Social Icons

Pages

Friday, April 17, 2015

MALAWI YAKUBALI USHIRIKIANO NA TANZANIA KUPITIA SEKTA BINAFSI

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi (kulia), akizungumza na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe, alipomtembelea Dk. Mengi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.Serikali ya Malawi kupitia ubalozi wake nchini, imekubali  kushirikiana na Tanzania katika masuala ya biashara kupitia sekta binafsi baina ya nchi hizo mbili. Hayo yalibainishwa na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe, baada ya kumtembelea na kuwa na mazungumzo ya pamoja na  Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi, katika ofisi za IPP, jana, jijini Dar es Salaam.
Balozi Ndilowe alionyesha mwitikio huo chanya kwamba Serikali ya Malawi haitakuwa na kigugumizi chochote  kuhusu ushirikiano wa sekta binafsi baina ya mataifa hayo, yakiwa ni maombi ya Dk. Mengi, kwa ajili ya kuimarisha na kufungua milango ya kibiashara kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Balozi Ndilowe alimpongeza Dk. Mengi kwa wito huo, akisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuwaleta pamoja wafanyabiashara wa nchi hizo kupitia sekta hizo. “Hilo ndilo eneo zuri la kuja pamoja tunaweza kushirikiana, kuangalia  maeneo tunayoweza kuungana…kupitia ushirikiano wa kiuchumi uliopo kutafungua fursa za biashara baina ya watu wa pande hizi mbili,” alisema Balozi Ndilowe.
 Pia alipongeza kukua kwa sekta binafsi nchini na kuunga mkono serikali ya nchi yake kutambua mchango wa sekta hiyo nchini humo katika kuwawezesha wafanyabiashara  wakiwamo wa chini.
Awali, Dk. Mengi, alisema litakuwa jambo jema kama sekta binafsi kutoka pande zote zitakubali kukaa pamoja na kwamba jambo hilo likiwezekana itakuwa ni enzi mpya katika kuwawezesha wafanyabiashara wa nchi hizo kuingiliana katika kibiashara huku kila upande ukiwa na nafasi ya kuangalia fursa upande mwingine kwa ajili ya kuwekeza.
Kutokana na hilo, Dk. Mengi, alisema ni muhimu kwa sekta binafsi kutoka nchi hizo, kujiamini, hivyo wafanyabishara wake kuwa na ujasiri wa kwenda kuangalia fursa ambazo zinapatikana katika nchi hizo.
Dk. Mengi pia alitoa wito kwa sekta hiyo kwa pande zote  kuwawezesha wafanyabiashara wakiwamo wadogowadogo.
Alitoa wito wa kuwashughulikia wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi akipendekeza kuchukuliwa hatua kali siyo kwa wauaji pekee bali pia kwa wanunuaji wa viungo vya miili ya binadamu kwani wasipofuatiliwa, wataendeleza uovu huo.
Dk. Mengi alitoa wito wa kukomesha vitendo hivyo  ambavyo vimekithiri huku akiipongeza Malawi kwa jinsi ivyodhibiti uovu huo, baada ya kuambiwa na balozi huyo kwamba vitendo hivyo havina nafasi nchini humo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: