Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Mnyika, ameitaka serikali
kulichukulia kwa uzito tatizo la kukithiri kwa ajali za barabarani, kama
ambavyo taifa linavyotumia nguvu kubwa kukabiliana na mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi (albino) yaliyofumka kwa kasi kubwa nchini.
Mnyika alisema takwimu za kiwango cha ajali zilizotokea ndani ya
siku 102 zilizotolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabara, Mohamed
Mpinga, zinaonyesha kuwa tatizo hilo ni kubwa, ambalo hatua za haraka
zinahitaji kuchukuliwa.
Alisema haitoshi kwa Rais Jakaya Kikwete kuishia kutuma salamu za
rambirambi kwa waathirika kila ajali inapotokea, badala yake anachopaswa
kukifanya ni kuchukua hatua za kuunganisha nguvu za kitaifa kudhibiti
tatizo hilo.
“Angechukulia uzito wa ajali kama taifa linavyotumia nguvu dhidi ya
mauaji ya albino, kwani idadi ya wanaokufa kwa ajali ni zaidi ya ile ya
albino wanaouawa. Rais aingie kwenye vita kubwa, badala ya kuziachia
takwimu za Mpinga, ambazo hazitekelezwi,” alisema Mnyika na kumtaka pia
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kulizungumzia tatizo hilo.
Alisema Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison
Mwakyembe, alipokuwa waziri wa uchukuzi, aliwahi kuunda kamati
iliyochunguza vyanzo vya ajali nchini. Hata hivyo, alisema uchunguzi huo ulikamilika, lakini mpaka sasa ripoti imefanywa kuwa siri.
Alimtaka Waziri Sitta kuiweke ripoti hiyo hadharani ili kila mdau ajue na kuunganisha nguvu ya pamoja kudhibiti tatizo hilo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment