
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Sakata la upatikanaji wa maji ya bomba katika Wilaya
ya Sengerema mkoani Mwanza, limechukua sura mpya baada ya Meneja wa
Mamlaka ya Maji wilayani humo, kutofautiana na ahadi ya Mbunge wa jimbo
hilo, William Ngeleja, kuwahuduma hiyo itapatikana ifikapo Juni, mwaka
huu.
Hivi karibuni Ngeleja akizungumza katika ya mikutano ya hadhara
jimboni humo, aliwahakikishia wananchi wa mji wa Sengerema kuwa huduma
ya maji itapatikana mapema mwaka huu.
Akizungumza na NIPASHE, Meneja wa Mamlaka ya Maji wilayani
Sengerema, Wawa Nyonyoli, alisema wilaya hiyo imepata mradi mkubwa wa
maji unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika na kugharimu zaidi ya
Sh. bilioni 23 na kwamba utakamilika Juni, 2016.
Alisema hiyo ni kwa mujibu wa mikataba iliyopo ofisini kwake na
kuwataka wananchi kuvuta subira na kutoamini zaidi maneno ya viongozi wa
kisiasa kuliko ya watalaam. "Mradi huo utakamilika Juni, mwakani na
wala siyo mwaka huu...wananchi wanapaswa kuelewa hivyo toka kwa
wasimamizi wa mradi huo wilayani hapa huku maji wakiendelea kupata kwa
mgawo mpaka mradi utakapokamilika," alisema Nyonyoli.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Marietha Kasongi, alisema
hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa yupo nje ya ofisi na atafanya hivyo
baada ya kurejea. Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Bukala mjini Sengerema walisema
tatizo la upatikanaji wa maji limekuwa sugu na kwamba linahatarisha ndoa
zao kutokana na wake zao kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta huduma
hiyo muhimu kwa umbali mrefu wa kilomita 20.
Juma Ramadhani, mkazi wa Sengerema, alisema wananchi wamekuwa
wakiyumbishwa kutokana na kauli mbalimbali za viongozi wa kisiasa katika
upatikanaji wa maji wilayani humo na kuiomba serikali kutambua tatizo
la maji kwa wakazi wa mji huo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment