamu vizuri
watakatishwa tamaa na umaarufu wa wagombea wengine hususan kutoka Ukawa.
Mbaya zaidi, inasisitizwa kuwa katika kampeni za mwaka huu, mgombea wa
CCM hatakuwa na mtu imara wa kumnadi, zaidi ya umaarufu wake na rekodi.
Jambo jingine linaloweza kumhukumu Balozi Mahiga, ni msimamo
wake kuunga mkono Serikali tatu. Nilikuwa Dodoma kwenye Bunge Maalumu la
Katiba (BMK) na nilijionea mwenyewe, “kuunga mkono serikali tatu kwa
mwana CCM kulikuwa ni dhambi kuliko kuua”. Dk Mahiga amewahi kuweka
msimamo wake akiunga mkono muundo huo, kama hatakuja tena hadharani
kugeuka msimamo wake wa awali, atajengewa hoja nzito kuwa yeye si
muumini wa Muungano, kwa sababu ndani ya CCM, mtu anayeunga mkono
Muungano lakini kwa serikali tofauti na mbili, anachukuliwa kama “mtu
mwenye njama za kuvunja muungano”. Hili ni jambo zito kwa Dk Mahiga.
Asipopitishwa (Mpango B)
Balozi Mahiga atakuwa na mipango kama minne ya kufuata ikiwa hatapitishwa kugombea kwa CCM.
Moja itakuwa ni kustaafu utumishi umma kwa
majukumu ya moja kwa moja (majukumu ya kila siku) kwa sababu umri wake
huenda kwa sasa unahitaji mapumziko na kujenga afya thabiti ya uzeeni
kuliko kuendelea kukimbizana. Katika mapumziko haya ndipo anaweza kuwa
anaishauri Serikali juu ya mustakabali wa mambo ya ndani na nje ya nchi.
Pili, anaweza kuendelea kuhudumu kimataifa katika
misheni za muda mfupi za utatuzi wa migogoro barani Afrika na
kwingineko. Yeye ni mzoefu kwenye eneo hilo na anaweza kuendelea kutoa
msaada.
Tatu, ni kurudi kusaidia ulezi wa wanafunzi vyuoni
ikiwa ni pamoja na kufundisha. Idara za mambo ya nje za vyuo vikuu
vyetu hazina wabobezi wa kiwango cha Balozi Mahiga. Akirejea kuwapa
uzoefu vijana, itakuwa jambo lenye heri. Ikumbukwe kuwa hadi sasa
anatumia muda wake mwingi kutoa mihadhara kwenye vyuo vikuu mbalimbali
duniani kuhusu utawala bora, utatuzi wa migogoro, ulinzi na usalama na
uhusiano wa kimataifa.
Hitimisho
Tangu Balozi Mahiga atangaze kushawishiwa kuwania
urais, mmoja wa watu muhimu kwenye moja ya kambi kuu za urais ndani ya
CCM alinieleza kwa uwazi kuwa mzee huyu tayari amewaogofya wenzake.
Rekodi yake kimataifa katika kazi za kidiplomasia na hata ile ya kuwahi
kuongoza kitengo cha Usalama wa Taifa (akiwa mwanzilishi) wa nchi yetu,
ukijumlisha na asili yake ya kuwa mtu asiye na makuu lakini thabiti,
ambaye hajawahi kuwa na tuhuma nzito za rushwa, vinamfanya awe mtu wa
pekee ambaye ni kitisho halisi kwa watu waliokuwa wanahitaji
kutengenezewa “chui wa ukweli”.
Kama kambi kuu za wagombea ndani ya CCM zilidhani
kazi imeshakwisha, ndiyo kwanza kumekucha na kama zilidhani kuwa
pataendelea kutengenezwa “chui wa karatasi” basi zitambue kuwa kazi
itakuwa ngumu zaidi. Namtakia kila la heri mzee huyu, Balozi mstaafu
Mahiga kwenye safari ambayo anaitumaini.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment