
Rais mstaafu Benjamin Mkapa
amesema sekta ya uwekezaji nchini inashindwa kukua kwa kasi
inayotarajiwa kutokana na baadhi ya wanasiasa kutokuielewa vizuri.
Akizungumza leo wakati wa kusaini makubaliano ya
kusaidia kuvutia na kuongea uwekezaji wa ndani na nje nchini kati ya
Taasisi inayoshughulikia mazingira ya uwekezaji Barani Afrika (ICF) na
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza
wa ICF alisema baadhi ya watu wanautazama uwekezaji kama unyonyaji.
“Watu wanaona wanataka kunyonywa na sio kunyonyana,” alisema Mkapa wakati akielezea mafanikio ya TIC tangu kuanzishwa kwake. Chini ya makubaliano hayo yaliyosainiwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa ICF, William Asiko na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC,
Juliet Kairuki, ICF itakisaidia kituo cha uwekezaji nchini kukuza,
kuinua na kulingaza dirisha la uwekezaji na kuimarisha uwezo wake katika
kuwezesha na kufuatilia uwekezaji nchini.
Kairuku alisema Dola 950,000 (Sh1.7 bilioni)
zitatolewa kwa ajili ya mradi wa dirisha la uwekezaji Tanzania ambazo
zitachangwa kwa pamoja kati ya ICF na Serikali ya Tanzania kwa lengo la
kurahisisha huduma zote zinazotolewa TIC kupatikana haraka, kwa ufanisi
na bila kupoteza muda. “Huduma zote zinazotolewa na TIC sasa zitakuwa
zikipatikana mtandaoni ikiwa ni pamoja na kulipia ada mbalimbali,
tunajaribu kuwa wa kisasa,” alisema Kairuki na kuongeza kuwa huduma hiyo
itawanufaisha zaidi wawekezaji wa mikoani.
Mpango huo unatarajiwa kuwapa wananchi nafasi ya
kupata huduma zote za kituo hicho kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato
nchini (TRA), Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya HIfadhi za
Jamii (SSRA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kwa
kutumia mfumo wa kieletroniki.
Mwenyekiti mwenza wa ICF, Neville Isdell alisema
uwekezaji unahitaji uwazi ili kuwavutia wafanyabiashara wa ndani na nje
kuendelea kuwekeza. “Biashara zote hususani zilizo ndogo zinahitaji
kuwa na mazingira yaliyo mazuri watakayofanyia shughuli zao. Kwa kuwa na
dirisha la uwekezaji biashara nyingi zitaweza kukua, kuongezeka na
kushamiri haraka,” alisema Isdell.
Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Christopher
Chiza alisema mradi huo utakapokamilika utasaidia kuboresha mazingira ya
biashara na ushindani nchini. “Kwa muda wa miaka michache iliyopita nafasi ya
Tanzania kimataifa katika kufanya biashara kwa mujibu wa ripoti
mbalimbali imekuwa hairidhirishi, ishara ambayo sio nzuri kwa wawekezaji
na sekta binafsi,” alisema Chiza.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment