Pages

Wednesday, April 22, 2015

ZITTO: ELIMU, AFYA TATIZO NCHINI

Kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema tatizo la elimu, afya na miundo mbinu ya barabara nchini limekuwa sugu na kuongeza kundi kubwa la vijana wasio na ajira.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mkendo, Musoma mjini, Zitto, alisema matatizo yanayoikabili taifa ni mengi na kuwakosesha ajira vijana wanaoteseka baada ya serikali kuamua kubinafsisha viwanda nchi nzima. “Wanasiasa tunatakiwa kutafuta ufumbuzi wa matatizo waliyonayo wananchi hususani vijana kwa kukosa ajira, tatizo ambalo kwetu ni bomu kwa taifa…rasilimali za nchi zinanufaisha wachache, ufisadi na rushwa umekuwa changamoto kubwa,” alisema Zitto.
Alisema: “Watoto hawana elimu bora, huduma za afya haziridhishi na miundombinu ya barabara imekuwa tatizo kubwa nchini, tuzungumzie hali hiyo badala ya kunyoosheana vidole.” Katika hatua nyingine, Zitto alisema hawezi kutumika na Chama Cha Mapinduzi (CCM), bali mambo yanayozungumzwa kuhusu chama hicho ni upotoshaji mkubwa.
“Sishangazwi na kauli hizo kwani hata CUF waliitwa ‘mashoga’ baada ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, Mbatia (James) naye aliitwa CCM B baada ya kuteuliwa ubunge na Rais Jakaya Kikwete na Mabere Marando akaitwa pandikizwi, baada ya kugombana na Mrema,” alisema Zitto.
Alisema Tanzania ni nchi tajiri, lakini wananchi wake ni maskini hali inayotokana na viongozi wa nchi kutojali maisha ya wananchi kwa kutoweka utaratibu wa kuhakikisha kila mmoja anaishi katika hali nzuri ya maisha kulingana na uchumi unaozalishwa nchini.
Naye mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Ngwira, alisema nia na madhumuni ya chama hicho ni kutetea maslahi ya wananchi kwa kufuata mafundisho ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyoyataja ni undugu, uzalendo na uwajibikaji.
Ngwira alisema endapo haki itatendeka katika utendaji wa serikali kulingana na hali halisi ya utajiri wa nchi, ni vyema kila Mtanzania akaanza kulipwa mafao ya uzeeni kutoka katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwahamasisha wananchi kuchangia gharama kidogo kulingana na hali halisi ya maisha anayoishi.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Shabani Mambo, alisema siasa ni maisha endelevu na kuwataka wananchi kutochezea siasa kwa kudanganywa na kwamba ikiwa watachezea siasa watakuwa wamechezea maisha.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment