Pages

Tuesday, March 17, 2015

MOTO WATEKETEZA MABIBO HOSTELI UDSM

 Baadhi ya vitu vilivyonusurika kuteketea kwa moto ulioonguza vyumba kadhaa vya wasichana katika hosteli za Chuo Kikuu Dar es Salaam zilizopo Mabibo jijini Dar es Salaam jana.

Mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Cecilia Mosha (24), amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kujirusha kutoka ghorofa ya tatu alipokuwa katika harakati za kujinusuru na ajali ya moto uliozuka katika jengo la bweni la wasichana katika Hosteli ya Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Pia mwanafunzi mwingine wa UDSM, ambaye hajafahamika, amelazwa katika zahanati ya chuo hicho, baada ya kupoteza fahamu kutokana na kuzidiwa na wingu zito la moshi uliotokana na moto huo. Moto huo, ambao chanzo chake kinadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme, umeteketeza vyumba vinne vya hosteli hiyo pamoja na mali zote zilizokuwamo.
NIPASHE ilifika eneo hilo na kushuhudia wanafunzi wengi wakiwa nje ya hosteli hiyo, huku vitu mbalimbali vinavyotumiwa na wanafunzi vilivyokuwa vikihifadhiwa sehemu ya ghorofa, yakiwamo mabegi, nguo na madaftari vikiwa vimetupwa chini.
Wanafunzi hao walilalamika kuibwa vitu vyao vilivyokuwa vikiokolewa kutoka ghorofani. Baadhi ya wanafunzi walisema moto huo ulianza majira ya saa 3.00 asubuhi na kwamba, uliteketeza vitu vyote vilivyokuwamo.
Mmoja wa wanafunzi, Samuel Mdema, alisema pamoja na kufanikiwa kuzima moto huo, vitu vya baadhi ya wanafunzi vimeibwa na watu waliokuwa wakijifanya kusaidia katika uokoaji. “Moto tulifanikiwa kuuzima tukishirikiana na wafanyakazi wa chuo, lakini mizigo ambayo ilikuwa ikirushwa kutoka ghorofani hadi chini haijaonekana kwa kuwa kuna baadhi ya watu walikuwa wanaiba vitu hivyo, kitendo hicho siyo kizuri. Kama mtu amepata matatizo, msaidie siyo kumuangamiza tena ,” alisema.
Alisema wakati tukio hilo linatokea, baadhi ya wanafunzi walikuwa chuoni Mlimani, hivyo hawana uhakika kama watakuta mali zao zikiwa salama kutokana na vitu vya wenzao kuibwa. Kabura Benjamin alisema alichobahatika kuokoa ni simu zake tu, lakini vitu vingine vyote aliviacha bwenini kwa kuwa muda, ambao moto ulianza kuwaka, alikuwa bafuni anaoga.
“Nilikuwa bafuni naoga. Ghafla nikasikia sauti za watu wanasema moto,  moto, moto,  huku wakikimbia na niliposikia, nilitoka bafuni na kanga nami nikaanza kukimbia kushuka chini kutoka ghorofani,” alisema Kabura. Disho Thomas alisema alisikia kelele za moto kutoka kwa wafanya usafi, hivyo akajiunga kwenda kuokoa baadhi ya vitu.
Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walifika eneo la tukio, lakini wakazomewa na wanafunzi huku wakiwaambia wameenda kufanya nini wakati moto umeshazimwa. Bosco Mrisho alisema zimamoto wamezoea kuchelewa kila matukio ya moto na kusema kama siyo matenki ya kuhifadhia maji kupasuka na kumwaga maji kwenye moto, ungeteketeza jengo lote.
Naye Sajenti wa kikosi hicho, Emmy Cosmas, alisema taarifa za moto walizipata saa 4:03 asubuhi na kwamba, walifika eneo la tukio saa 4:19 asubuhi kutoka Tazara-Mchicha na walipofika walikuta chumba kimoja kimeshateketea na vitu vyote vilivyokuwamo ndani ya chumba hicho.
Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Rwekaza Mukandala (pichani), alisema wanafunzi  45 waliokuwa wakiishi ghorofa ya tatu watatafutiwa sehemu ya kuishi hadi pale watakapopokea taarifa kamili kutoka kwa watu wanaofanyia uchunguzi jengo hilo. Prof. Mukandala alisema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
Hata hivyo, alisema wanafunzi hao watatafutiwa sehemu nyingine ya kuishi na chuo kitawagharimia mahitaji yote.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment