Mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Cecilia Mosha (24), amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kujirusha kutoka ghorofa ya tatu alipokuwa katika harakati za kujinusuru na ajali ya moto uliozuka katika jengo la bweni la wasichana katika Hosteli ya Mabibo, jijini Dar es Salaam.
NIPASHE ilifika eneo hilo na kushuhudia wanafunzi wengi wakiwa nje
ya hosteli hiyo, huku vitu mbalimbali vinavyotumiwa na wanafunzi
vilivyokuwa vikihifadhiwa sehemu ya ghorofa, yakiwamo mabegi, nguo na
madaftari vikiwa vimetupwa chini.
Wanafunzi hao walilalamika kuibwa vitu vyao vilivyokuwa vikiokolewa kutoka ghorofani. Baadhi ya wanafunzi walisema moto huo ulianza majira ya saa 3.00 asubuhi na kwamba, uliteketeza vitu vyote vilivyokuwamo.
Mmoja wa wanafunzi, Samuel Mdema, alisema pamoja na kufanikiwa
kuzima moto huo, vitu vya baadhi ya wanafunzi vimeibwa na watu waliokuwa
wakijifanya kusaidia katika uokoaji. “Moto tulifanikiwa kuuzima tukishirikiana na wafanyakazi wa chuo,
lakini mizigo ambayo ilikuwa ikirushwa kutoka ghorofani hadi chini
haijaonekana kwa kuwa kuna baadhi ya watu walikuwa wanaiba vitu hivyo,
kitendo hicho siyo kizuri. Kama mtu amepata matatizo, msaidie siyo
kumuangamiza tena ,” alisema.
Alisema wakati tukio hilo linatokea, baadhi ya wanafunzi walikuwa
chuoni Mlimani, hivyo hawana uhakika kama watakuta mali zao zikiwa
salama kutokana na vitu vya wenzao kuibwa. Kabura Benjamin alisema alichobahatika kuokoa ni simu zake tu,
lakini vitu vingine vyote aliviacha bwenini kwa kuwa muda, ambao moto
ulianza kuwaka, alikuwa bafuni anaoga.
“Nilikuwa bafuni naoga. Ghafla nikasikia sauti za watu wanasema
moto, moto, moto, huku wakikimbia na niliposikia, nilitoka bafuni na
kanga nami nikaanza kukimbia kushuka chini kutoka ghorofani,” alisema
Kabura. Disho Thomas alisema alisikia kelele za moto kutoka kwa wafanya usafi, hivyo akajiunga kwenda kuokoa baadhi ya vitu.
Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walifika eneo la tukio,
lakini wakazomewa na wanafunzi huku wakiwaambia wameenda kufanya nini
wakati moto umeshazimwa. Bosco Mrisho alisema zimamoto wamezoea kuchelewa kila matukio ya
moto na kusema kama siyo matenki ya kuhifadhia maji kupasuka na kumwaga
maji kwenye moto, ungeteketeza jengo lote.
Naye Sajenti wa kikosi hicho, Emmy Cosmas, alisema taarifa za moto
walizipata saa 4:03 asubuhi na kwamba, walifika eneo la tukio saa 4:19
asubuhi kutoka Tazara-Mchicha na walipofika walikuta chumba kimoja
kimeshateketea na vitu vyote vilivyokuwamo ndani ya chumba hicho.
Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Rwekaza Mukandala (pichani), alisema
wanafunzi 45 waliokuwa wakiishi ghorofa ya tatu watatafutiwa sehemu ya
kuishi hadi pale watakapopokea taarifa kamili kutoka kwa watu
wanaofanyia uchunguzi jengo hilo. Prof. Mukandala alisema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
Hata hivyo, alisema wanafunzi hao watatafutiwa sehemu nyingine ya kuishi na chuo kitawagharimia mahitaji yote.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment