
Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC),
kimesema bajeti ya 2015/ 16 inayotarajiwa kusomwa bungeni katika mkutano
ujao, itawaumiza wananchi wa hali ya chini.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hassan
Doyo, wakati akihutubia wakazi wa kijiji cha Songe Mnadani, Wilaya ya
Kilindi, Tanga. Doyo alisema moja ya vitu vinavyoonyesha kwamba bajeti hiyo
itamuumiza mwananchi wa hali ya chini ni bei ya mafuta ya ndege ambayo
ushuru wake utashushwa.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona huduma zinazotumiwa na watu
wa hali ya juu zinashushwa huku zile zinazotumiwa na watu wa hali ya
chini zikiendelea kupanda. “Asilimia kubwa ya watu wanaotumia huduma ya usafiri ya ndege ni
wenye kipato kikubwa siyo masikini, wengi wanaotumia usafiri wa basi ni
walala hoi wasio na kipato kizuri, lakini eti leo hii mafuta ya ndege
yanaondolewa ushuru,” alidai Doyo.
Pia alisema kuwa mafuta ya taa yatapanda kwa asilimia 75 na kwamba
kama bajeti itapitishwa kama ilivyopangwa, gharama ya maisha kwa watu wa
chini itapanda. Aliongeza kuwa hali hiyo itapandisha matumizi katika serikali ijayo itakayoundwa mwishoni mwa mwaka huu.
Aliwaomba Wabunge kuhudhuria kwa wingi katika Bunge hilo ili
kuibana serikali isipitishe bajeti hiyo kama ilivyopangwa kwa kuwa
kufanya hivyo ni kuwakandamiza wananchi wanyonge. “Najua Wabunge hivi sasa wana mambo mengi, wamejichimbia kwenye
majimbo yao kwa ajili ya kujiandaa katika uchaguzi mkuu, ninaomba katika
Bunge hilo la bajeti linalotarajia kuanza Mei 12, mwaka huu waache
shughuli zao waende kuwapigania wananchi kwa sababu bila kufanya hivyo
maisha yatakuwa magumu sana,” alisema Doyo.
Mwenyekiti wa ADC, Said Miraaj, alisema gharama za maisha ya
Watanzania zimeendelea kupanda huku watu wenye kipato cha chini
wakiendelea kunyonywa na walionacho wakizidi kuongezewa. Aliwataka Watanzania kutofanya makosa katika uchaguzi mkuu mwaka
huu kwa kuhakikisha wanachagua viongozi wenye nia ya kuwakomboa.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment