Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru amesema viongozi
wa serikali wanapaswa kutambua mipaka yao ya kiutawala, na kuliacha
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lijiendeshe lenyewe kama taasisi ya
kibiashara.
Pia amezitaka taasisi nyeti za serikali zinazodaiwa madeni na
Tanesco kulipa madeni hayo mara moja, vinginevyo watakatiwa umeme pasipo
kujali umuhimu wa taasisi hizo. Aliyasema hayo wakati wa ukaguzi wa miradi ya umeme inayoendeshwa
na Tanesco, ikiwamo kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi
kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 150.
Alisema viongozi wengi wa serikali wanasahau majukumu yao ya
kiutendaji, na kufanya majukumu ambayo siyo yao akitolea mfano Tanesco
inavyoingiliwa katika utendaji. Alisema kuna viongozi wengi wa serikali
wanaokuwa na mamlaka ya kiutendaji kwa shirika hilo, jambo
linalokwamisha Tanesco kufikia malengo iliyojiwekea.
Mafuru alisema Tanesco linazidai fedha nyingi taasisi nyingi za
serikali ambazo zinadaiwa kuwa ni nyeti na haziwezi kukatiwa umeme. “
Naagiza tena, kama kuna taasisi ambazo zipo chini ya Msajili wa Hazina
na zinadaiwa na Tanesco ninaomba niletewa majina yake ili nianze nazo,”
alisema Mafuru.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alieleza kuwa
ujenzi wa kituo hicho cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi unatarajiwa
kumalizika Juni mwaka huu. Alisema kitakapokamilika na gesi kutoka Mtwara itakapofika,
kitakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme mwingi utakaowatosheleza wakazi wa
Dar es Salaam. “Kama mnavyoona kituo kinaendelea vizuri, mwezi wa sita kitakuwa
kimekamilika na shida ya umeme haitakuwapo tena katika Jiji la Dar es
Salaam,” alisema Mramba.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment