Pages

Thursday, April 23, 2015

WILLIAM NGELEJA: MBUNGE WA SENGEREMA

William Ngeleja, Mbunge wa Sengerema alisoma katika Shule ya Msingi Bitoto mwaka 1976 – 1982 kabla ya kuelekea mkoani Dodoma kwa masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Mpwapwa kati ya mwaka 1983 –1986. Baada ya kufaulu vizuri aliendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Ihungo mkoani Kagera kati ya mwaka 1987 – 1989.
Historia yake
William Mganga Ngeleja alizaliwa Oktoba 5, 1967 mkoani Mwanza hivyo atafikisha miaka 48 mwezi Oktoba mwaka huu.
Ngeleja alisoma katika Shule ya Msingi Bitoto mwaka 1976 – 1982 kabla ya kuelekea mkoani Dodoma kwa masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Mpwapwa kati ya mwaka 1983 –1986. Baada ya kufaulu vizuri aliendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Ihungo mkoani Kagera kati ya mwaka 1987 – 1989. Ngeleja alifaulu vizuri masomo yake na akajiunga moja kwa moja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani akichukua kozi ya sheria mwaka 1991. Alihitimu na kutunukiwa shahada ya kwanza ya sheria (LLB) mwaka 1994 na kuajiriwa serikalini kama Mwanasheria wa Serikali mwaka 1994–1996. Ngeleja aliamua kujiendeleza zaidi, akarejea UDSM mwaka 1996 kusomea shahada ya uzamili ya sheria (LLM) na kuhitimu mwaka 1999.
Kati ya mwaka 1995 hadi 2000 Ngeleja pia alifanya kazi na kampuni maarufu ya uwakili duniani ya Price WaterHouse Coopers, ambayo ina matawi mengi ulimwenguni ikiwamo Tanzania.
Mwaka 2000 aliacha kazi Price WaterHouse Coopers na kujiunga na kampuni ya Vodacom ambako alifanya kazi kama mwanasheria wa kampuni, kwa miaka mitano, hadi 2005. Katika kipindi chote hiki Ngeleja aliendelea na kazi huku akikisaidia chama chake, CCM, katika masuala mbalimbali na wakati huohuo akifikiria kuingia katika siasa za ushindani.

Mbio za ubunge
Safari ya kuusaka ubunge aliianza mwaka 2005 alipojitosa kuomba ridhaa ya ubunge katika Jimbo la Sengerema; akapita mchujo wa kura za maoni na kuwa mgombea wa CCM. Kwenye uchaguzi alikumbana na Essau Balalukuliliza Pelece wa UDP, Stella Cosmas Chetto wa CUF na Joshua Zebrone Subi wa Chadema akawashinda kwa kupata asilimia 69.3 ya kura zote. Baada ya kuwa mbunge alitumikia nafasi hiyo, kwa mwaka mmoja, kabla ya kuongezewa wadhifa wa unaibu waziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kwenye wizara ya Nishati na Madini kutokea Januari 2007 hadi Agosti 2008.
Mwaka 2008 kulipofanyika mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Ngoyayi Lowassa kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Rais Kikwete aliunda Baraza la Mawaziri jipya na kukuza “ngekewa” ya Ngeleja ambaye alipewa uwaziri kamili wa Nishati na Madini kukamilisha miaka miwili iliyokuwa imebakia kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwkaa 2010.
Mwaka 2010 Ngeleja alijitosa tena kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kutetea nafasi yake; alishinda kura za maoni na kwenye uchaguzi wenyewe akawa hana mpinzani, yaani wagombea wa upinzani waliingia “mitini” na kumpa “zawadi ya ushindi”.
Baada ya kupita bila kupingwa aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini, nafasi aliyoitumikia hadi Juni 2012 mwaka ambao Rais Kikwete alifanya mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaziri na kumtupa nje Ngeleja. Nafasi yake ilichukuliwa na Profesa Sospeter Muhongo.
Pamoja na kuwa nje ya uwaziri, safari yake kisiasa iliendelea kukumbwa na mawimbi mengi. Mwanzoni mwa mwaka huu, alilazimika kuachia ngazi katika nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kutokana na kuwa miongoni mwa viongozi waliopokea mgawo wa fedha zilizochukuliwa kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Alipoitwa kujieleza kwenye Tume ya Maadili, Ngeleja alikiri kuwekewa shilingi 40.4milioni na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering & Marketing, James Rugemalira lakini mwenyewe alisisitiza kuwa fedha hizo hazikuwekwa kwa nia mbaya. Na kibaya zaidi yeye mwenyewe hakutoa taarifa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mbio za urais
Ngeleja ni mmoja wa watu waliotajwa sana kama watu wanaomuunga mkono Lowassa katika safari ya kuisaka Ikulu tangu alipokuwa Waziri Mkuu chini ya Rais Kikwete na hata baada ya kujiuzulu nafasi hiyo mwaka 2008.
Na hata Ngeleja alipoteuliwa tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini, mara baada ya kuteuliwa kwa mara ya pili Januari 2011, ilisemekana kuwa anamuunga mkono waziri mkuu huyo aliyejiuzulu. Lakini katikati ya mwaka 2013, inasemekana wanamtandao wa urais katika kundi la Lowassa wanaotokea Kanda ya Ziwa, waliona vema kumuibua mgombea anayeweza kuungwa mkono kutoka kanda yao na ndipo akainuliwa Ngeleja.
Katika harakati za chini kwa chini akawa miongoni mwa makada sita walionaswa na chama wakifanya kampeni za siri na wakazuiwa kwa miezi 12 kuanzia Februari mwaka jana. Kamati ya Maadili inaendelea kuwachunguza.
Hata harakati zake za kuwapigania wachimbaji wadogowadogo wapate maeneo zaidi kwa ajili ya uchimbaji, kuwaanzishia mfuko maalum wa kuwasaidia, kupiga marufuku usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje ya nchi, na hatua kama hizo, zilikuwa zinahusishwa na mbio hizo hasa kwa kuzingatia kuwa maeneo yenye madini yana wapigakura wengi sana. Hata hivyo, jambo hilo halijathibitishwa.
Watu walio karibu naye, miongoni mwao wakiwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, wanasema kwamba yeye huwa anajinasibu kuwa anaweza kuwa chaguo mbadala makada maarufu watakapokatwa majina yao.

Nguvu zake
Ngeleja amewahi kuwa karibu sana na Lowassa, na hadi leo. Kwa hiyo, anaujua vizuri mtandao wa ushindi ndani ya CCM hasa kwa sababu alishiriki pia shughuli kama hiyo wakati wa kumpigania Kikwete mwaka 2005. Jambo hili linampa nguvu kubwa.
Nguvu nyingine ya Ngeleja inatokana na umri wake, kwani anaonekana bado kijana sana. Ikiwa CCM itahitaji kupitisha mgombea mwenye umri wa “usasa” na ambaye ana kaliba inayoweza kuwavutia vijana na watu wengine, Ngeleja atakuwa miongoni mwa watu wenye sifa hiyo.
Tukija katika uzoefu, eneo hili pia linampa Ngeleja nguvu kubwa. Tangu mwaka 1994 Ngeleja ameweza kutumika serikalini na katika mashirika binafsi na ya kimataifa kama mwanasheria. Uzoefu huo una maana kuwa anaifahamu vizuri nchi na mazingira ya kazi katika sekta ya umma na sekta binafsi. Hakika kigezo hiki kinampa nguvu ya kipekee tofauti na wagombea wengine ambao labda wamewahi kufanya kazi serikalini tu.
Nguvu nyingine ya Ngeleja inapatikana kwenye taaluma yake. Sheria ni taaluma ya “kipekee” na ina tofauti kubwa sana na masomo ya sanaa. Mara nyingi viongozi wanasheria wanatarajiwa kujiamini na kutenda masuala ambayo yanaweza kutohojiwa kirahisi. Ikiwa itachukuliwa kwa mtazamo huo na kwamba CCM inahitaji msomi mzuri mwenye taaluma ya kipekee na inayoweza kumfanya mtu afanye kazi katika mazingira yoyote kwenye sekta nyingine, basi Ngeleja atakuwa miongoni mwa wanaofuzu.

Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa wa Ngeleja ni kuwa karibu na wanasiasa wanaotajwa vibaya na wenye taswira hasi katika jamii. Kama nilivyowahi kueleza katika maandiko yangu mengine, CCM safari hii, itahitaji kuwa na mgombea ambaye ana rekodi sahihi na mwenye nguvu ya kutosha kukisaidia chama chake kishinde uchaguzi kirahisi na siyo mtu ambaye atakuwa mzigo au kusafishwa kwa “dodoki”. Kwa dhana hii Ngeleja anaweza kuonekana kuwa mmoja wa “mizigo” inayopigwa vita.
Udhaifu mwingine wa Ngeleja upo kwenye utendaji. Ngeleja amekuwa Waziri wa Nishati na Madini kwa takribani miaka sita, lakini ameondoka katika wadhifa huo nchi ikiwa na changamoto kubwa sana za kiusimamizi na kimiundombinu. Jambo moja linaweza kuhitimishwa katika hali kama hiyo, kwamba siyo mtendaji mzuri. Pamoja na baadhi ya mazuri aliyofanya Ngeleja, lakini aliiacha wizara ikiwa na matatizo mengi kama mtangulizi wake.
Na mfano mwingine ni namna alivyokuwa akishughulikia ukosefu wa nishati ya umeme. Mwanzoni mwa Desemba 2010 Ngeleja aliwatangazia Watanzania kuwa “mgawo wa umeme sasa basi”. Lakini wiki tatu baadaye, hata kabla mwezi huo haujaisha, Tanesco ikatangaza mgawo wa umeme mkali kuliko uliowahi kutokea nyuma yake. Udhaifu huu kiusimamizi na kimamlaka hautapita hivi hivi bila kujadiliwa.
Ndani ya Bunge kwenyewe, alilalamikiwa sana kutokana na utendaji wake mbovu katika sekta ya Nishati na Madini. Mwaka 2011 matatizo yale yale ya mgawo wa umeme yaliendelea kujitokeza hadi aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alimshutumu Ngeleja kuwa amekuwa mtu wa kukimbia, kujificha na kutosema ukweli kuhusu tatizo la umeme nchini.
Ngeleja alitupiwa shutuma kwa sababu kauli ya Serikali aliyoitoa bungeni juu ya hali ya umeme nchini ikiwemo kukodishwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 260 ifikapo Juni na Julai mwaka huo wa 2011 haikuwa imetekelezwa huku Waziri akiwa kimya. CCM katika baadhi ya matamko yake kwenye mikutano ya hadhara ilisisitiza pia kuwa “kitendo cha Waziri Ngeleja kukimbia na kujificha, kinaonyesha kuna ombwe la uongozi ndani ya Wizara ya Nishati na Madini”. Chama kiliungana na Kamati ya Makamba na kumsisitiza ambane Ngeleja ili aeleze utekelezaji wa mipango yote aliyoiainisha kwenye ahadi za serikali vinginevyo aachie ngazi.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama kuna jambo litaweza kumbeba Ngeleja basi ni elimu na uzoefu wake. Kama nilivyoeleza hapo awali Ngeleja ana elimu nzuri na ana uzoefu mzuri wa kufanya kazi na sekta binafsi na ya umma na anaifahamu nchi hii vizuri. Kama CCM ikiamua kumpitisha basi hii itakuwa sababu mojawapo.
Lakini pia, Ngeleja ni mtu wa kuthubutu. Pamoja na mapungufu yake yote, anaweza kusimamia jambo fulani na likaonekana japokuwa anaweza kuonekana kama amelifanya kwa kiwango cha chini utakapomlinganisha na watu wengine wenye uwezo kumshinda. Nilitoa mfano wa kusimamia masuala ya vitalu vya wachimbaji wadogowadogo na kuanzisha mfuko wao. Haya ni mambo ambayo wamekuwa wakiyalalamikia muda mrefu lakini hayakufanikishwa hadi alipoingia Ngeleja japo hadi sasa hayajawa na tija. Hata hivyo, walau unaweza kusema yeye ni mtu wa kuthubutu.
Na pia, ikiwa CCM itataka kumpitisha mgombea ili kuyafurahisha makundi yanayosigana, yeye anaweza kuwa chaguo. Kwamba yale makundi makubwa na wakuu wao, itakapoonekana hawastahili basi atafutwe mtu ambaye anaweza kuwa anaungwa mkono na kundi lolote na ambaye akiteuliwa makundi yote yanaweza kumkubali kwa sababu si mkuu wa kundi fulani, atakuwa Ngeleja, japokuwa ikifikia hapa chama kitakuwa kinajimaliza chenyewe.

Nini kinaweza kumwangusha?
Ngeleja ana taswira ya kukosa uadilifu na hivyo ndivyo ilivyo. Alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini, wizara yake iliendelea kutuhumiwa kufanya “madudu” mengi sana.
Alishindwa kuwasimamia watendaji wa Tanesco na mashirika mengine yaliyo chini ya wizara yake dhidi ya ubadhirifu mkubwa ambao ulikuwa unafanywa huko. Kuna wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ilionyesha madudu mengi katika wizara yake na kila yalipokuwa yanatajwa unaona mengine yangeweza kuondoshwa kwa juhudi za waziri mwenyewe, lakini hakuchukua hatua.
Wakati wa mgawo mkali wa umeme mwaka 2011, mmoja wa wananchi alimkejeli Ngeleja kwenye mitandao ya kijamii juu ya mgawo wa umeme akisema “….Ni kweli tangu alipoingia madarakani msimu wa kwanza wa 2005-2010 na sasa msimu huu wa 2010-2015 kauli yake imekuwa ni hiyo hiyo. Na ukweli ni kwamba nampongeza sana ‘Mheshimiwa’ huyu kwani ametekeleza ahadi yake ya kuufanya mgawo wa umeme kuwa ni historia, na imekuwa historia ambayo inajulikana hata na mtoto mchanga”.
Mwananchi huyo aliendelea kusisitiza kuwa “….kwa hiyo msimshambulie anatekeleza kauli yake na ahadi yake ya kufanya mgawo wa umeme kuwa ni historia katika nchi hii. Mgawo wa umeme umeongezeka siku hadi siku na umebaki kuwa historia, mmuelewe hivyo na kama hivyo tena ameahidi kupigana kufa na kupona kuufanya uendelee kuwa ni historia. Kipi kigumu hapo wakuu?”
Utendaji wa aina hii alioufanya Ngeleja kwenye sekta muhimu kama nishati na madini utamhukumu kwenye kinyang’anyiro cha urais bila ajizi.
Sakata la Escrow linaweza kumsababishia anguko. Sote tunajua kuwa sakata hili lilimhusisha yeye kuchukua kiasi cha Sh40.4 milioni kutoka kwa James Rugemalira, mfanyabiashara ambaye alikuwa mbia katika kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Na inatafsiriwa ni kama vile Ngeleja alikuwa analipwa fadhila kwa kusimamia jambo fulani.
Ikumbukwe, Ngeleja aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini katika vipindi ambavyo Tanesco na IPTL vilikuwa kwenye mvutano mkubwa kuhusu viwango vya tozo. Huyo ndiye baadaye naye anaonekana amepokea fedha zilizotokana na mgogoro wa sekta ambayo alikuwa anaiongoza. Mbaya zaidi ni kwamba anapopokea fedha hizo hafuati mkondo wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kutoa taarifa. Sakata la Escrow linaweza kumuumiza kabisa Ngeleja kisiasa na kumuondoa miongoni mwa watarajiwa ndani ya CCM.
Lakini pia ikumbukwe kuwa Ngeleja ni miongoni mwa makada sita ambao walinaswa na chama wakifanya kampeni za siri na wakazuiwa kwa miezi 12 kuanzia Februari mwaka jana. Kamati ya Maadili inaendelea kuwachunguza hatujui kamati hiyo itakuja na uamuzi gani, hapo napo ni mtihani kwa Ngeleja.

Asipopitishwa (Mpango B)
Ikiwa Ngeleja hatapitishwa kugombea urais ndani ya CCM nadhani atarudi Sengerema kugombea ubunge na anaweza kushinda. Tatizo ambalo naliona katika harakati za kurudi kwenye ubunge ni kwamba chama chake kinaweza kumtosa kwa staili ile ile na sababu zile zile zitakazokuwa zimemwangusha kwenye urais. Kwamba CCM itahofu kuwa na mgombea mwenye tuhuma za kuhusishwa na Escrow na labda chama hicho kitataka kujitutumua kwa wananchi kuwa kinapambana na ufisadi kwa vitendo.
Ngeleja ni mwanasheria mwenye uzoefu mkubwa na amefanya kazi serikalini na nje ya serikali, kwa hiyo, anaweza kuwa na mchango mkubwa kwa jamii ikiwa ataendeleza taaluma yake hasa itakapotokea kuwa CCM imemtosa kwenye urais na labda hata kwenye ubunge. Namwona kama mwanasheria mwenye mafanikio makubwa baadaye ikiwa itampasa kupita kwenye njia hii.

Hitimisho
Naona kama Ngeleja atakuwa na wakati mgumu kupita kwenye mchujo wa wagombea urais ndani ya CCM na ni kama vile jina lake linaweza kukatwa mapema ili kuwapisha wana CCM wengine wenye sifa zaidi waweze kuchukua jukumu hilo la kidemokrasia. Lakini pia hatujui chama hicho kitatumia mfumo gani na sifa zipi kumpata mgombea wake. Kwa lolote lile litakalojiri, naye tunamtakia kila la heri kwenye malengo yake.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment