Dk Hamisi Andrea Kigwangalla alizaliwa Agosti 7,
1975 mkoani Kigoma, hivyo Agosti mwaka huu atafikisha umri wa miaka 40.
Baba yake mzazi Nasser Kigwangalla alikuwa mfanyakazi wa benki na
baadaye mwandishi wa habari, huku mama yake mzazi, Bagaile Lumola akiwa
mwalimu na baadaye akaingia katika siasa ndani ya CCM.
Historia yake
Dk Hamisi Andrea Kigwangalla alizaliwa Agosti 7,
1975 mkoani Kigoma, hivyo Agosti mwaka huu atafikisha umri wa miaka 40.
Baba yake mzazi Nasser Kigwangalla alikuwa mfanyakazi wa benki na
baadaye mwandishi wa habari, huku mama yake mzazi, Bagaile Lumola akiwa
mwalimu na baadaye akaingia katika siasa ndani ya CCM.
Baba na mama wa kijana huyu ni “Wanyamwezi” wa
Tabora kwa asili, na kuzaliwa kwa ‘Kigwa’ mkoani Kigoma kulitokea kwa
vile wazazi wake wote walikuwa waajiriwa huko.
Kigwangalla alitumia sehemu ya maisha yake ya
utotoni katika maeneo ya Goweko na Mlimani yanayopatikana Wilaya ya Uyui
mkoani Tabora na alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari
Kigoma kidato cha kwanza mpaka cha nne.
Baadaye alijiunga kidato cha tano na sita katika
Shule ya Sekondari Shinyanga (Shy Bush) akichukua mchepuo wa PCB
(Physics, Chemistry, Biology). Mwaka 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam ambako alichukua masomo ya udaktari wa binadamu na
alihitimu shahada yake mwaka 2004.
Watu waliosoma na Kigwangalla pale ‘Shybush’ na
hata chuo kikuu, wanamtazama kama kijana wa Kitanzania mwenye juhudi,
anayependa kujisomea, anayependa uongozi wa kujitolea na mwanamichezo
mahiri.
Baada ya hapo Kigwangalla aliendelea na masomo ya
juu zaidi katika Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge nchini Sweden ambako
alisomea Shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA). Pia, alijiunga katika
Taasisi ya Karolinska ambako alisomea Shahada ya Uzamili ya Afya ya
Jamii (MPH) “Public Health”. Taasisi zote hizi ziko nchini Sweden.
Baada ya kuhitimu masomo yake ya juu ughaibuni,
Kigwangalla alirejea nchini na kuanza harakati za kazi za kujipatia
kipato na kuendesha maisha ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wagonjwa kama
daktari.
Alifanikiwa kuanzisha kampuni binafsi na kwa maoni
yake ilimletea mafanikio makubwa ambayo yalisaidia katika safari yake
nyingine, ambayo imekuwa ndoto yake ya muda mrefu – “safari ya kisiasa”.
Kigwangalla ameoa na ana watoto wawili.
Mbio za ubunge
Kigwangalla ni mwana CCM tangu enzi za chipukizi
alipokuwa shule ya msingi. Ni kati ya vijana waliokua na kulelewa na
familia ambayo iliunga mkono chama hicho, hasa mama.
Wakati anaendelea na shughuli zake za ujasiriamali
na kuongoza kampuni yake, aliamua kuweka nguvu za kisiasa katika Jimbo
la Nzega, mahali alipokulia, na mwaka 2010 aliingia rasmi kwenye
kinyang’anyiro cha kuusaka ubunge kupitia CCM.
Mbio za urais
Nguvu zake
Udhaifu wake
Nini kinaweza kumwangusha?
Asipopitishwa (Mpango B)
Hitimisho
Hakika, uamuzi wake wa kugombea ubunge katika jimbo hilo
haukuonekana kama jambo la “mashiko” kwa wana CCM wa jimbo hilo. Kwanza,
hakuwa anafahamika Nzega; pili, hakuwa chaguo la wana Nzega. Chaguo la
wana Nzega lilikuwa Hussein Bashe, ambaye katika kura za maoni,
alishinda na kuwaacha mbali mbunge aliyekuwa anamaliza muda wake Lucas
Selelii huku Kigwangalla akishika nafasi ya tatu.
Vikao vya juu vya CCM vilipokutana Dodoma, tayari
makundi ya ndani ya chama hicho yalikuwa yanashughulikiana na hivyo “kwa
mizengwe ya hali ya juu” chama hicho kilimtosa Bashe. Aidha, CCM
haikumchukua mshindi wa pili kwenye kura ya maoni yaani Seleli,
kikamrukia mshindi wa tatu ambaye ni Kigwangalla.
Ni muhimu tukakumbushana kuwa Kigwangalla ni mtu
mwenye bahati sana; kutoka kuwa mshindi wa tatu kwenye kura ya maoni
ndani ya chama hadi kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho,
kushinda ubunge katika mazingira ya kupingwa ndani ya chama na sasa kuwa
mtangaza nia ya urais. Ni wanasiasa wachache sana wamepitia bahati
kubwa kama hii.
Hadi ninapoandika uchambuzi huu, Kigwangalla ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Kijamii ambayo
inafanya kazi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Mbio za urais
Kigwangalla aliingia katika orodha ya watangaza
nia ya urais ndani ya CCM, Septemba 7, 2014 jijini Dar es Salaam. Alitoa
hotuba ya kurasa 21 kwa vyombo vya habari akijieleza yeye ni nani,
ametoka wapi na kwa nini anaitaka nafasi kubwa kabisa ya uongozi wa
nchi.
Siku hiyo aliambatana na mke wake na watoto wake
pamoja na wanafamilia wengine ili kuonyesha kuwa katika kuianza safari
yake hiyo hayuko peke yake, kwani familia nzima inamuunga mkono.
Kigwangalla hajaonywa na chama chake kama wenzake
sita na labda hiyo inatokana na aina ya mikakati yake ambayo haijavunja
taratibu za chama hicho kikongwe.
Nguvu zake
Nguvu za Kigwangalla zinatokana na maarifa
aliyopata katika elimu yake. Huyu ni kijana makini na mfuatiliaji wa
kila jambo na hapendi kupitwa na lolote lile ambalo ana wasiwasi kama
litamkwamisha au kuwakwamisha wengine mbeleni.
Shahada zake tatu za chuo kikuu ni moja ya
mafanikio makubwa kwa kijana yeyote ambaye ana visheni pana siku za
mbele. Elimu hii, akiichanganya na uzoefu wake katika ubunge anaweza
kuwaeleza wana CCM kwamba yeye ni chaguo lao.
Ujana unaweza pia kuwa sababu muhimu kwake.
Hatujui CCM itakuja na ‘gia’ gani katika uchaguzi huu, baada ya
kukamilisha miaka 10 ya Rais Jakaya Kikwete. Mbinu inayoweza kutumika ni
ya kutafuta mtu wa kizazi cha sasa na hilo likitokea itakipasa chama
hicho kumfikiria yeye na vijana wengine walioomba ridhaa. Ujana ni
silaha ambayo itamsaidia Kigwangalla pamoja na mambo mengine.
Nguvu nyingine ya Kigwangalla ni ung’ang’anizi. Kati ya vijana
ambao hung’ang’ania jambo lao hadi liwe ni pamoja na Kigwangalla. Yeye
mwenyewe anajitambua hivyo na anakumbuka enzi za nyuma akiwa shuleni
ambavyo wenzake pia walimchukulia hivyo.
Faida ya uki-ng’ang’anizi ni mafanikio, lakini pia
hasara yake huwa ni kung’angania hata yale ambayo hayapaswi
kung’ang’aniwa. Viongozi ving’ang’anizi, mara zote, hufika mbali na huwa
hawakati tamaa katika mipango yao hata wachekwe. Ndiyo maana pamoja na
kujua kwamba Bashe ndiye ameiteka Nzega kiasi kile, bado alikwenda
kuomba ridhaa na ikamletea bahati iliyompeleka bungeni. Asingekuwa
king’ang’anizi na akaogopa vivuli vya Bashe na Selelii, hakika
asingefika bungeni.
Udhaifu wake
Moja ya taswira za Kigwangalla na ambayo si salama
kwake, ni majivuno. Kwa watu wanaomfahamu ni kijana anayejisikia sana
na anadhani ni mwerevu kuliko watu wengine. Mfano, tulipokuwa katika
Bunge Maalumu la Katiba, mara kadhaa, wabunge wenzake wa CCM na hata
kundi la 201 walisikika wakimsema na ukiwauliza walikuwa wakisema ni;
“mtu wa kujisikia”.
Inawezekana kabisa Kigwangalla akawa anatupiwa
maneno yasiyo ya kweli, lakini masuala ya uongozi huathiriwa sana na
mitazamo ya jamii juu ya kiongozi. Kama jamii inakuchukulia wewe si mtu
msafi, basi jambo hilo ni hatari kwako. Kwa siasa za “nipe nikupe” ndani
ya CCM mtu anayejisikia anakuwa na nafasi ndogo kwa sababu atashindwa
kutimiza matakwa ya makundi ya chama hicho, ambacho kinajiendesha kwa
siasa za kulipana hisani.
Udhaifu wake mwingine ni kutojijenga jimboni kwake
Nzega. Siku chache baada ya yeye kukoswakoswa risasi katika harakati za
kuwatetea wachimbaji wadogo wa Nzega, nilikuwa mjini Nzega.
Nilipowauliza vijana juu ya mbunge wao huyo kijana walinijibu kuwa
“…huyo ni wa wakubwa” na eti mbunge wa wana Nzega alipokonywa Dodoma.
Baadhi ya wana Nzega wanasisitiza kuwa Kigwangalla
si mbunge wao wa moyoni jambo lenye maana kuwa hajajijenga kisiasa.
Kama umekuwa mbunge na umeshindwa kujijenga jimboni mwako, huo ni
udhaifu mkubwa sana ambao unakupunguzia alama za kuendelea na safari
hiyo au ya juu zaidi.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Mambo mawili yanaweza kumfanya Kigwangalla apewe
uzito na CCM. Jambo la kwanza ni elimu yake ambayo imechanganyika na
utaalamu wa masuala ya biashara na kutibu binadamu. Nchi yoyote ile
ingependa kuwa na rais ambaye moja ya sifa zake pia ni elimu nzuri,
isiyo na mashaka mashaka na ambaye anaweza kutumia elimu na maarifa yake
kulinufaisha taifa lake.
Kuongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za
Jamii ni sifa thabiti ambayo inamfanya Kigwangall awe na uzoefu wa
kujivunia, ambao pengine raia na wanasiasa wengi hawataweza kuipitia.
Uzoefu huu, japokuwa ni wa kawaida, una maana kubwa kwake katika safari
yake hii.
Jambo la tatu, CCM inaweza kujikuta inahitaji mtu
mwadilifu. Kigwangala hana rekodi ya kuwa kiongozi wa Serikali au ya
kuwa mtendaji wa Serikali mwenye mamlaka makubwa. Jambo hilo linamfanya
awe mbali na kashfa nyingi ambazo huwakumba watu wa namna hiyo. Kati ya
wagombea urais wanaotajwa ndani ya CCM, huenda yeye ndiye anaweza kuwa
miongoni mwa wasio na kashfa na jambo hili ni msingi mkubwa wa kuomba
ridhaa.
Nini kinaweza kumwangusha?
Kukosa uzoefu na uongozi ndani ya chama chake ni jambo moja
linaloweza kumwangusha kwenye mchujo wa urais. Ndani ya CCM, sifa hii ni
muhimu na ukiikosa unapaswa walau kuwa na sifa nyingine zinazotajwa.
Kwa bahati mbaya, Kigwangalla hana uzoefu wa kutosha wa uongozi wa ngazi
ya juu ndani ya chama chake.
Vita ya urais ni jambo kubwa sana. Inataka
maandalizi, utayari, historia ya muda mfupi au muda mrefu, rekodi
mbalimbali n.k. Zaidi ya rekodi nzuri ya elimu pamoja na uongozi wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kigwangalla hana rekodi nyingine kubwa ya
masuala aliyoyasimamia katika nchi hii. Siyo kwa sababu hana uwezo wa
kusimamia masuala hayo, la hasha! Ni kwa sababu aliingia katika siasa
mwaka 2010, tena katika ngazi ya ubunge na miaka mitano baadaye
anahitaji kuwa rais.
Pia, kukosa uzoefu wa uongozi serikalini ni tatizo
lingine. Kigwangalla hakuwahi kufanya kazi serikalini kama mtu muhimu
au kama kiongozi au mtendaji muhimu katika Serikali na kwa hivyo,
hajashiriki ipasavyo katika “urasimu” wa Serikali na kujua nini
kinaendelea ndani. Atakapopambanishwa na wenzake ataonekana kama chaguo
la kubahatisha.
Sababu ya tatu inayoweza kumwangusha ni kukosa
mvuto kwa vijana. Ikumbukwe kuwa ikiwa CCM itaamua kumsimamisha Rais
kijana katika kinyang’anyiro cha mwaka huu, lengo litakuwa kusaka kura
za vijana. Lakini CCM haiwezi tu kumweka kijana yeyote yule.
Kwa bahati mbaya, Kigwangalla hatazamwi vizuri na
vijana wengi wa Tanzania na kipimo kidogo ni namna ambavyo vijana wengi
wanamtolea maoni katika mitandao ya kijamii pale anapotoa maoni yake.
Mara nyingi hupingwa na kusemwa vibaya. CCM itahitaji kura za urais na
itahitaji kijana mwenye mvuto ikiwa itaamua kumweka kijana. Simwoni
Kigwangalla katika “mvuto” huo unaoweza kuwashawishi wapiga kura.
Ukitaka kuwa rais kupitia chama chochote, lazima
uwe unaungwa mkono vizuri katika chama chako, viongozi wenzako na watu
wenye mamlaka katika vikao vya maamuzi. Upekuzi wangu umejiridhisha kuwa
Kigwangalla hatajwi kabisa na viongozi mbalimbali wa chama chake na
hata wanachama, linapokuja suala la kumfikiria katika nafasi hiyo nyeti.
Kutoungwa mkono huku ndani ya chama ni sababu muhimu ya kutopitishwa
kuwa mgombea.
Jambo la mwisho litakalomwangusha Kigwangalla ni
kufanya mambo mengi peke yake na kukosa mtandao wa kutosha ndani ya CCM
na wakati huo huo akiwa hana pesa za kutosha. Ndani ya CCM kama huna
mtandao wa kutosha, waratibu wa kutosha na pesa za kutosha, urais
unabakia ndotoni mwako na unaweza kuusaka milele.
Asipopitishwa (Mpango B)
Ninachokiona, Kigwangalla ametangaza safari ya
urais huku akiwa hajui mbele kukoje. Namwona kama ni “parliamentary
material” (anayefaa kwa ubunge) kuliko “Presidential Material” (anayefaa
kwa urais) kwa wakati huu. Ikiwa hatachaguliwa kuipeperusha bendera ya
urais, Kigwangalla atarudi kugombea ubunge japokuwa, hali ya kisiasa
ndani ya CCM jimboni Nzega siyo nzuri.
Kigwangalla hadi sasa ana nafasi finyu sana ya
kupenya kwenye tundu la kura ya maoni ndani ya CCM kusaka ubunge wa
Nzega, kwa mara ya pili, achilia mbali mzigo mzito anaojipa wa kutaka
kujitwisha urais.
Mpango wake mwingine unaweza ukawa kurudi chini na
kuomba ridhaa ya uongozi ndani ya chama chake, kwa ngazi ya wilaya,
mkoa au taifa na kujipanga kukitumikia chama hicho miaka mingine mitano,
kuonyesha uwezo wake na kutumia fursa hiyo kuijua mifumo ya uendeshaji
wa CCM, kuwa karibu na wanachama na kujiibua tena upya akitokea ndani ya
chama kuomba ridhaa kubwa za kiserikali.
Hitimisho
Watu wenye historia ndefu duniani na ambao waliingia katika
siasa na ndani ya muda mfupi wakakwaa ukubwa wa nchi ni pamoja na Rais
Barack Obama wa Marekani. Obama alikuwa seneta na kisha akawa rais,
lakini ukifuatilia utagundua ni Mmarekani mweusi aliyesimamia masuala
makubwa sana nchini mwake tangu akiwa mwanafunzi wa sheria na hata ndani
ya chama chake cha Democrat. Huenda Kigwangalla hana hata robo ya sifa
za Obama kabla hajawa rais.
Ni vema muda mwingi anaotumia kusaka urais
angeutumia kugeuza vichwa vya wana Nzega pamoja na wana CCM wenzake ili
watathmini kazi aliyofanya kama mbunge na walau kumpa kipindi cha pili
cha uongozi jimboni.
Ukiniambia nimpe alama rafiki yangu Kigwangalla,
naweza kumpa alama chache sana kama uhakika wa kupenya vizingiti vya
ndani ya CCM na kuteuliwa kukiwakilisha chama chake kwenye uchaguzi mkuu
wa Oktoba mwaka huu. Hata hivyo, tunamtakia kila la heri katika
kutimiza ndoto zake kisiasa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment