Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi (kulia), akizungumza na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe,
alipomtembelea Dk. Mengi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.Serikali ya Malawi kupitia ubalozi wake nchini,
imekubali kushirikiana na Tanzania katika masuala ya biashara kupitia
sekta binafsi baina ya nchi hizo mbili. Hayo yalibainishwa na Balozi wa Malawi nchini, Hawa Ndilowe, baada
ya kumtembelea na kuwa na mazungumzo ya pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi
ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi, katika ofisi za
IPP, jana, jijini Dar es Salaam.
Balozi Ndilowe alionyesha mwitikio huo chanya kwamba Serikali ya
Malawi haitakuwa na kigugumizi chochote kuhusu ushirikiano wa sekta
binafsi baina ya mataifa hayo, yakiwa ni maombi ya Dk. Mengi, kwa ajili
ya kuimarisha na kufungua milango ya kibiashara kwa wafanyabiashara wa
pande zote mbili.
Balozi Ndilowe alimpongeza Dk. Mengi kwa wito huo, akisema hiyo
ndiyo njia pekee ya kuwaleta pamoja wafanyabiashara wa nchi hizo kupitia
sekta hizo. “Hilo ndilo eneo zuri la kuja pamoja tunaweza kushirikiana,
kuangalia maeneo tunayoweza kuungana…kupitia ushirikiano wa kiuchumi
uliopo kutafungua fursa za biashara baina ya watu wa pande hizi mbili,”
alisema Balozi Ndilowe.
Pia alipongeza kukua kwa sekta binafsi nchini na kuunga mkono
serikali ya nchi yake kutambua mchango wa sekta hiyo nchini humo katika
kuwawezesha wafanyabiashara wakiwamo wa chini.
Awali, Dk. Mengi, alisema litakuwa jambo jema kama sekta binafsi
kutoka pande zote zitakubali kukaa pamoja na kwamba jambo hilo
likiwezekana itakuwa ni enzi mpya katika kuwawezesha wafanyabiashara wa
nchi hizo kuingiliana katika kibiashara huku kila upande ukiwa na nafasi
ya kuangalia fursa upande mwingine kwa ajili ya kuwekeza.
Kutokana na hilo, Dk. Mengi, alisema ni muhimu kwa sekta binafsi
kutoka nchi hizo, kujiamini, hivyo wafanyabishara wake kuwa na ujasiri
wa kwenda kuangalia fursa ambazo zinapatikana katika nchi hizo.
Dk. Mengi pia alitoa wito kwa sekta hiyo kwa pande zote kuwawezesha wafanyabiashara wakiwamo wadogowadogo.
Alitoa wito wa kuwashughulikia wauaji wa watu wenye ulemavu wa
ngozi akipendekeza kuchukuliwa hatua kali siyo kwa wauaji pekee bali pia
kwa wanunuaji wa viungo vya miili ya binadamu kwani wasipofuatiliwa,
wataendeleza uovu huo.
Dk. Mengi alitoa wito wa kukomesha vitendo hivyo ambavyo
vimekithiri huku akiipongeza Malawi kwa jinsi ivyodhibiti uovu
huo, baada ya kuambiwa na balozi huyo kwamba vitendo hivyo havina nafasi
nchini humo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment