Pages

Wednesday, March 25, 2015

'BVR KUKWAMISHA UCHAGUZI MKUU'

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameonyesha wasiwasi juu ya uwezekano wa nchi kuingia kwenye machafuko kutokana na uchaguzi mkuu kuhofiwa kutofanyika Oktoba, mwaka huu, kinyume cha inavyotarajiwa.
Amesema hofu hiyo inatokana na taarifa kwamba, upigaji wa kura ya maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa, utafanyika Agosti, mwaka huu. Uamuzi huo unadaiwa kuchukuliwa na serikali baada ya kubaini kwamba, upigaji wa kura hiyo kufanyika Aprili 30, mwaka huu, kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete, hautawezekana.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba, tarehe hiyo inaweza kufika, huku daftari jipya la kudumu la wapigakura, ambalo uandikishaji wake kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR) umekuwa ukisuasua, likiwa halijapatikana. Daftari hilo, ambalo uandikishaji wake unaendelea kufanyika mkoani Njombe tangu Februari 23, mwaka huu, ndilo linalotarajiwa kutumika kwenye upigaji wa kura hiyo na pia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema katika mahojiano maalumu na NIPASHE jana kuwa, iwapo upigaji wa kura ya maoni utafanyika Agosti kama inavyodaiwa, basi zitakuwa ni ‘ndoto za alinacha’ uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba. Alisema itakuwa miujiza kura ya maoni itapigwa Aprili 30, kwani hadi sasa Tanzania hakuna daftari la kudumu la wapigakura, ambalo linaweza kutumiwa kufanyika mchakato huo na uchaguzi mkuu, kitu ambacho ni cha hatari.
Vilevile, alisema mpango wa kutaka daftari la zamani liboreshwe ili litumike kwenye kura ya maoni na katika uchaguzi mkuu, nao pia hautawezekani. Alisema hiyo inatokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kueleza bayana kuwa daftari la zamani limechafuka na kwa maana hiyo, halipo kabisa. Hata hivyo, alisema kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakifanya jitihada za kutaka kukutana na Rais Kikwete ili wajadiliane na hatimaye kuwa na kauli moja dhidi ya tatizo hilo, aliloliita ‘janga’.
Alisema ana amini mazungumzo kati yao na Rais Kikwete yatasaidia yote yanayowatenganisha Watanzania katika kuelekea kutekeleza mambo hayo, yarekebishwe na kuwaweke pamoja. Mbatia alisema ni jambo la kusikitisha kuona tangu Februari 23, Nec imeshindwa kukamilisha uandikishaji wapigakura katika wilaya moja (ya Njombe) , huku wilaya 132 zilizoko Tanzania zikiwa hazijafikiwa kwa mchakato huo. Alisema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uchache wa mashine (BVR kits) za kuandikisha wapigakura zinatumika hivi sasa kuendesha mchakato huo.
Mbatia alisema wakati hali ikiwa hivyo, kabla ya hapo, Februari 12, Nec ilikutana na wadau na kuwaeleza kuwa hadi ifikapo Machi 14, mwaka huu, mashine zilizosalia kati ya zile zinazohitajika zingekuwa zimekwishapatikana. Hata hivyo, alisema hadi kufikia jana mashine hizo zilikuwa bado hazijapatikana.
Alisema kati ya mashine 8,000 zinazohitajika kuandikisha wapigakura milioni 23 nchini kote, hadi sasa zilizopo ni 250 tu, nchi marafiki, ikiwamo Kenya na Nigeria zikikataa kuisaidia Tanzania vifaa hivyo. Mbali na hilo, alisema Nec pia haina rasilimali watu wa kuendesha mchakato huo kwa kutumia BVR, kwani makamishna ilionao hawana utaalamu wa masuala ya kielektroniki na teknolojia kwa jumla.
Hivyo, akaonya kuwa: “Bila kuwa na daftari taifa litaingia kwenye machafuko.” Alisema madai kwamba, uamuzi wa serikali wa kuahirisha upigaji kura ya maoni utaupa umaarufu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hayana nafasi kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na janga. “Tuondokane kujadili matukio, kwani machafuko hayatachagua huyu ni Ukawa na huyu ni CCM,” alisema Mbatia.
Pia alisema kipindi hiki siyo cha kulaumiana na kuvurugana, bali ni cha kurejesha utulivu unaoonekana kutaka kutoweka miongoni mwa Watanzania na kufanya kazi kama timu moja ya taifa. Mbatia alisema ana amini kuwa, wapo wadau ambao wana weledi mkubwa wa mambo hayo, hivyo yafaa wote wakakubaliana kushughulikia tatizo lililopo ili kulinda amani iliyopo kutoweka. “Hivyo, fikra zetu zote na mawazo yetu yote yaelekezwe kwenye jambo hili. Tukishajua tatizo tunalitafutia tiba. Tunao wataalamu na nikiwa mtaalamu wa masuala ya majanga niko tayari,” alisema Mbatia.
 
MNYIKA: JK ATEKELEZE MAKUBALIANO
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amemtaka Rais Kikwete, kutekeleza moja ya makubaliano aliyoafikiana na vyama vya siasa kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuhusu hatma ya mchakato wa katiba mpya.
Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, pia amemtaka Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, kuwahakikishia Watanzania kuwa, kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa haiwezi kufanyika Aprili 30 kupitia uzeofu alioupata katika uandikishaji wa daftari hilo unaoendelea kwa kusuasua katika mji mdogo wa Makambako, mkoani Njombe.
Mnyika alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Chadema na wenyeviti wa serikali za mitaa wanaotokana na chama hicho, jijini Dar es Salaam. Alisema serikali inapaswa kuacha kuwapa matumaini hewa Watanzania kuwa kura ya maoni itafanyika mwaka huu, badala yake inapaswa kuwekeza kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ili wananchi wachague viongozi bora, ambao hatimaye watasaidia kupatikana kwa katiba mpya inayotokana na wananchi.
“Kushindikana kwa kura ya maoni kwa ajili ya katiba mpya mbali na kupingwa na makundi mbalimbali katika jamii ni mpango wa Mungu na ameamua kuwaonyesha watawala kuwa mchakato huu wanaotaka kuulazimisha kwa njia haramu hauwezekani,” alisema Mnyika. Aliongeza: “Makundi mbalimbali katika jamii yamesema kuwa kura ya maoni haiwezekani kufanyika mwaka huu wapo viongozi wa dini kwa madhehebu yote, Wakristo, Waislamu, wametoa kauli hizo, lakini wachache waliounga mkono msimamo wa CCM wa kulazimisha kura hiyo ifanyike Aprili 30 jambo, ambalo haliwezekani,” alisema.
Alisema hatua ya kura ya maoni katika mchakato wa katiba mpya haiwezi kupigwa bila kuandikisha upya wapigakura. Mnyika alisema kauli zinazotolewa na viongozi wa serikali na Nec yenyewe zinalenga kuwalisha Watanzania matumaini hewa au kuwadanganya kwa sababu uzoefu uliopatikana katika kata za Makambako, mkoani Njombe unadhihirisha kuwa kura ya maoni haiwezekani kufanyika mwaka huu.
 
NEC: BADO TUNASUBIRI VIFAA
Nec imesema bado inasubiri vifaa  vya BVR kwa ajili ya uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu nchi nzima. Wiki mbili zilizopita Nec ilieleza NIPASHE kuwa vifaa 3,200 kati ya 7,750 vipo njiani na wakati wowote vitawasili kwa ajili ya kurahisisha uandikishaji kufanyika nchi nzima.
Hali iko hivyo, huku zikiwa zimebaki ziku 27, ukitoa siku za Jumapili na sikukuu, ambazo uandikishaji haufanyiki kufika siku ya kura ya maoni kama ilivyotangazwa na serikali. Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Lubuva alisema vifaa vipo njiani na vikiwasili uandikishaji utafanyika kwa haraka zaidi.
“Ninachoweza kuwaeleza waandishi wa habari ni kuwa vifaa vipo njiani na wakati wowote vitawasili,” alisema Jaji Lubuva, ambaye alipoulizwa lini hasa vinatarajiwa kuwasili alisema: “Umma ujue kuwa vipo njiani.” Alisema kwa sasa BVR kits 250 ndizo zinatumika kwenye uandikishaji mkoani Njombe na mara baada ya kuwasili kwa vifaa 7,750, uandikishaji utafanyika nchi nzima.
Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya wadau mbalimbali wa uchaguzi, ambao wamedai kutoridhishwa na uandikishaji wapiga kura huku msimamo wa serikali ukiwa ni kura ya maoni kwa Katiba pendekezwa ni Aprili 30, mwaka huu.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment