Social Icons

Pages

Thursday, April 02, 2015

NGELEJA APINGWA MRADI WA MAJI

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Sakata la upatikanaji wa maji ya bomba katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, limechukua sura mpya baada ya Meneja wa Mamlaka ya Maji wilayani humo, kutofautiana na ahadi ya Mbunge wa jimbo hilo, William Ngeleja, kuwahuduma hiyo itapatikana ifikapo Juni, mwaka huu.
Hivi karibuni Ngeleja akizungumza katika ya mikutano ya hadhara jimboni humo, aliwahakikishia wananchi wa mji wa Sengerema kuwa huduma ya maji itapatikana mapema mwaka huu.
Akizungumza na NIPASHE, Meneja wa Mamlaka ya Maji wilayani Sengerema, Wawa Nyonyoli, alisema wilaya hiyo imepata mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika na kugharimu zaidi ya Sh. bilioni 23 na kwamba utakamilika Juni, 2016.
Alisema hiyo ni kwa mujibu wa mikataba iliyopo ofisini kwake na kuwataka wananchi kuvuta subira na kutoamini zaidi maneno ya viongozi wa kisiasa kuliko ya watalaam. "Mradi huo utakamilika Juni, mwakani na wala siyo mwaka huu...wananchi wanapaswa kuelewa hivyo toka kwa wasimamizi wa mradi huo wilayani hapa huku maji wakiendelea kupata kwa mgawo mpaka mradi utakapokamilika," alisema Nyonyoli.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Marietha Kasongi, alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa yupo nje ya ofisi na atafanya hivyo baada ya kurejea. Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Bukala mjini Sengerema walisema tatizo la upatikanaji wa maji limekuwa sugu na kwamba linahatarisha ndoa zao kutokana na wake zao kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta huduma hiyo muhimu kwa umbali mrefu wa kilomita 20.
Juma Ramadhani, mkazi wa Sengerema, alisema wananchi wamekuwa wakiyumbishwa kutokana na kauli mbalimbali za viongozi wa kisiasa katika upatikanaji wa maji wilayani humo na kuiomba serikali kutambua tatizo la maji kwa wakazi wa mji huo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: