Social Icons

Pages

Thursday, April 16, 2015

KAULI YA HAKIMU YA KATIBA MPYA YATISHA VIONGOZI WA DINI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali wilayani Mbozi, Mbeya wameshitushwa na ufafanuzi wa hakimu kwamba kitendo cha mtu kushawishi watu aina ya kura ya kuipigia Katiba inayopendekezwa ni ukiukaji wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 29 ya mwaka 1977 na kwamba ni kosa kuingilia uhuru wa mtu mwingine.
Akiwasilisha mada katika kikao cha pamoja na viongozi hao na wazee maarufu, kati ya Kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya kilichoitishwa na Mkuu wa wilaya ya Mbozi, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Rahimu Mushi, alisema katika mjadala wa katiba inayopendekezwa yameibuka makundi ambayo yameanza kufanya kazi ya watu wengine ikiwemo kuingilia uhuru na haki za watu wengine.
Alisema chanzo cha makundi hayo ni tabia ya Watanzania kutopenda kusoma ambayo imechangia hata wengi kushindwa kuisoma Katiba inayopendekezwa licha ya kugawiwa bure, hivyo kutoa mwanya wa baadhi ya watu kuwasomea na kuwashauri aina ya kura wanayostahili kupigia Katiba hiyo.
Hakimu huyo alisema katika ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa uhuru wa mtu kuwasilisha mawazo yake, lakini Ibara ya 39 kifungu kidogo cha (1) ( a na b) katika katiba inayopendekezwa inatoa uhuru huo pia, lakini ibara ya 19 inakataza mtu kuingilia uhuru wa mtu mwingine, hivyo kuhamasisha watu aina ya kura ya kuipigia katiba hiyo kuwa ni kosa.
Mushi aliongeza kuwa ni vizuri wananchi wenyewe wakaisoma katiba ya sasa na inayopendekezwa, lakini inapotokea mijadala basi waelezwe uzuri wa katiba hizo na ubaya wake kisha waachwe wenyewe watoe maamuzi wanayotaka.
Mchungaji wa Kanisala Baptist, Mlowo Ibrahimu Bukuku, alisema wamepewa katiba hii ili waisome na waelimishe waumini wao inakujaje tena wanaanza kutishiwa, wakati huko nyuma tayari watu wamesikika wakiwaambia watu waipigie kura ya ndiyo na wengine kura ya habana.
Alisema kauli ya hakimu imekuja kama kutoa mwelekeo fulani na vitisho kwa wachungaji na kwamba basi kama ni hivyo waanze kukamatwa kwanza waliotangaza kuwa katiba inayopendekezwa ipigiwe kura ya hapana ama ya ndiyo.
Awali akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ahmad Namohe, aliwaomba viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao kuhusu suala la amani katika jamii na kuacha kuhubiri chuki kwa kupandikiza maneno ya uchochezi hasa katiba inayopendeezwa.
Aidha, aliwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapigakura muda utakapowadia ili kuwapa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais Oktoba mwaka huu pamoja na kuipigaia katiba kura ya ndiyo au hapana baada ya tarehe kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

CHANZO: NIPASHE

No comments: