Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akifafanua jambo
alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalumu na waandishi na wahariri wa
magazeti ya Mwananchi Communications Limited, alipotembelea ofisi za
magazeti hayo Tabata Relini, Dar es Salaam jana.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji
Peter Msigwa amesema zaidi ya asilimia 80 ya wabunge waliopo bungeni
sasa hawakustahili kuwa wabunge kwa sababu baadhi yao wana uwezo mdogo
kiakili alioulinganisha na GB moja ya kompyuta. Msigwa alisema kwa maoni yake, ni asilimia 20
pekee ya wabunge ndiyo wenye uwezo na vigezo vinavyostahili kupata
nafasi hiyo ya uwakilishi wa wananchi katika chombo hicho cha kutunga
sheria.
Mchungaji Msigwa alikuwa akizungumza na wahariri
alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd
inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, Tabata
Relini, Dar es Salaam jana. Alisema wakati umefika kwa Taifa kuweka viwango maalumu vya kuwapata viongozi wa kisiasa wakiwamo wabunge na Rais.
“Tatizo kubwa Watanzania hatuna ‘standards’
(viwango) na vigezo tunavyoviweka kwa mtu anayetaka kuwa kiongozi, yaani
tujue kuwa mtu anayekuja kuomba uongozi anapaswa awe mtu wa aina gani. “Tutakuwa tunafanya makosa makubwa kama Taifa,
ikiwa hatutakuwa na ‘standards’. Vinginevyo tutapata hata wasio na sifa
ndiyo hawa wanaojitengenezea maandamano kwa kujifanya kuwa ni maarufu.”
Alisema kigezo kinachozingatiwa katika siasa ili
kuwa mbunge cha kujua kusoma na kuandika hakitoshi na siyo sahihi, hivyo
kinapaswa kitazamwe upya ili kupata wawakilishi watakaoweza kutimiza
wajibu wao ipasavyo wakiwa watungaji wa sheria na watetezi wa rasilimali
za Taifa. “Tunaambiwa kigezo muhimu cha kuwa kiongozi
akiwamo mbunge ni kujua kusoma na kuandika, hii siyo sahihi kwani kujua
kusoma na kuandika pekee hakutoshi kuwa kigezo cha mtu kuwa mbunge au
kiongozi,” alisema.
“Kujua kusoma na kuandika siyo kigezo cha kupitia
vifungu vya sheria. Unajua kuna baadhi ya wabunge kutokana na upeo
mdogo, mtu kama Tundu Lissu akiongea kule ndani (bungeni) hawaelewi,
ndiyo maana unakuta wanaishia kumwona kama kichaa. “Wabunge wengi hawamuelewi Tundu Lissu, kwa sababu
vichwa vyao vina ‘GB’ moja za ubongo. Sasa ‘kucontain’ (kukusanya)
mambo yote yale ya Bunge, kichwa kinapata moto na ili kupata majibu
rahisi, wanasema ni (Lissu) kichaa, maana hawawezi kufikiri kiwango kile
kutokana na akili yao kuwa ni ndogo sana,” alisema Msigwa bila kutaja
majina ya wabunge hao.
Alisema mbunge anapaswa kuwa na uwezo wa
kujieleza, kuelewa mambo, kusoma mambo mengi, akisisitiza kuwa kwa
ilivyo sasa ni kama asilimia 20 ya wabunge wote, ndiyo wenye sifa na
uwezo wa kujadili mambo.
“Wengi wao wamekaa kaa tu, hawawezi kusema lolote,
wabunge wengine tunaposafiri nao, tunashuhudia mambo ya aibu tupu.
Wengi wanakuwa kama mabubu, wamekaa kaa tu, hawasemi chochote, hawana
michango yoyote, wanasubiri kufanya ‘shopping’ tu kana kwamba wamekwenda
kwa ajili hiyo,” alisema Msigwa. Alisema wapo wabunge ambao tangu walipochaguliwa hawaonekani kuwa na thamani kwani hawachangii lolote bungeni.
Suti za wabunge
Alipoulizwa jambo analojutia katika maisha ya
siasa, Mchungaji Msigwa alisema kabla ya kuwa mbunge hakufahamu haiba ya
wabunge waliopo, akivutiwa na suti zao, hadi alipopata fursa ya kuingia
bungeni na kushuhudia udhaifu wa wabunge walio wengi. “Nilipokuwa naona wabunge wanavaa suti kule ndani,
nilikuwa navutiwa nao na kutamani niwe mbunge baada ya kuwa mbunge na
kuingia ndani kule, nimegundua wabunge wengi hawana sifa zinazofanana na
suti wanazovaa. Hawapo makini na wanawadanganya Watanzania na suti zao,
zile suti zao ni kuficha uhalisia wao, lakini hawana nia na dhamira ya
dhati ya kuleta mabadiliko,” alisema.
Aliongeza: “Wengi wao hawajui wanachokitaka, ndiyo
maana unaona mbunge anasema akitoka chama hiki, anakwenda kile, maana
lengo lake ni kuendelea kuwa mbunge tu.” Kuhusu jambo analojivunia alisema: “Nimefanya kazi
kubwa ya ‘kuchange mind set’ (kubadilisha fikra za watu). Hiyo ndiyo
ilikuwa hoja yangu jimboni, naamini hata bungeni nimelifanya hilo.”
Vigezo vya Chadema kushinda
Akizungumza kwa kujiamini, mchungaji huyo
aliyeingia bungeni mwaka 2010 alisema katika Uchaguzi Mkuu ujao Chadema
kina uhakika wa kushinda kutokana na vigezo walivyonavyo huku
akiviainisha. “CCM imeendelea kushuka, kwa mfano, jimbo langu
pale, CCM imekuwa ‘unpopular’ (siyo maarufu tena). Wanashindwa hata
kufanya mikutano kwenye jimbo, lakini kibaya zaidi Serikali imeshindwa
kabisa kutimiza malengo na matumaini ambayo wananchi walikuwa nayo.
“Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, chama
chetu kimekua sana. Kwa muda mrefu chama chetu kilikuwa kinasubiri Zitto
Kabwe, Dk Willibrod Slaa au Freeman Mbowe wafanye mikutano, lakini
baada ya kuunda kanda 10, chama chetu kimepanuka sana. “Kimepanuka kwa sehemu kwa sana kama vile matofali
yakichomwa likianza moja mengine yanaanza kujiunguza yenyewe. Mikutano
ya Chadema haimsubiri mtu. Hiyo siyo kwa Iringa pekee, ukienda Mufindi,
Kilolo, Ludewa ndiyo hivyohivyo ni kila mahala hata maeneo ambayo
hatuna mbunge, moto umesambaa… wananchi wameendelea kuiamini Chadema.
“Jingine, katika uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2010,
Rais Jakaya Kikwete ameingia madarakani baada ya kupata asilimia 62 ya
kura wakati alikuwa anatoka Ikulu. Alikuwa na ‘control’ (udhibiti) wa
‘machinery’ (mifumo) yote. Sasa anakuja mwingine kukutana na adui
yuleyule ambaye ameimarika zaidi na pale Ikulu inakwenda kuwa Ikulu
ambayo haina mwenyewe,” alisema. “Tunakwenda kwenye majimbo ambayo kila
mtu anakwenda kufa peke yake. Hautakuwa kama uchaguzi wa Kalenga ambao
walikuja wote kushambulia, sasa hivi kila mtu anakwenda kupambana
mwenyewe. Ndiyo maana tunasema, tuna kila sababu ya kusema uchaguzi huu
kama utakuwa wa huru na haki hawa jamaa hawachomoki.”
Ukomo wa ubunge
Manispaa ya Iringa
Akitaja kigezo kingine cha ushindi wa Chadema Mchungaji Msigwa
alisema: “Kwa msuguano uliopo ndani ya CCM… haitatoka salama. Kama
wakati ule makundi ya Kikwete yalidumu kwa miaka 10 hata sasa, makundi
ndani ya chama hicho hayatakosekana. Kwa hiyo kugawanyika kwao ni faida
kwetu.”
Ukomo wa ubunge
Akizungumzia majaliwa yake kisiasa, Mchungaji
Msigwa aliyesema ana uhakika wa kushinda ubunge kwa kipindi cha pili,
endapo chama hicho hakitashinda urais Oktoba mwaka huu, kitakuwa kipindi
chake cha mwisho kwa ubunge. “Labda tukishinda nchi (urais) nitagombea tena,” alisema Mchungaji Msigwa.
Alipoulizwa iwapo kauli yake kuwa ataendelea
kuwania ubunge iwapo watatwaa urais inaonyesha wasiwasi wake wa
kutoshinda nafasi hiyo, Msigwa alisema: “Siwezi kusema nina wasiwasi, lakini katika
chaguzi za kiafrika ‘anything can happen’ yaani unaweza ukashinda
ukanyang’anywa, hata katika uchaguzi uliopita nilikuwa katika hatari ya
kunyang’anywa.
“Nilishinda tangu saa mbili usiku, lakini matokeo
yakatangazwa siku ya pili saa 10 jioni na hapo niliambiwa na vijana wa
Usalama wa Taifa, unajua kuna Usalama wa Taifa ni wazuri. Waliniambia
umeshinda lakini wanataka kukunyang’anya ushindi. Sikulala siku hiyo
vijana waliniletea ‘Red Bull’ 10,” alisema Msigwa.
Manispaa ya Iringa
Alisema katika uchaguzi ujao, mbali na ilani ya chama, atafanya kampeni ya kuchukua Manispaa ya Iringa Mjini. “Nataka tuongeze pato la Iringa Mjini. Wakati
ninaingia, manispaa ilikuwa inaingiza Sh900 milioni na sasa tunaingiza
Sh3.2 bilioni, tunataka mapato yaongezeke na kufikia Sh7 bilioni ili
Iringa mjini tuweze kujijengea miundombinu. Tujue ‘pedestrian’ (waenda
kwa miguu) wanatembeaje hata waendesha baiskeli, badala ya kutegemea
Serikali Kuu,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu hatima ya Ukawa katika uchaguzi
na anavyompima mpinzani wake kisiasa kutoka CCM, David Mwakalebela,
ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe kama ni tishio kwake,
alisema: “Nianze na jimbo. Kwa Mwakalebela siyo ‘threat’
(tishio) kwangu hata kidogo. Sasa hivi CCM wanagombana kuhusu ubunge.
Wakati ule walisema nilishinda kwa sababu eti Mwakalebela hakugombea.
Sasa Kikwete (Rais) angefanya vizuri sana asingempeleka
Wanging’ombe, angemleta Mwakalebela pale Iringa Mjini kuwa mkuu wa
wilaya, tuwe wote pale yeye anakuwa na cheo cha DC, mimi mbunge.
Angefanya vizuri sana kampeni zake za ubunge. Nasema hivi kwa sababu ‘he
is not a threat at all’ (yeye siyo tishio kwangu kabisa).”
Aliongeza: “Kinana alivyokuwa Iringa Mjini
aliwaambia watu wa Iringa mjini huyu Msigwa alishindaje? Mmemchaguaje
wakati ninyi ni watu wa CCM, mmefanya makosa… Walimdanganya, lakini
majibu ya hoja aliyoijenga mwenyewe wameyapata katika uchaguzi wa
Serikali za Mitaa uliopita. Mimi nilishinda ubunge nikiwa na mwenyekiti
mmoja wa Serikali za Mtaa, sasa nina wenyeviti wa mitaa 67 kati ya 130.
“Hiyo ni ishara tosha kuwa wananiamini. Hiyo ni
ishara tosha ya kwamba nakubalika. Hayo yametokea baada ya Kinana kusema
mimi nina mwenyekiti mmoja. Nimewapa maneno ambayo hayatoki kichwani.
Hata vijiweni wanani-quote (wananinukuu). Utawasikia, hata Mchungaji
Msigwa alisema niliwaambia mimi sitawapa samaki, nitawafundisha kuvua
samaki na ndiyo maana niliwaambia mimi siyo ATM, miezi sita ya mwanzo
nilikuwa ‘unpopular. Kiongozi ni yule anayefanya mambo sahihi, siyo
mambo mazuri.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment