Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Mnyika, amewataka
wanachama wa chama hicho wilayani Tarime kuachana na makundi
yanayosababisha kukigawa Chama.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Sabasaba
mjini Tarime na kuhudhuriwa na umati wa wananchi, Mnyika alisema kuwapo
makundi kunasababisha Chama kugawanyika hivyo kudhoofisha nguvu zake.
Aidha, aliwapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa kufanikisha chama
hicho kunyakua viti vingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa
uliofanyika Desemba 14, mwaka jana katika nafasi za uenyekiti wa mitaa,
vijiji na vitongoji pamoja na wajumbe.
“Pamoja na kuwapongeza huko, lakini nawaomba wananchi mjitokeze kwa
wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura muda
utakapowadia,” alisema Mnyika.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), John Heche, aliwaasa
wana-Tarime wawe na mshikamano wa kushirikiana kuleta maendeleo kwa
kupiga vita maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi huku
akichukua nafasi hiyo kujitangaza kuwania nafasi ya ubunge Jimbo la
Tarime.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment